Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kazi nyingi ambazo anaendelea kuzifanya katika nchi yetu lakini pia hata utengamano wa taifa, kuna utulivu wa kutosha. Naompongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa ajili ya bajeti nzuri ambayo imetayarishwa na Wizara yake, Naibu Waziri pamoja na timu yake yote. Kwa kweli bajeti hii kila Mtanzania, kwa sisi tunaotoka huko nje kila mtu anaisifia. Imegusa karibu kila maeneo na matarajio ya watu; kwa hiyo watu wana matarajio makubwa sana na bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba, kutengeneza bajeti nzuri ni jambo moja lakini kutekeleza bajeti hii ni jambo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yangu kwamba bajeti hii itatekelezwa kwa ukamilifu wake. Isipotekelezwa katika ukamilifu wake maana yake pongezi zote hizi zitakuwa za bure. Kwa hiyo nakusihi sana Mheshimiwa Waziri, bajeti hii ikitekelezwa vizuri Watanzania wanakwenda kukomboka kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia habari ya barabara za vijijini (TARURA). Ninaipongeza Serikali kwa kuamuzi wa kutoza tozo la shilingi 100 kwa ajili ya kuchangia mfuko wa TARURA. Nchi hii inashida kubwa sana, barabara za vijijini zina urefu wa kilomita zaidi ya 108,000; lakini katika hotuba yako umesema ni kilometa 2,250 tu ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo utaona kuna tofauti kubwa sana. Na mimi naamini kuongezeka kwa bajeti hii kutaongeza mtandao wa barabara za kiwango cha lami katika Mfuko huu wa TARURA; kwa hiyo nakupongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi hizi za vijijini zimedumaza uchumi wetu kwa sababu kule ambako zinakwenda ndiko kwenye uzalishaji wa kilimo. Na utaona kwamba hakuna mahusiano kati ya barabara na maeneo yanayozalisha mazao ya kilimo na maeneo yenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo. Kwa hiyo mazao mengi yanaozea porini kwa sababu hakuna barabara ya kupeleka mazao kwenye maeneo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana barabara hizi fedha zitoke barabara zitengenezwe ili wananchi wanapofanya shughuli za kilimo na mazao yakipatikana yasafirishwe mara moja kwenda kwenye maeneo ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwenye upande wa kilimo. Tunaamini kabisa kama asilimia 65 ya uchumi wetu unategemea kilimo. Ningeshauri sana Serikali tujikite kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kutukomboa kwa sababu kama unafanya kilimo cha umwagiliaji unaweza kuvuna mara mbili au mara tatu kwa mwaka; Badala ya kutegemea kilimo cha mvua ambacho mnategemea kuvuna mara moja na huna uhakika kwa sababu mvua inaweza kuwa nyingi, kuna maeneo mengine mvua inakuwa hakuna. Kwa hiyo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ni lazima Serikali itenge maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na hapo ndipo kufanyike kilimo cha kutosha. Kwa hiyo naomba sana Serikali kupitia bajeti ya kilimo Wizara ya Kilimo basi tushughulike sana na kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, papo maeneo mengi yenye maji ya kutosha. Tulikuwa tunapita juzi kutoka Singida, kuna mabwawa yamezagaa huko njiani lakini maeneo yanayozunguka mabwawa hakuna hata mchicha, hakuna mtu anashughulika hata na mchicha tu pale. Sasa ni lazima tubadilishe mindset ya watu wetu, yale maji ya kwenye mabwawa yanayozagaa hovyo katika nchi yetu tuyatumie effectively. Kama ni elimu basi itolewe kupitia Wizara yetu ya Kilimo, watu wayatumie vizuri yale maji. Lakini matokeo yake yale maji mpaka yatakauka, yatatumiwa na Wanyama, hakuna mtu anayeshughulika hata kulima mboga maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo uchumi wetu hauwezi kuendelea kwa sababu hata maji yale machache tunayoyaona barabarani hayatumiki vizuri. Kwa hiyo naomba sana elimu itolewe ili wale watu wanaoishi katika maeneo yanayozunguka maeneo ya maji basi wafanya kilimo cha umwagiliaji. Lakini pia kwenye kilimo bado haitoshi kama hatutakuwa na mbegu bora. Shida kubwa ya nchi yetu hatuna mbegu za kutosha ambazo ni mbegu bora. Naomba tujikite sana kwenye utafiti, wataalam wetu watafiti sana habari za mbegu. Tunatakiwa kuwa na mbegu bora ili tuweze kupata kilimo chenye tija. Tunaweza kuwa na maji, tunaweza kuwa miundombinu mizuri ya umwagiliaji lakini kama tuna mbegu ambazo hazina tija tutaendelea kupiga mark time hatutapata mazao ya kutosha kwa ajili maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mbegu ni jambo ambalo Serikali lazima litoe kipaumbele. Mbegu inayopatikana sasa haitoshi, na hata hiyo kidogo inayopatikana inauzwa kwa bei ya juu sana ambayo watu wetu asilimia 90 hawawezi ku-afford kabisa. Kwa hiyo ni lazima tutafute mbegu za kutosha, mbegu bora, na ikiwezekana Serikali itoe subsidy ili watu wazipate katika bei ambayo wanaweza ku-afford, na hasa watu wetu ambao wako kwenye maeneo ya uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali kwa ajili ya kuwakumbuka Waheshimiwa Madiwani. Sisi wote tunatoka kwenye halmashauri zetu, tunaona namna Madiwani wanavyohangaika. Wakiitwa kwenye vikao mbalimbali wanageuka kuwa ombaomba kwa sababu hawana fedha za kusafiria kwenda wilayani. Kwa hiyo lazima either wamuombe Mbunge au nani, hii kitu inawadhalilisha Madiwani. Madiwani ni watu waliochaguliwa kama sisi na wananchi, hivyo lazima Serikali ione umuhimu wa Waheshimiwa Madiwani. Na sisi Wabunge mara nyingi tunawatumia Madiwani kutusaidia kupita kwenye chaguzi zetu, kwa hiyo tuna kila sababu ya kuwatetea. Namimi nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya uamuzi wake wa kuamua kwamba sasa walipwe kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyojua zipo halmashauri ambazo zipo hoi kabisa katika nchi hii, na hazina vyanzo vya mapato vya kutosha. Kwa hiyo kila siku Waheshimiwa Madiwani wanakwenda vikao wanakopwa. Wengine wanamaliza muda wao wanakuwa hawajalipwa posho nyingi tu, na mpaka leo wanadai kwenye halmashauri. Lakini si kwa sababu labda ya ujeuri Mkurugenzi, kwa sababu halmashauri hazina vyanzo vya kutosha. Kwa hiyo jambo hilo naomba lizingatiwe vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia upande wa afya, kuna maboma ya Vituo vya Afya, Zahanati ambayo yamekaa zaidi ya miaka mitano mpaka 15. Wakati umefika sasa Serikali iende ikamalizie haya maboma. Tuna maboma ya zahanati zaidi ya 8,000, maboma ya vituo vya afya zaidi ya 1,500 katika nchi hii. Haya yote yangekuwa yanafanya kazi huduma za afya ingeboreka Zaidi, lakini yote yapo na haya yamejengwa kwa nguvu za wananchi. Wamefika mahali wameshindwa, sasa Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuboresha ama kumalizia haya majengo ili huduma za afya kwa wananchi ziweze kuwa za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu, nataka nizungumzie eneo la Bodi ya Mikopo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, amezungumza vizuri sana, akasema mikopo wanayopewa wanafunzi si hisani, ni fedha ambayo baadaye wanatakiwa kuirudisha, na zipo taratibu za kuzirudisha fedha hizo, kwa hiyo siyo hisani. Hata hivyo idadi wanaonufaika na mfuko huu bado ni ndogo sana, idadi ya wanaobaki wanaoachwa bila ya kupewa mikopo na wakiwa na sifa ni wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana Bodi ya Mikopo ijaribu kupanua wigo. Mheshimiwa Waziri amezungumza habari ya kuwaongezea bajeti Bodi ya Mikopo, hii itasaida vijana wetu wengi kujiunga na elimu ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, utaratibu wa kuwatambua wanufaika bado mimi nauona una kasoro kubwa sana. Wapo vijana wengi ambao kweli wanahitaji na wanasifa za kupewa mikopo hiyo, lakini kwa sababu mbalimbali hawapewi mikopo. Kwa hiyo bajeti ikiongezeka kwa vyo vyote vile vijana wengi watapata mikopo na wataweza kujiunga na Elimu ya Juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nipongeze uamuzi wa bodaboda. Watu wengi wanaoishi mjini wanafanya biashara za bodaboda; na vijana wengi ndio wanaohusika. Anakuwa aidha amepewa bodaboda na mtu au yeye mwenyewe kajikusulu kanunua bodaboda. Na kwa sababu ya wingi wa bodaboda uliopo, biashara ya bodaboda bado hailipi sana. Kwa hiyo ilipokuwa inafikia hatua ya kumtoza faini ya Shilingi 30,000 kwa kosa la barabarani, sawa sawa na mtu aliyekosea anayeendesha lori haikuwa sawa kabisa. kwa hiyo nataka nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hilo na kuwapunguzia adhabu ili angalau tujaribu kuwasaidia waweze kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)