Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara yetu hii. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya toka achukue madaraka haya ya Urais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejadili na kupitisha bajeti mbalimbali za Wizara hapa na michango mbalimbali tumechangia. Ni dhahiri bajeti hii ambayo tunataka tuipitishe hapa imetokana na Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa maana yale yote ambayo tumeyajadili ndiyo yamekuja kujumuishwa katika bajeti ya Wizara hii ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumza sana suala zima la TARURA iongezewe fedha. Tumeona katika Bajeti ya Wizara ya Fedha kila Jimbo limepewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kwenda kukarabati miundombinu ya barabara. Tumechangia kuhusiana na namna gani ambavyo tunaweza tukaongeza fedha kwa ajili ya kuzipeleka TARURA. Tumetoa michango mbalimbali, wapo waliogusia kuhusiana na ongezeko la fedha katika mafuta, wapo waliochangia katika miundombinu ya mawasiliano na bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha, vyote hivyo vimejumuishwa. Tafsiri yangu ni kwamba bajeti hii iliyoletwa hapa imezingatia michango ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno mengine bajeti hii ni bajeti yetu, ninachotaka kusema tunazo kazi za kufanya, zipo kazi kwanza kwa sisi Wabunge, kwa sababu yaliyoletwa ndiyo tuliyoyataka, kazi yetu ya kwanza kama Wabunge tunatakiwa twende tukawaelimishe wananchi wetu, twende tukawaelimishe wananchi wetu ili bajeti hii iweze kutekelezeka. Ipo sheria ile ya property tax, ambayo ni wajibu wa kila mwenye jengo kuilipia kodi ya majengo, tumekuwa zamani huko tukikusanya kwa kupitia halmashauri zetu, tukaenda TRA, lakini ufanisi ukawa mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumekuja na mbinu mbadala ya kukusanya kupitia mita za LUKU. Tutakapoenda kuwaelimisha wananchi wetu, nini kinachoenda kutendeka hatutapata tabu kwenye ukusanyaji wa hizi fedha za property tax. Madhalani mwenye nyumba anayepangisha nyumba kwa mwezi shilingi 300,000/= tukiweka utaratibu mwananchi akajua kwamba kwenye 300,000/= hii kwa kila mwezi 1,000 ni kodi ya majengo, kwa hiyo, ni rahisi unaenda kulipa 299,000/= (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, ni kama vile kwenye majumba haya yaliyopangishwa yapo mashimo ambayo yanabeba maji taka, maji taka yale ni jukumu la mwenye nyumba kuyanyonya pale yanapojaa. Sasa kwenye mikataba ni namna ya kukubaliana tu. Aidha, kwenye kodi yangu utakata kiasi kadhaa ili shimo likijaa uwezekunyonya au nipe kodi yangu shimo likijaa nitakuja kunyonya, kwa hiyo, kubwa hapa kinachoitajika ni elimu kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa bajeti hii sisi ndiyo tumechangia kwa kiasi kikubwa mpaka hapa tulipofikia, ninaamini bajeti hii pia ni yawananchi, kwa sababu Wabunge tuliochangia hapa tumewawakilisha wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa upande wa pili kwa Mawaziri, tunaenda kuwahamasisha wananchi wetu ili waweze kulipa kodi, boda boda wapunguze makosa na mambo mengine, lakini pale fedha zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo tuwaombe sasa na ninyi Mawaziri mchukue wajibu wenu kupeleka fedha hizi katika hii miradi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ile miradi michango yetu na elimu yetu tunayoenda kuitoa kwa wananchi tutawaambia, gharama hizi za simu zinaenda kupelekea tupate fedha kwa ajili ya kukarabati barabara, kwa ajili ya kumalizia miradi mikubwa ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninyi mawaziri msipopeleka fedha katika hiyo miradi maana yake sasa pamoja na elimu tuliyoitoa kwa wananchi mnaenda kutupalia makaa kwa wananchi wale, kwa hiyo upande wa mawaziri kwa maana ya Serikali na ninyi tunawaomba mtimize wajibu wenu kuhakikisha miradi ile yote iliyotengewa fedha inaenda kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri mambo machache katika masuala mazima ya barabara hasa barabara zile zinazomilikiwa na TARURA. Huko nyuma halmshauri nyingi hasa zile za Dar es Salaam zilikua zinatenga fedha kwa ajili ya barabara zaidi ya bilioni 4 nakumbuka halmashauri ya jiji la Ilala na Temeke zilishawahi kutenga katika miaka mbalimbali. Hebu sasa tuangalie Serikali kama halmashauri hizi huko nyuma zilikuwa zinauweozo wa kutenga hizo fedha hebu angalieni Serikali namna ya kuzikopesha halmashauri hizi fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; halmashauri ya Temeke Ilala na hizi nyinginezo zikakopeshwa labda bilioni 20 kila moja kwa ajili ya kwenda kukarabati barabara, halafu kila mwaka mkawahambia muwe mnalipa labda bilioni tatu tatu, naamini baada ya miaka mitano barabara zitakuwa zimetengenezwa na fedha zitakuwa zimerudi katika mfuko mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ulizungumza katika hotuba yako kwamba majadiliano yanaendelea kuhusiana na mradi huu wa DNDP, kwa Dar es Salaam mradi wa DMDP ni muhimu kweli kweli. Tunaomba sana muharakishe mazungumzo katika mradi huo wa DMDP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho posho la wenyeviti wa Mitaa na madiwani, Mheshimiwa Waziri umezungumza halmashauri zile 16 zitaendelea kulipa kwa mapato yake ya ndani. Sisi tuwaombe sana Dar es Salaam tuna mizigo mikubwa sana na sisi Dar es Salaam mchukue gharama hizi Serikali Kuu muweze kulipa ili fedha hizi sasa ambazo wamekua wakilipwa sasa hivi madiwani ziende zikalipe wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa ambao kiukweli wamekuwa na hali mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumpongeza Waziri wetu wa TAMISEMI, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameonyesha kwa kiasi kikubwa ushirikiano mkubwa na Waheshimiwa Wabunge. Kila Mbunge hapa ameandikiwa barua na Mheshimiwa barua na Mheshimiwa Waziri aeleze vipaumbele vyake katika ujenzi wa shule za Sekondari, Wabunge wote tumeandika na zimemfikia waziri naamini ile migongano ya kugombania Sekondari ikajengwe wapi itakuwa imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe na mawaziri mwingine wote tuunge sasa juhudi alizozifanya Waziri wetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu na sisi kwa kufanya hivyo naamini mambo mbalimbali yataenda kubadilika katika halmashauri zetu, barabara zitajengwa, mashule yatajengwa, zahanati zitajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)