Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa kuchangia bajeti hii ya mwaka 2021/2022. Kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kukamata usukani wa nchi yetu na kututembeza mpaka hapa tulipofika, nchi imetulia na nchi imekuwa na maelewano mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Waziri wa fedha na mipango, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara hii kwa kuleta bajeti nzuri ambayo imekuwa ni ya kupigiwa mfano, kwa sababu hii ni bajeti ya kwanza kwa Mheshimiwa Rais Samia, lakini watu wameikubali. Mimi ni mmoja wa watu wanaounga mkono bajeti hii,na nina ushahidi wa kutosha kwamba bajeti hii imekuwa na kiasi kikubwa sana cha mambo ambayo Wabunge waliyaomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na ukweli kwamba bajeti hii itamalizia miradi ambayo ilikuwa ya kimkakati kama reli ya SGR, mradi wa umeme kule Mto Rufiji na mradi wa REA wa kupeleka umeme vijiji vyote. Vile vile bajeti hii imetafuta fedha kwa ajili ya TARURA ambazo Wabunge tumekuwa tunalia humu kwamba TARURA iwezeshwe na tumetafuta fedha kwenye vyanzo vya uhakika ambavyo tutawapa TARURA ifanye kazi ya kutengeneza barabara kwenye vijiji ambavyo hakuna barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia miradi mbalimbali ya kufua umeme, ambao umeme huo utatumika kwenye Mradi wa REA. Sasa hivi Mradi wa REA hata ukikamilika umeme utakatika kwa sababu uliopo sasa hivi hautoshi, pia miradi mbalimbali ya maji itakamilika. Kuhusu afya bajeti hii imelenga kumalizia majengo na kupeleka vifaa tiba kwenye majengo ya hospitali ambayo sasa yapo, lakini hayana vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fedha za majimbo. Hii ni bajeti ya kwanza ambayo imetupa hela mkononi Wabunge. Kwanza milioni 500 za kujengea barabara, vile vile milioni 600 za kujengea shule katika kata ambazo hakuna shule. Hapa nina maboresho kidogo, fedha hizi milioni 600 kuna majimbo mengine tayari yana shule na watapata hizo hela na kuna majimbo mengine yana kata zaidi ya tano katika kata 20 hazina shule, inakuwa tabu sana. Kwa mfano, jimboni kwangu nina kata mbili, hazina shule za sekondari. Hata hivyo, wenyewe tumeaanza kufurukuta, tumejenga kwa kutumia Mfuko wa Jimbo na michango ya wananchi. Kwa hiyo ningeomba kabisa mimi hizi hela milioni 600 nizigawe miloni 300 kila kata na tunaweza kumalizia shule ya sekondanri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lingine ambalo bajeti hii imeligusa, nalo ni kuwagusa waajiri na wafanya kazi. Katika nyanja hiyo, bajeti hii Serikali imependekeza kupunguza PAYE kutoka asilimia tisa mpaka nane. Kwa hili tunaipongeza sana Serikali yetu. Pia Serikali imependekeza kwamba waajiri wenye wafanyakazi mmoja mpaka wanne sasa wasilipe tena SDL kama ilivyokuwa zamani, tumesogeza ile idadi ya chini ya wafanyakazi kuwa 10. Sasa hii imesaidia sana na waajiri wengi watalipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna huu Mfuko wa Matibabu au Malipo kwa Wafanyakazi Wanaoumia Kazini, yaani Workers Compensation Fund, tumekubaliana kwamba na bajeti imeonyesha kwamba sasa waajiri wa sekta binafsi walikuwa wanalipa asilimia moja watalipa asilimia 0.6. Sisi tuna maoni kwamba ingefaa hizi asilimia 0.5 kwa ajili ya wafanyakazi wa Serikali au public, iwe sawa na kwa ajili ya wafanyakazi binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kabisa nina maoni machache, kuboresha tu bajeti hii ambayo nimeisifia kwa ajili ya watu wote. Maoni yangu kwanza. Ni kweli kabisa naamini kwamba VETA ingefanya kazi vizuri sana kama ingekuwa chini ya Wizara ya Kazi chini ya Waziri Mkuu, kwa sababu VETA maana yake ni kuhudumia watumishi kwa wafanyakazi wa waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napendekeza sasa Serikali ijiingize kabisa kabisa kwa ajili ya blue prints, tutekeleze mpango wa blue prints ambao ungerahisisha kufanya kazi kwa kufanya biashara yaani easy doing business hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu tozo za wafanyakazi nimeisemea, kuhusu tozo ya SDL. leo tumesimama katika asilimia nne ya mshahara wa mfanyakazi, nchi zote za Afrika Mashariki na SADC tozo hii ni ndogo sana. Kwa hiyo hii inatuongezea kuwa na gharama za ufanyaji biashara hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niongelee posho ya Madiwani ambayo Serikali inalipa, itawalipia moja kwa moja Madiwani wetu badala ya kulipwa na Halmashauri. Hii imeleta na imeibua wazo la utawala bora, maana wanaesema mtu anayemlipa mpuliza zumari, anachagua na wimbo wake. Sasa hii watalipwa Madiwani hao kwa hiyo watasimamia Halmashauri zetu vizuri. Naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina matatizo madogo jimboni, lakini sugu kabisa ni vituo vya afya. Jimbo zima lina kata 19, lina kituo kimoja tu cha afya. Nimelisema sana hili mpaka naona aibu kulirudia rudia, kama Waziri wa Afya yupo, Waziri wa TAMISEMI yupo, watusaidie kumalizia majengo kwenye kata ambazo nimezitaja; Shitage, Mabama, Ilolanguru na Usagari ambako tunajenga wenyewe kwa hela zetu za Mfuko wa Jimbo na nguvu za wananchi. Tuna shida kweli ya hospitali, tungependa sana kama Serikali itaingilia kati suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado naendelea na pongezi kwa Wizara ya Maji, imefanya kazi nzuri sana ya kugawa maji jimboni kwangu na nchi nzima. Hata juzi tumekwenda kufungua mradi huko Misungwi na Mheshimiwa Rais. Wizara hii imefanya kazi nzuri sana nawapongeza sana Mheshimiwa Aweso na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala muhimu sana la kilimo. Kilimo ndio uti wa mgongo katika nchi hii, lakini kilimo hakithaminiwi na Serikali kabisa. Wamesema Wabunge wengi hapa kwamba tunapata bajeti nzima ya Serikali kilimo kinachangia asilimia 27. Matokeo yake Serikali inawekeza 1.8 ya bajeti kwenye kilimo na tumesahau kitu kimoja kikubwa sana, nchi hii itatokea vita au ugomvi mkubwa sana kwa sababu Serikali haijaweka ardhi ya kilimo kama ambavyo tumeweka ardhi ya wanyama yaani hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, akishawekwa mwekezaji hapa anataka ekari 200 ziko wapi, hakuna. Anataka hekari 500, hakuna, anataka hekari 10,000 aweze kuweka shamba kubwa na uzalishaji wa tija, hakuna. Matokeo yake wananyang’anywa watu wenye mashamba yao kama vile sijui wamenyang’anywa na matumbo, kwa sababu hawa watu wenye mashamba yao watakula wapi, walikuwa wanalima, inachukuliwa ardhi anapewa mwekezaji. Iko haja ya Serikali sasa kuweka ardhi ya kilimo, demarcated kabisa kwamba ardhi ya kilimo ni hii, kama ambavyo tumeweka ardhi ya wanyama ni hii, itatusaidia sana kuondoa migogoro huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala hili la kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu limepitwa na wakati. Tunangoja mvua zinyeshe ndipo tuvune, kama hazikunyesha hatuvuni na hatuna simu sisi na Mwenyezi Mungu kwamba tuletee maji, tuletee mvua mwaka huu, hatujui, hata Waziri wa kilimo leo hajui kama kesho mvua itanyesha, imekuwa tu utabiri wa hali ya hewa ambao wanaona mawingu na kadhalika, hakina uwezekano wa kutoboa sisi kilimo bila ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri, Serikali ibadilike itoke nje ya box, ising’ang’anie kusukuma wakulima na pembejeo tu kwenye maji ambayo hawayajui yako wapi, wakati kila mwaka mvua inanyesha maji mengi yanapita kwenye madaraja na tunakazana kujenga madaraja tu ili maji yapite, tuzuie sasa hayo maji tufanye umwagiliaji wa kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia bajeti hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)