Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona nami niweze kuchangia machache niliyokuwa nayo. Vilevile namshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, aliyeniwezesha kusimama mahali hapa ili niweze kuongea. Zaidi naomba sana nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri anayoifanya na hata sisi wanawake tunajivunia kuwa wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme nawapongeza sana Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa jinsi ambavyo wameweza kuleta bajeti ambayo naamini na wenzangu wanaamini hivyo kwamba ni bajeti yenye matumaini kwa nchi yetu. Hivyo basi, napenda kuwapongeza sana na niamini kwamba kile walichokuwa wamekiandika, basi wataenda kukitendea haki ili nchi nzima tuweze kufurahia matunda ya bajeti ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisiwe nyuma sana, mimi kama mimi nilikuwa nazoea tu kusikia bajeti hii kuisoma au kuangalia katika runinga, lakini napenda pia nijipongeze kwamba ni mmojawapo sasa katika kuhakikisha kwamba bajeti hii inapita vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana niweze kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, mama ambaye amekuwa msikivu, nasi kama Wabunge hapa tulikuwa na vilio vingi ambavyo tumevisema, lakini amekuwa makini na kuvisikiliza hata kuifanya Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba yale tuliyoyasema yanakwenda kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri kwa kilio kikubwa kwanza tulicholia kwa ajili ya barabara zetu za TARURA. Ameweza kutoa fedha shilingi milioni 500 katika kata zetu, nasi kama Wabunge ambao tunakwenda kuziangalia fedha hizi kwa makini, tuweze kupitisha barabara hasa ambazo zina vilio vikubwa vijijini pamoja na mijini kwetu, sisi tunaita barabara za ndani. Mfano kama kwangu, naweza kusema kwamba barabara zile za Tandika hakika ni muhimu sana kwani tunaita Kariakoo ndogo kule kwetu Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kwamba tunamshukuru sana kwa fedha hizi. Siyo hilo tu, nampongeza kwa fedha ambazo naamini zinakuja, fedha zile za mashule kwa kujenga Shule za Sekondari katika kata ambazo zina mahitaji makubwa ya shule. Sitasita kuendelea kumpongeza mama yetu Rais kwa jinsi ambavyo hata juzi uwanja wa Mwanza kule ameongea mengi sana. Mama nakupongeza sana kwa sababu kwa hakika umetunyanyua sana wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizidi kuipongeza sana Serikali sikivu kwa kusikia hasa vijana wetu ambao wamekopeshwa bodaboda, wengine wamekuwa wakifanya kazi zile za watu wenye bodaboda, hata hizi faini zimeweza kushushwa sasa na badala ya kuwa shilingi 30,000/=, imekuwa ni shilingi 10,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu ndugu zangu, Wabunge wenzangu, nimetumwa na Jimbo langu la Temeke niwashukuru sana Wabunge wote waliolia kilio hiki na hata sasa vijana wale wanasema watafanya kazi kwa bidii na siyo tu kwamba watafanya bila makosa, lakini watatii sheria bila shuruti. Nawashukuru sana Wabunge wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ambayo wenzangu wameyaongea hapa, mimi leo nilisimama ili niweze kushukuru na kusema kwamba ahadi hizi zote zilizoweza kuwekwa hapa kwa niaba ya wananchi kupitia Wizara ya Fedha ya kwamba tunatamani kama alivyosema mwezangu hapa yasiwe katika maandishi. Sisi kama Wana- Temeke pia wananchi wote sasa hivi tumekaa macho, tunaangalia kwa macho, inawezekana mimi na wenzangu tunayasoma hapa na kuona kwamba yako kwenye maandishi, lakini wananchi wetu wako macho sasa kuangalia hivi fedha ambazo tunasema tumekwenda kuzitoa kwenye petrol, diesel pamoja na mafuta ya taa kwamba ni shilingi 100 inaongezeka, nasi tunaziomba ziende kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana sasa Wizara ya Fedha mziangalie hizi fedha na mtakapozileta hakika zije katika yale ambayo yanategemea kufanyika pamoja na hizi fedha, zisiwe tu katika maandishi lakini sisi tuko tunatoa macho sasa tuweze kuona barabara zetu kwenye elimu, afya hata dawa zinaweza kupatikana vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu kwamba Wizara ya Fedha nisikilizeni, mtakapokuja kutoa hotuba yenu ya mwisho hapa mtuambie mmeweka mkakati gani wa hizi fedha zinazokusanywa hili zitumike kwa mahitaji yanayotakiwa hasa katika majimbo yetu na hasa katika barabara pamoja na mambo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba naishukuru Serikali yangu sikivu na ninaamini ya kwamba yote waliyoyasema yatakwenda kutimia na Mungu awabarika sana. Ahsanteni. (Makofi)