Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Zulfa Mmaka Omar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ZULFA MMAKA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni hii kuchangia katika bajeti yetu hii ambayo iko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala kwa kutujaalia uzima wake na uhai wake na pumzi zake ambazo hatulipii kiasi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza mama yetu mama Samia Suluhu Hassan kwa utendaji wake mzuri na umahiri wake na njia nzuri ambayo wametuonesha sisi wanawake kama tunaweza kuongoza bila ya kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwa mama angu mama Samia nimpongeze Mheshimiwa Rais wangu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kule Zanzibar na bajeti nzuri ambayo imesomwa tu hivi juzi ambayo imeleta matumaini makubwa na imeleta chachu kubwa ya maendeleo hasa katika uchumi wa blue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kaka yangu Naibu Waziri na Mawaziri wote kwa ushirikiano wao wa kutuletea bajeti hii iliyojaa matumaini ya watanzania hususan wazanzibar katika zile sehemu ambazo wametutaja na wametusema na wametuhurumia na kutuonyesha kwamba muungano huu tunazidi kuunganisha kwa mambo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuzungumzia masuala ya nyanja za kodi katika sekta ya kilimo. Nimpongeze sana Mheshimiwa mama yetu kwa kuona kwamba iko haja ya kupunguza kodi hizi katika sehemu ya kilimo pamoja na pembejeo. Wakulima hawa wataweza kulima na kupata pembejeo kwa njia nzuri na kufanya kilimo hiki bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hapo niipongeze kwa kuondoa katika kodi za masuala mazima ya uchimbaji wa madini suala hili litachangia sana uchimbaji mzuri wa madini katika nchi yetu na madini haya yataweza kuongeza pato katika nchi yetu na uchumi wetu utazidi kuimarika kwa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo naomba nichangie katika suala la biashara la Tanzania Bara na Zanzibar. Tuseme wazanzibar tumefarijika sana kutokana na imani yao ambayo tumeonyeshwa. Kulikuwa na changamoto kidogo ambazo zilikuwa zinaikabili katika suala zima la biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaumia sana pale biashara zetu Zanzibar tunapolipia mara mbili ushuru huu lakini sasa hivi tumeona kwamba bajeti hii ambayo iko katika meza zetu imeondosha changamoto hii kwa hali nzuri sana. Jambo zuri husifiwa na tunaona kwamba imani kubwa ambayo tumeoneshwa sisi wazanzibar tunaahidi kwamba tutailipa imani hii kwa kushirikiana na kuleta maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli suala hili ni zuri na sisi twaahidi kwamba tutashirikiana ila tumuombe Mheshimiwa Waziri suala hili aliangalie vizuri hasa katika bandari zetu. Watu wa bandari wanausumbufu sana katika suala hili kwa hiyo tusiichukulie tu kwamba tayari limeshawekwa lakini Mheshimiwa Waziri usimamie watendaji wako ulifatilie ili suala hili liweze kuenda sambamba na nia ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niende katika miradi ya Muungano tuna miradi mingi sana Zanzibar ambayo fedha zake zinatoka katika Serikali ya Muungano wa Tanzania kuna baadhi ya miradi hii inachelewa kutendeka kutokana na ucheleweshaji wa kusaini mikataba ama pesa wakati mwingine kusuasua katika miradi hii tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri suala hili akae tena na watendaji wake washauriane vizuri na wasimamie vizuri ili fedha hizi ziweze kupelekwa kwa wakati na miradi ile iweze kutendeka na Zanzibar ifaidike ilivyo katika mgao huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa watanzania mjenga nchi ni mwananchi kwa hiyo niwashauri sana watanzania wenzangu tuungane kwa Pamoja kulipa kodi kusimamia rasilimali za Tanzania ili ziweze kutuongezea pato katika nchi yetu. Mambo mazuri yanaletwa na mwananchi mwenyewe, tukianza kusuasua katika ulipaji wa kodi naamini kwamba yale mazuri ambayo yamekusudiwa katika bajeti hii hayatoweza kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa ushauri wangu kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu, mama yetu katuonyesha njia nzuri sana ya kuifata. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge bajeti hii ambayo ipo katika meza yetu inataka kumshusha mwanamke ndoo kichwani, bajeti inaenda kumaliza vifo vya mama na Watoto, bajeti hii inaenda kuleta madawa hospitalini, bajeti hii inasimamia wamachinga waweze kufanya kazi zao vizuri, bajeti imewasema wamama waweze kujiwezesha na wao watasaidiwa katika Serikali hii, bajeti hii inaenda kujenga barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tuipitishe kwa moyo mmoja na tuwe na nia moja na tuungane kwamba watanzania wajue kwamba Wabunge tumekusudia kupitisha bajeti yenye mambo mazuri bajeti ya kimapinduzi ambayo imetengenezwa kwa umahiri mkubwa na umakini mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)