Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nipende sana kumshukuru Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia kwa jinsi ambavyo anachapa kazi. Lakini Zaidi nimshukuru Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa bajeti ambayo kwa kweli mimi kama kijana najivunia na kama Mtanzania najivunia kwamba ni bajeti ambayo imeenda kuleta mabadiliko makubwa sana. Shukrani hizi nazitanguliza na quote moja kutoka kwa Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama, anasema; “Change will not come if you wait for someone or other person. We are the ones we have been waiting for, we are the change that we seek.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niseme jambo moja, kwamba Mheshimiwa Waziri you are the game changer. Wewe ni game changer kwenye siasa ya Serikali yetu kwa sababu gani, bajeti hii inatubeba Wabunge wote katika majimbo yetu huko tunakoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumekuwa tukilisubiria jambo kama hili, kuwa na bajeti ambayo ni inclusive kwa mawazo ya Wabunge, ya Mawaziri na wananchi. Ndiyo maana wakati wote Mheshimiwa Waziri wa Fedha akiwa anasoma bajeti hii hapa alisema nimeagizwa na mama tuzungumze na Waziri wa TAMISEMI, nimeagizwa na mama tuzungumze na Waziri wa Mambo ya Ndani, nimeagizwa na mama niongee na Waziri huyu; maana yake ni kwamba ni bajeti ambayo ni inclusive kuanzia Mawaziri hadi Wabunge. Hili ni jambo ambalo nasema wewe ni game changer. Kwa hiyo mimi nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nasimama kwa mara nyingine tena nikishukuru. Mimi hili ni Bunge langu la kwanza la Bajeti, lakini nilishauri mambo karibia Matano kama siyo manne ndani ya Bunge hili na yote yamependekezwa kwenye bajeti hii na yanaenda kupitishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nilishauri Serikali iondoe kodi kwenye nyasi bandia, Serikali imepokea na imeenda kulifanyia kazi. Nilishauri kwenye Bunge hili kwamba kwenye michezo ya betting, betting companies zichangie michezo kwenye nchi hii, bajeti imelichukua imeingizwa humu ndani, asilimia tano za betting companies zitakuwa zinapelekwa kwenye michezo. Nilisimama kwenye Bunge hili nikashauri kuwa gharama za bodaboda ni nyingi, mama yetu amesikia kilio cha bodaboda zimeondolewa toka elfu 30 hadi elfu 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikasimama kwenye Bunge hili tena nikashauri viwanja vyote vya mpira kwenye nchi hii viwekwe nyasi bandia. Rais akiwa Mwanza juzi ameagiza Chama cha Mapinduzi kuanzia sasa kiruhusu mchakato wa kuweka nyasi bandia kwenye taifa hili. Kwa niaba ya wanamichezo wa taifa hili nimesimama kushukuru na kusema ahsante sana. Kwa sababu haya ambayo mmeyafanya hamyafanyi kwa maslahi ya Watoto wenu mnafanya kwa maslahi ya Watanzania wote. Wanamichezo walioko huko saa hizi wanasherehekea kuona kwamba sasa mpira wao utaenda kufanyika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, masuala ya betting companies sasa yataenda kuchangia michezo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitatumia dakika nyingi sana nikuombe jambo moja tu katika wakati wako na wakati mwingine hayo umetupokea. Suala lingine nilishauri Serikali iangalie namna ya kuunda ama kampuni au wakala wa kuruhusu vifaa vya michezo vipunguzwe kodi mashuleni; mambo ya jezi na mipira, nilishauri hapa ndani ya Bunge. Na ninakusihi Mheshimiwa Waziri, ninakumbuka una ahadi kule Ruruma Sekondari, ninakumbuka una ahadi kule Kengege Sekondari. Kila Mbunge ameahidi vifaa vya michezo huko kwenye shule mbalimbali. Ukienda kwa Mheshimiwa Tulia, Mbeya Sekondari ameahidi vifaa vya michezo, ukienda kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ameahidi vifaa vya michezo kule Iringa. Kila Waziri hapa ameahidi vifaa vya michezo shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ione tija sasa kuwa na wakala maalum ambako sisi Wabunge tutaenda kununua vifaa vya michezo kwa punguzo ili nchi nzima watoto wetu wasianze kushangaa kuona jezi wakienda kwenye UMITASHUMTA, jezi wakutane nazo tangu wakiwa shuleni. Kwa sababu kwa sasa kila Mbunge anatumia fedha zake nyingi za mfukoni kuagiza vifaa vya michezo China ili aende aka- support michezo jimboni kwake. Tuliomba Serikali ihangaike. Kama tuna wakala wa mbegu kama tuna kampuni za ranchi za taifa kama tuna kampuni za ndege, kwanini tusiwe na wakala wa vifaa vya michezo shuleni ambaye atasimamiwa na Serikali? Na hivyo vifaa vitakuwa vimepunguzwa ruzuku au imeondolewa kodi ili sisi Wabunge iwe ahueni kwetu na watoto wetu waweze kupata vifaa vya michezo vingi na vya kutosheleza na hatimaye michezo ya nchi hii iweze kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina mambo mengi sana, na niwaombe watanzania kwa haya aliyoyasema Mheshimiwa Waziri tuunge mkono bajeti. Hatuwezi kujenga nchi kwa kufurahia tu kodi kupunguzwa, tufurahie kujenga nchi yetu pia kwa kulipa kodi kwa wakati na kodi ambayo inastahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niwaombe Watanzania kokote waliko yeyote anayekushauri uilalamikie bajeti hii anakupotosha, kwa sababu nchi itajengwa na wenye moyo na wenye moyo ni Watanzania wote. Kwa hiyo mimi niombe tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri, tuiunge mkono bajeti ya Serikali na tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wetu. Ameonesha njia na ameshirikisha mawazo ya Wabunge walio wengi. Wakati ni wa kwetu sisi Wabunge, tukitoka hapa twende majimbo ili tukai-support bajeti hii asilimia 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha za vijana mjini Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mama Samia wameupiga mwingi sana. Kwa sababu gani, leo hii hakuna bodaboda anapiga kelele kuhusu mambo ya bodaboda., hata traffic wenyewe wataacha kusumbua. Shilingi elfu 10 ni reasonable, kwa sababu kama basi lilikuwa linapakia watu 30, lilikuwa inapakia watu 60 analipa 30,000, boda boda anapakia mtu mmoja analipa 30,000, ile imetuonyesha kabisa sisi ni watu wa aina gani. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri you are the really game changer na kwa hili Mungu akubariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina mambo mengi, ahsante.