Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchana huu, juu ya hii bajeti ya Serikali. Nami niungane na wasemaji waliokwisha tangulia kuanza kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka dira iliyotafsiriwa vizuri sana na Waziri wa Fedha na Mipango, siyo kutafsiri tu na hata kuiwasilisha kwa ufundi kweli kweli. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba umejieleza vizuri na tumekuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Waziri na timu yake akiwemo Naibu Waziri Mheshimiwa Masauni, Katibu Mkuu Tutuba, Naibu Makatibu wote watatu, Ndugu Amina Shaaban, Ndugu Adolf Ndunguru na Dkt. Khatibu Kazungu na Makamishna wote wa Wizara ya Fedha. Kwa kweli mimi naomba Waheshimiwa Wabunge wote tuiunge mkono bajeti hii kwa sababu ninaiona ni bajeti iliyoandaliwa kwa usikivu wa kiwango cha juu sana. Naomba kwa muda niliopangiwa nirejee maeneo machache, yanayoonesha kwamba tunastahili kuiunga mkono bajeti hii kwa asilimi 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza usikivu wa hii tozo ya shilingi mia kwa lita ya diesel au petrol ili kuhudumia barabara zilizo chini ya TARURA. Wabunge wote tumeonge kuhusu hali mbaya ya barabara zetu na kwa uamuzi huu, kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri mwenyewe, tutapata zaidi ya shilingi bilioni 322. Fedha hizi zikiongezwa kwenye fedha iliopo ya sasa kwa mchanganuo wa asilimia 30 kwa 40 zinazokwenda TARURA, ambazo ni bilioni 272.5 kutakuwa na jumla ya shilingi bilioni 594.7 kwa ajili ya kuhudumia barabara za Halmashauri na za jamii. Haya ni mapinduzi makubwa kufanywa, mwaka wa kwanza wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini fedha hizi zikitumika vizuri, zitasaidia sana kupunguza mfumko wa bei kwa sababu wataalamu wa uchumi wanatuambia mfumko wa bei unasababiswa na kupanda kwa gharama za chakula, imekuwa ni ada chakula Mpanda kule kiko chini sana maeneo mengine kipo juu kwa sababu hatuwezi kufika kutokana na miundombinu ni mibovu. Kwa hali hii bei ya chakula kitaifa kila mtu ataweza kuimudu na itakuwa ya chini vilevile hata maisha ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aliongea kwa uchungu hapa hali ya barabara ilivyo mbaya, wagonjwa kufia njiani, madaraja yaliyokatika hayawezi kuhudumiwa, lakini kwa fedha hii nina imani hali inaweza ikawa nzuri kwenye barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu ambalo naomba nikumbushe hapa, ni iwapo fedha hizi zitatumbukizwa kwenye mfuko wa barabara zigawanywe na Road Funds Board, au kutakuwa na sheria maalum iliyotengwa kwa ajili ya hizi fedha. Kwa sababu kama zitaingia mfuko wa barabara basi kuna umuhimu wa ile sheria ya mfuko wa barabara irekebishwe kuondoa ile uiano wa asilimia 30 to 70, na kama itakuwa na sheria yake mahsusi, zikaenda TARURA bila ya vikwazo itakuwa vizuri. Kwa hiyo naomba hilo Mheshimiwa Waziri alifikirie lisije likaturudisha kwamba sheria haijabadilishwa tutaenda kwa mgao ule wa 30 kwa 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo naliona ni mapinduzi makubwa, Waheshimiwa Wabunge wote tumelizingumza ni malipo kwa Madiwani, maeneo mengi ilikuwa ni changamoto, mbaya kabisa ilikuwa inafedhehesha. Madiwani ndiyo watunga sera kwenye vyombo vyetu vya Serikali za Mitaa, ndiyo wafanya maamuzi, ndiyo waajiri, lakini kwa kweli Halmashauri nyingi zipo chini kimapato walikuwa wanafedheheka sana na waligeuka kuwa wanyonge, wengine Mkurugenzi anaweza kuamua akasema sina hela hawalipi kwa hiyo anaweza kuwakopa ili waendelee kuwa wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa Serikali wa kuwalipa moja kwa moja hili nalo linamapinduzi sana, Madiwani wetu watakuwa na uwezo sasa hivi wa kusimamia Halmashauri zetu bila ya kushawishiwa kwa kupewa fedha. Jambo ambalo naishauri TAMISEMI yale malipo mengine ya vikao, tumeondoa kwenye posho zao za kila mwezi Serikali kuu inatoa, sasa tena tusisikie na siyo jambo jema kusikia Wakurugenzi hawawalipi hata posho zao zile za vikao, hili ni la TAMISEMI najuwa Waziri yuko makini na wasaidizi wake litatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze kwa uamuzi wa kuwapa hawa Maofisa wa ngazi za Tarafa, na Kata posho ya kuwawezesha kusafiri kwenda kuhudumia wananchi, nilitaka niseme kitu lakini sasa ndiyo kimetoka hicho cha shilingi laki moja. Kule kwenye ngazi ya jamii ukienda kwenye Kata kuna Maafisa Elimu Kata, zamani tukiwaita waratibu wa elimu Kata, wao wanapata posho ya shilingi laki mbili kwa mwezi, na wanapewa vyombo vya usafiri pikipiki ili waweze kuzitembelea Kata zao. Sasa Afisa mwenye Tarafa nzima anapewa shilingi laki moja, lakini siyo jambo baya maana ndiyo tumeanza, tuone umuhimu wa kuiboresha kwa miaka ijayo ili kuwawezesha hawa watu kufanya majukumu yao vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la ulipaji wa kodi ya majengo kupitia umeme. Ninajua yapo maamuzi ya kisera yalishafanywa na Serikali zetu ziliyopita na hii ya sasa, kwamba kuna watu walishasamehewa hata kulipa kodi za majengo wakiwemo watu wazima, wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huu unless Wizara ije na utaratibu, sheria au kanuni zake zikae vizuri. Je, watu wenye umri mkuwa ni namna gani watakaokuwa exempted, vinginevyo kwa vile wana nyumba za kutumia umeme ikiwa generalized ina maana hata hawa ambao tuliowasamehe, watalazimika kulipia kodi za majengo kupitia umeme. Kwa hiyo hili nalo tumuombe Waziri kwenye sheria au kanuni ile aliweke vizuri sana, kwa sababu wananchi wameshtuka wanadhani watabanwa kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo nataka kulisema kama ushauri kwa Serikali, ili uchumi ukue kwa kiwango tunachotaka Serikali ikubali kuajiri watumishi hasa wa kada muhimu. Muda wangu mwingi nimefanya kwenye utumishi nimeufanyia kwenye sekta za Serikali za Mitaa. Ninafahamu kuna kada muhimu sana kule ambazo zinaupungufu mkubwa wa watumishi. Moja ni Internal Auditors, maeneo mengi Internal Auditors hawapo na hawa ndiyo wanafanya ile preliminary audit kabla CAG hajaingia. Hasa kama hawa hawapo na ndiyo wadhibiti wa mwanzo itakuwa ni changamoto, kwenye Local Government hakuna Wahandisi, Quantity Surveyors hawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilidhani Serikali ifanye kazi ya kuchambua zile kada muhimu ambazo zikiwepo zitasaidia kusimamia uchumi tunaotaka ukue, pia tutaimarisha utoaji wa huduma bora kwenye mamlaka zetu. Kwa maoni yangu nilidhani kada hizi tatu nilizozitaja tungezipa kipaumbele cha ajira ili waweze kusaidia kusukuma mbele Serikali zetu za Mitaa na Serikali Kuu kwa wale ambao hawana ajira hizi, vinginevyo naunga mkono hoja hii na tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri akafanye kazi yake kwa mwaka ujao. Ahsanteni sana. (Makofi)