Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nikushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili bila kuwasahau wananchi wangu wa Newala ambao wamenifanya niwe katika jengo hili, nawashukuru. Niwaambie kwamba waendelee na maandalizi ya msimu wa korosho wa 2016/2017 ambapo wamebakiza miezi miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kutoa mchango wangu kwa Wizara hii, nianze kumpa pongezi Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchapa kazi nzuri. Pia nimpe pongezi Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. Vilevile niwapongeze Mawaziri wangu na niwaambie kwamba nawapongeza sana lakini waendelee kuchapa kazi pamoja na ugumu wanaoupata katika bajeti hii, wao waendelee tu hivyo hivyo na sisi tutaendelea hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukakosa kila kitu maisha yakaendelea, lakini huwezi kukosa afya maisha yakaendelea maana huo utakuwa ndio mwisho wa uhai wako. Hii inaonesha umuhimu wa Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua nia nzuri ya Serikali yangu kwamba sera ya Chama cha Mapinduzi ni kujenga vituo vya afya kwa kila kata na kujenga zahanati katika kila kijiji. Pia kutoa maisha bora kwa watumishi wote ambao watakuwa katika hivyo vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikumsikia Mheshimiwa Waziri ambaye ndiye mwenye dhamana akizungumzia kuhusu mpango wa kujenga vituo vya afya. Maana nilitarajia Mheshimiwa Waziri angekuja na mpango mkakati wa kuonesha kwamba je, hiyo sera yetu ya Chama cha Mapinduzi ya kujenga vituo vya afya kila kata utakuwaje na kwa maeneo yapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matibabu ya wazee na tumeanza kutoa michango ya matibabu ya wazee tangu tukiwa Madiwani karibu miaka mitano au sita huko nyuma, kila siku tumekuwa tukizungumzia kwamba sera ya wazee inatayarishwa na ipo mezani. Sisi ambao tulikuwa tunapita kunadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tulikuwa tunawaambia kwamba Mheshimiwa Magufuli akishapita basi tunatarajia kwamba matibabu kwa wazee yatakuwa bure. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hakuja na mpango mkakati wa kuonesha wale wazee ambao hawana uwezo watatibiwa vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa hivi wakati umefika kuwa na mkakati kuhakikisha wale wazee ambao wapo katika vijiji maana yeye amezungumzia wale wazee waliopo katika vituo kwamba wanatoa vyakula na kutoa huduma za kimsingi lakini Serikali ina mpango gani kuhusu wale wazee ambao hawapo katika vituo vya kulelea wazee? Vijijini ndiko ambako kuna wazee wengi ambao kwa kweli wengine hawana uwezo, hawana hata pesa ya kuweza kununua dawa. Kwa hiyo, ni wakati umefika Serikali kuona hawa wazee ambao hawana uwezo ni nani ambaye anaweza akawalipia hizi bima za matibabu ili na wao waendelee na maisha kwani sote hapa ni wazee watarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata kule ambako kuna vituo vya afya vichache hakuna watumishi katika vituo hivyo. Mimi natokea katika Wilaya ya Newala, nina vituo vya afya viwili lakini nina kata 22 ambako kuna vijiji zaidi ya 146 lakini hatuna watumishi katika vituo hivyo vya afya. Vituo hivyo vya afya vilijengwa early 1970’s wakati Waziri wa Afya akiwa Mheshimiwa Nangwanda Sijaona lakini vilijengwa jengo tu lakini hakuna zile huduma za mama na mtoto, ina maana sehemu ya akina mama kujifungulia hakuna. Kwa hiyo, sisi tunapata matatizo kwani akina mama hawa wanajifungulia kwenye chumba kidogo hivyo kukosa uhuru na kushindwa kujifungua kwa nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hao watumishi wachache waliopo hawana sehemu ya kuishi. Mheshimiwa Waziri hakuja na mkakati wa kuonesha kwamba hawa watumishi wachache waliopo katika hivi vituo vya afya watajengewa nyumba ama wataboreshewa vipi makazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningemuomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atueleze vile Vituo vya afya vya Kitangali na Chihango ambavyo vilijengwa miaka ya 70 ambavyo vilishindwa kumaliziwa na Serikali za awamu mbili au tatu ambazo zimepita, Serikali hii ina mpango gani wa kuweza kuzimalizia ili ziwe na sifa ya kusema kweli kwamba hivi ni vituo vya afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu dawa au tiba tunazozipata hospitalini maana tunapokwenda tunakosa dawa lakini unapokwenda kununua katika maduka ya dawa unakuta dawa ambazo zimeruhusiwa kuingia hapa nchini ni dawa kutoka India tu. Ina maana kwamba wanaotengeza dawa ni watu kutoka India pake yake katika dunia hii na watu wote wananunua dawa kutoka India? Huko India kuna kitu gani, ina maana Wazungu wao wananunua dawa huko? Inasemekana kwamba magonjwa mengi ya ini na figo yanatokana na matumizi ya dawa ambazo hazikidhi viwango. Ina maana sisi tunakula dawa nyingi ambazo zinakosa viwango na ambazo zipo chini viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inavyosemekana baadhi ya dawa kutoka India zinakosa vile viwango na ndiyo maana watu wengi wanatumia zile dawa kwa muda mrefu bila kupata unafuu.
Kwa hiyo, naomba kama kuna dawa zinapatikana katika nchi zingine ambazo zina viwango vya juu basi Serikali ifanye mkakati wa kuingia katika hilo soko ambalo nchi zingine au nchi za Ulaya au soko la Ulaya wanaenda kununua hizo dawa siyo kufanya masihara au mchezo na maisha ya Watanzania. Maana nchi bila afya njema haiwezi kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza awali kwamba unaweza ukakosa kila kitu, ukakosa barabara, ukakosa huduma ya maji lakini ukikosa afya njema hilo Taifa haliwezi kuwa na nguvu. Naomba Wizara hii ijikite katika kuhakikisha kwamba dawa ambazo tunanunua ni zile ambazo zipo katika soko la awali au dunia ya kwanza ndizo wanazokula na sisi tule hizo ili tuwe na afya bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine tumeambiwa hapa kwamba bajeti ambayo ilikuwa imetengwa mwaka jana ni asilimia 100 lakini iliyofika kule ni asilimia 39, tatizo ni nini? Kama Wizara zingine zimekwenda kule asilimia mpaka 70, afya tumeifanyia masihara. Jamani tuache kufanya masihara na afya zetu, afya ni jambo la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuhakikishe kwamba hao vijana ambao hawajaajiriwa waajiriwe ili wawepo katika hivi vituo vya afya. Mbona Wizara ya Elimu imeweza japokuwa kunakuwa na upungufu lakini ule upungufu wa Wizara ya Elimu hauwezi kufananishwa na Wizara ya Afya. Wizara ya Afya ni kweli kabisa hasa katika wilaya au mikoa iliyoko pembezoni kule hakuna kabisa watumishi. Unamkuta mtumishi au nesi, yeye ndiye anayekupokea, anaandika cheti, ndiye anayekupa dawa. Hivi inawezekana vipi ukapiga kona wewe mwenyewe na ukaenda ukafunga wewe mwenyewe, inawezekana hiyo?
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri afanye tathmini hasa kwa hii mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi hii. Kwa mfano, sisi Wilaya ya Newala ina Hospitali ya Wilaya pale lakini wale watu wanaokuja kutibiwa wengine wanatoka Msumbiji. Pamoja na kuwa na hiyo Hospitali ya Wilaya lakini nina vijiji karibu 146 na hiyo Town Council yenyewe ina vijiji karibu 80, je, vinatosha?
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.