Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangi kwenye bajeti hii ya 2021/2022 katika Bunge lako Tukufu. Na mimi nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru sana Serikali ya mama Samia Suluhu Hassan ya awamu ya sita pamoja na Waziri wa Fedha na Mawaziri wote kwa ujumla kwa jinsi ambavyo wameshirikiana kutengeneza bajeti hii na kuiwasilisha kwenye Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo ninaenda kuchangia katika maeneo kadhaa, nikianzia kwenye eneo la ukusanyaji. Ili tuweze kutekeleza bajeti hii na bajeti hii iwe salama lazima Wizara yetu ya Fedha pamoja na taasisi zake zote, zikiongozwa pia na TRA, kuhakikisha kwamba mapato yakutosha yamekusanywa kulingana na bajeti yetu. Kwa sababu bajeti hii inategemea makusanyo ndipo tuweze kuteleza. Kama makusanyo hayatasimamiwa vizuri kama ambavyo wamejitahidi kusimamia ya 2021 malengo yetu haya yote tuliyoyategemea yatashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, kwa jinsi ambavyo Waziri amewasilisha, na alivyojipanga, ninaamini kazi itaendelea vizuri. Katika bajeti hii kama hatutakusanya vizuri hatutapata maji, barabara zile barabara zetu za kwenye majimbo, ukosefu wa maji, vituo vya afya na zahanati haitatelezwa. Lakini naamini Waziri akisimama vizuri, na Mawaziri wote wa idara zote bajeti itatekelezwa na hatimaye makisio haya ya trioni 36 ambayo tumekadiria kukusanya yatakusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri ahakikishe kwamba ameweka mifumo rahisi na itakayowavutia walipa ili kodi walipe kodi kwa utaratibu mzuri kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na masharti yasiwe mengi katika kulipa kodi. Kuna watu ambao wanataka kulipa kodi lakini wanapoona huo mlolongo mrefu na vikwazo mbalimbali basi wanashindwa na wanachoka kwenda kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiweka urahisi katika kulipa kodi, tuweke usawa, kwa mfano mtu anapokwenda kupeleka fedha benki mlolongo unakuwa ni rahisi kwa sababu anaweka fedha benki lakini anapotoa inakuwa ngumu. Sisi katika kulipa kodi tunaweka mlolongo mrefu. Ningeomba milolongo hiyo ipunguzwe ili walipa kodi walipe kodi ili miradi yetu iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kukusanya kuna suala la upelekaji wa fedha kwenye majimbo na halmashauri. Hili nalo Mheshimiwa Waziri tunawapongeza kwa kipindi hiki cha 2020/2021 kwa sababu mmejitahidi kwa kweli. Kwa mfano kwenye jimbo langu mmetuletea bilioni mbili na point juu, mmetupa tena milioni 500 ambayo imetolewa na Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa awamu ya sita kwa kweli mmejitahidi. lakini tunaomba basi tutakapokwenda kukusanya tujitahidi tena mara dufu kwa sababu wananchi wetu wanategemea na wanaamini kwamba pale ambapo tutapeleka fedha za kutosha kwenye miradi tuliyopanga, hiyo ndiyo ahueni na furaha; na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi itatimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata tutakapokwenda mbele ya wananchi tutakwenda kifua mbele kwa sababu tumetekeleza ilani ya 2021/2022 bila shida yoyote na watatuelewa vizuri. Kwahiyo naomba hili la upelekaji wa fedha tuhakikishe kwamba tunajitahidi kama tulivyojitahidi 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kupeleka fedha pia nizungumzie suala la uhaminifu na uhadilifu, kwa maana ya nidhamu katika matumizi. Hili suala la nidhamu na uadilifu katika matumizi ni suala muhimu na nyeti kwa sababu kama tutapeleka fedha lakini bila usimamizi tutakwenda kupata panya wanaotoboa magunia, watatoboa miradi yetu mara tutakapopeleka fedha itakuwa hatujatekeleza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tuhakikishe kwamba tumewazuia panya wasiharibu bajeti hii, tumewazua waharibifu, kwa sababu inashangaza sana na inasikitisha pale ambapo watu wanaofanya wizi, ujambazi, ufisadi na ulafi ni wale watu ambao wanalipwa mishahara, wanakaa lakini bado wanatamaa ya kuharibu bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta mtumishi amepewa gari, ofisi, watumishi, wasaidizi, kila kitu lakini bado anaungana na njama za kufanya ufisadi kwenye maeneo ya miradi naomba.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji kaka yangu anayechangia kiukweli anaongea ukweli kabisa, kwamba hii bajeti imekaa vizuri sana. Kama haitapata panya wakazitafuna hizo pesa tunazozipitisha hapa Serikali yetu itakuwa juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilikuwa nataka nimpe taarifa tu mchangiaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema, watu hawa ambao ni waharibifu tukiwaachia wakienda kukondesha bajeti hii, bajeti hii ikakonda kwa sababu panya, hatutaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Mawaziri wote, kwa sababu watatelekeza bajeti hii, wahakikishe kwamba bajeti hii haitakonda, haitakondeshwa, ili hatimaye malengo, nia na madhumuni ya kutelekeza ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika sekta za maji, barabara, elimu, afya na miundombinu vyote kwa ujumla viweze kufikiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo panya hawa tukiwaruhusu; na inashangaza, kama nilivyosema, mtu analipwa mishahara lakini bado ni mwizi na fisadi, yeye ndiye anaanzisha timu ya kufanya uhalifu. Ifike mahali sisi wote kwa ujumla wetu tupige vita rushwa, tutosheke na mishahara yetu. Kwa sababu hata ukikusanya dunia nzima, hata ukikusanya mali ngapi utakufa utaacha lakini huku umewatesa wa akina mama, hawana dawa, umewatesa akina mama wajawazito pamoja na wagonjwa wengine wakakosa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali hata milango yote ya ofisi za Serikali milangoni tuweke acha kupokea rushwa, acha kutoa rushwa. Tukienda kule msalani iwepo acha kutoa rushwa acha kupokea rushwa. Kwenye magari ya Serikali tuweke acha kutoa rushwa acha kupokea rushwa. Kila mlango wa Serikali iweke na popote pale panapotolewa huduma; hata mezani pale kama ni kwa Waziri liwekwe bango linalosema acha rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya pili nizungumzie suala la posho ya madiwani. Ninaishukuru sana Serikali kwa sababu imewakumbuka madiwani wetu na kuwaweka kwenye sehemu ya kulipa posho zao kutoka wizarani moja kwa moja. Hilo ni jambo jema sana na ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita. Hata hivyo kwa mshahara huu wa madiwani bado tunaomba Serikali iendelee kuangalia, kwa sababu kimekuwa ni kilio cha muda mrefu. Diwani huyu ndiye anayehangaika na kila kitu katika kata. Vilevile tusiwasahau wenye viti wa vijiji na vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuyaangalie maeneo hayo kwa sababu nao wanateseka sana, wenye viti wa vitongoji na vijiji na hata watendaji wetu wa vijiji ni wachapakazi kule na tunawakabidhi majukumu ya aina mbalimbali. Sehemu hii Serikali yetu imekaa vizuri sana katika masuala ya utawala, lakini naomba basi ikaangalie maeneo hayo kwa kuwa tumetoa fedha hizo za madiwani, na kama zinalipwa na Serikali Kuu naomba Shilingi 250,000 iliyobaki ikawaangalie wenyeviti wetu wa vijiji, watendaji wetu wa vijiji pamoja na wenyeviti wetu wa vitongoji ili nao waweze kuneemeka na Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri atakapokuwa ku-windup wajaribu kutoa waraka maalum wa kuhakikisha kwamba huu utaratibu wa kuwalipa Maafisa Tarafa iko Serikali Kuu lakini hii ya halmashauri itoe waraka unaosema Watendaji wa Kata walipwe kulingana na waraka huu kwenye vituo vya vitongoji kwenye vituo vya vijiji na Watendaji wa Vijiji. Hii itasaidia sana katika kuhakikisha kwamba utaratibu huo uliopangwa kwenye bajeti hii kwa watumishi wetu hawa wa chini inafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la property tax, kwa maana ya kodi ya majengo. Nilikuwa nasema naipongeza Serikali kwa sababu imekuja na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa kodi hii; na muendelee na huo utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningeomba muangalie sana hizi nyumba za tembe, kwa maana ya nyumba za udongo. Unakuta nyumba nyingine ni ya udongo na ina umeme. Je, nayo ni miongoni mwa zinazoolipa proparty tax? Hilo ni suala ambalo Waziri kama ni miongoni au kama si miongoni basi uhakikishe kwamba umeweka utaratibu wa kufanya analysis ya kutosha ili wananchi wetu wasiumie. Ukusanyaji wa kodi ni muhimu ili bajeti hii iweze kufikiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na kazi iendelee. Ahsante. (Makofi)