Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuamsha asubuhi ya leo tukawa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuipongeza hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hotuba ya bajeti ya Serikali na mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi mbalimbali anazozifanya katika kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele kukuwa katika uchumi pamoja na kuinua maisha ya mwananchi mmoja mmoja katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi, kwa juhudi zake mbalimbali anazofanya katika kuhakikisha Zanzibar inakwenda mbele na inasonga mbele kiuchumi na kimaendeleo pamoja kunyanyua hali za wananchi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha Naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya na mashirikiano ya pamoja hadi kufikia kutuletea bajeti nzuri ambayo inaenda kutatua changamoto za wananchi mbalimbali, changamoto za wakulima, wavuvi, wafanyabiashara na wananchi kwa jumla nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wizara yake kwa kututambua sisi asasi zisizo za kiserikali - NGOs akatuweka katika bajeti yake kwamba na sisi tumechangia katika uchumi wa Taifa kwa kweli taasisi zisizo za kiserikali nazo zinafanya kazi kubwa katika kunyanya maisha ya mwananchi, kutatua changamoto za wananchi, kutatua changamoto za ajira, lakini kuinua uchumi wa nchi ni vyema sasa michango yetu nayo ikatambuliwa na dhamani gani tumewekeza katika mazingira yote, katika maeneo yote ya sekta zote za uchumi maendeleo ya jamii na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupongeza bajeti hii kwa kuondoa ushuru katika mazao ya Kilimo, Ufugaji, Viwanda na Biashara. pamoja na kuondoa ushuru huu wa forodha, tusisahau kuzingatia mazingira katika bajeti zetu zote tuhakikishe kwamba pamoja na mambo yote tunayoyafanya kuilinda nchi yetu na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, na katika bajeti imo, Mheshimiwa umetenga fedha kwa ajili ya mazingira, ni vizuri sana tukawa na fedha zetu za ndani za kuwekeza katika kuhifadhi mazingira yetu ya nchi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napenda kuchangia kwamba pamoja na mambo yote tunayoyafanya ya kuwekeza lakini tutenge ardhi katika maeneo muhimu ikiwemo uhifadhi wa misutu, uhifadhi wa uoto wa asili, uhifadhi maeneo tengefu kwa ajili ya kulinda mazingira ya nchi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napongeza Serikali kwa kuondosha ushuru katika uwekezaji wa mbolea na viwanda vya mbolea ni kweli itasaidia kutatua changamoto za mbolea katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nashauri katika uwekezaji huo huo wa mbolea tusisahau mbolea zetu za asili kwa maana ya kuhifadhi ardhi yetu iendelee kudumu na kutumika milele na vizazi vijavyo. Naamasisha pia katika mipango inayokuja tuwekeze pia katika kilimo hifadhi na kilimo hai, kilimo hifadhi na Kilimo hai kitakwenda kulinda afya ya mimea yetu na mazao tunayozalisha hayatakuwa hayana chemical, lakini pia tutahifadhi ardhi na udogo wa nchi yetu kwamba usiendelee kuharibiwa na chemical za viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea katika hicho hicho kilimo, kuna kilimo cha mazao ya bustani na mboga mboga, kilimo hiki kimetokea kuwa na soko kubwa duniani na tunaingiza fedha nyingi za kigeni kupitia kilimo hiki cha bustani na mboga mboga.

Narudia kusisitiza kwamba Kilimo hiki kuna baadhi ya maeneo wanakata miti mikubwa wanaondosha uoto wa asili badala yake tunakwenda kupanda bustani na mazao ya mboga mboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tulitizame kwa upana wake pia na ndiyo nikasisitiza kwamba tuweke na maeneo ya kuhifadhi uoto wa asili na misitu kwa maana kila bidhaa zikiwa nyingi huko duniani na sisi kilimo tutaongeza kupanua maeneo, tukipanua maeneo tunakata miti ya asili, tunakata na misitu, lakini tunapanda mboga mboga, naomba hili tuliweke angalizo katika mipango yetu ya maendeleo kwa kila mwaka, na hii nakuja pale kusisitiza kwamba kupima maeneo yapi ya Kilimo, yapi ya ufugaji, yapi ya viwanda, na yapi ya uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea naipongeza Serikali kwa kuondoa ushuru wa ongezeko la thamani katika taa za solar, pamoja na vifaa vya kutengenezea solar, lakini katika hapa nilikuwa nauliza Serikali inijibu kwamba katika kusamehe hizi tozo na kodi inaunganisha na ile mitambo ya kusukuma maji katika visima vyetu kama hicho hakipo nashauri Serikali mitambo ya kusukuma maji katika visima vyetu viondolewe kodi. kwa sababu uwekezaji wa visima vya maji kwa kutumia diesel na petrol tumegundua kwamba ni gharama kubwa ya uendeshaji na hivyo mzigo unamwelemea mwananchi anayetumia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali yetu, ni ya Rais wetu ni kuhakikisha mwanamama anamtua ndoo kichwani lakini wananchi kwa ujumla wanapata maji safi na salama. Kwa hivyo tukipunguza kodi kwenye vifaa vya kusukumia maji katika visima vya maji itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa visima vya maji na maji yatapatikana kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye Sekta ya uvuvi naipongeza Serikali sana, sasa tumejipanga katika uvuvi, uvuvi wa bahari kuu na Serikali ina mpango wa kununua meli za uvuvi. Ushauri wangu pamoja na kujiingiza kwenye uvuvi huo mkubwa kwa kununua meli uvuvi wa Bahari Kuu, uvuvi wa Kisasa tusisahau wavuvi wetu wadogo wadogo, wavuvi wetu wadogo wadogo na wao waende sambamba na ukuaji huo wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bado zana zao ni duni, zana zao hafifu mvivu anapokwenda baharini anajua kwenda lakini uhakika wa kurudi hana kwa sababu atakachokutana nacho baharini hajui kama ni mawimbi makali au ni dhuruba, au atapata samaki au hapati, kwa hivyo uchumi huu mkubwa tuwachukue wavuvi wetu wadogo wadogo ambao wametusaidia mpaka kufika hapa kwamba uvuvi bado Tanzania upo tuwawezeshe kwa zana za kisasa ili na wao tuwainue kiuchumi lakini pia waongeze mapato ya Taifa na waweze kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nasema hivi naipongeza sana Serikali tumuunge mkono Rais wetu atuletee maendeleo nampongeza Makamu wa Rais, nampongeza Waziri Mkuu, nampongeza Rais wa Zanzibar kwa juhudi kubwa anazofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo na sisi wananchi tuko bega kwa bega kuhakikisha maendeleo haya tunayapata yanawafikia wananchi wetu, yanatufikia na sisi wenyewe na vizazi vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ahsante sana, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)