Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu na ninaomba nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Engineer Masauni pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu kwa jinsi anavyoendelea kuwapigania Watanzania wa rika zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nikimwangalia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na Mama Samia ninakumbuka mbali sana. Mwaka 2015 wakati wakitafuta kura walikuwa wanatembea Pamoja; mama na mtoto wote walikuwa wakiruka kwa chopa kuhakikisha Serikali ya CCM inashinda. Sasa ninaiangalia bajeti yao ya kwanza Mheshimiwa Mama Samia akiwa Rais wa Awamu ya Sita jinsi gani wanavyofanya kazi mama na mtoto, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mama Samia kwa namna alivyoshusha pressure ya wafanyabiashara kwa kuwahamasisha kulipa kodi bila shuruti. Namshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia na wananchi wamelipokea kwa furaha kubwa sana na pressure zao zimeshuka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uwezeshaji wa wanawake na vijana. Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Halmashauri zetu imehamasisha wanawake na vijana kuwezeshwa ili waweze kujiajiri hatimaye waweze kupata kipato na kuchangia kodi katika Taifa letu pale watakapokuwa wameweza kusimama vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee kuhusu wanawake wafanyabiashara wa Kariakoo. Soko la Kariakoo la vitenge limekamatwa na wanawake. Wanawake hawa walihangaika kutafuta mitaji, hatimaye wakasimama na wakaweza kuagiza mizigo kutoka nchi za nje na wamekuwa wakifanya vizuri na wamekuwa wakilipa kodi vizuri sana, lakini kutokana na kodi kutokuwa Rafiki, wamefika mahali wanashindwa kufanya biashara zao kwa sababu kodi inakuwa hailipiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sisi tumezungukwa na nchi za DRC, Zambia, Uganda na nchi zote ambazo zimetuzunguka zimekuwa zikija kuchukua biashara Tanzania, lakini baada ya kuwa kodi siyo rafiki kwa wafanyabiashara wa Tanzania wale wote waliokuwa wakija Tanzania kununua vitenge wamehamia nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma walikuwa wakilipa kodi 0.4 na wakati huo walipokuwa wakilipa namna hiyo walikuwa wanaweza kuchangia kwa mwezi shilingi bilioni 9.7 mpaka shilingi bilioni 10. Kwa maana hiyo, wafanyabiashara wa Kariakoo kila mwezi walikuwa na uwezo wa kushusha makontena kuanzia 90 mpaka 120; na kontena moja limekuwa likilipwa kwa shilingi milioni 128. Nchi jirani ya Zambia kontena hilo ambalo Tanzania wanalipa shilingi milioni 128 wao wanalipa shilingi milioni 30. Angalia tofauti iliyopo, ni karibia shilingi milioni 100 nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kugundua hivyo, nchi jirani zilizotuzunguka wameteka masoko ya Watanzania, wanaagiza biashara wao wenyewe na biashara zile zinapita kwenye bandari ya Tanzania. Wanapitisha nchini mwetu, wanazipeleka nchini kwao, baadaye zinarudi nchini mwetu kwa sababu vitenge vilivyopo Tanzania, vya kwetu sisi havina…(Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki anachokizungumza mzungumzaji, kwanza nimpongeze kwa sababu ni kweli kwamba soko la vitenge la Kariakoo limeingia mchanga. Kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maua ambayo yanatengenezwa kwenye vitenge vya Tanzania ndiyo yanaongoza kwa ubora katika East Africa na Afrika nzima, lakini kutokana na kupanda kwa kodi kutoka 0.4 na kwenda kwenye 0.6 tumepoteza kabisa soko kwa Watanzania wengi, wamekuwa stranded. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kenya, Uganda, Zambia… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga usichangie. Karibu Mheshimiwa Genzabuke, malizia.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake. Kwa maana hiyo, wapo wafanyabiashara ambao tayari wameshahama Tanzania wameenda kuwekeza nchi za nje, lakini wanawake wameshindwa kuhama kwa sababu mama ni mlezi. Mama hawezi kuhama akamwacha baba, mama hawezi akahama akawaacha watoto. Kwa hiyo, wale wameshindwa kuhama wamebaki hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kilio hiki kimfikie Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mpendwa, Mama Samia Suluhu aangalie jinsi ya kuwasaidia wanawake hawa ambao ni walipa kodi wazuri, wamekuwa wakiipigania Tanzania ili biashara hii iendelee kubaki Tanzania, Tanzania iendelee kupata kodi kupitia wafanyabiashara wa Tanzania kuliko nchi jirani kuendelea kunufaika na bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara zinapita kwenye bandari yetu zinaenda nchi za Jirani, baadaye zinarudi Tanzania. Tanzania inakuwa haiingizi mapato, mapato yanapotea, hatupati wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)