Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipatia hii nafasi. Vile vile nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia sisi hapa angalau kupata uhai na afya njema, tunasema ahsante Mungu. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya kama mama mwenye upendo kwa kuhakikisha maendeleo ya Tanzania yanapatikana na juhudi kubwa anazozifanya na sasa hivi hata sisi akinamama tunapata nguvu kuwa tunaye Jemedari wetu ambaye anapambana na uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitazungumzia upandw wa Bandari, katika njia kuu nne za uchumi mojawapo ni bandari. Toka enzi ya ukoloni walifanya utafiti mkubwa sana wa kuona mafanikio ya bandari zetu hasa Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga na Bandari ya Dar es Salaam; nitajikita katika Bandari ya Tanga na Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona leo hizi bandari zikiwa zimeachwa hazina kazi ya kufanya wakati tunahangaika na mizigo katika bandari hii ili kuleta pato na kodi kubwa katika uchumi wa nchi yetu tutaanzia na bandari wa Mtwara, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutoa tamko kuwa Korosho zote zinazotoka Mikoa ya Mtwara na Lindi zinakwenda katika Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio makubwa sana kuifanya ile Bandari itakuwa inafanya kazi lakini vile vile sio zao la korosho tu tunataka hata kahawa ya Mbeya, kahawa ya Ruvuma yote iende katika Bandari ya Mtwara. Nilikuwa naangalia kilometers za kutoka Ruvuma mpaka Bandari ya Mtwara. Kutoka Ruvuma-Songea mpaka Mtwara ni saa 8.53 na kutoka Ruvuma au Songea mpaka Dar es Salaam ni saa 14.53 ina maana ni masaa 15 ukiachilia mbali foleni za Dar es Salaam lakini utashangaa kahawa ya Mbinga badala ya kuipeleka Mtwara inapelekwa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijauliza urasimu huu unatokana na nini kuifanya nchi inadumaa kibiashara? Si hivyo tu Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Ruvuma tunapakana na nchi jirani zikiwemo Malawi, Zambia pamoja na Kongo DRC. Mizigo ya Kongo DRC imehama kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya urasimu, lakini tujiulize kwa nini kuwepo kwa urasimu wakati kuna eneo ambalo ni karibu Bandari ya Mtwara ambayo katika miaka ya nyuma ilikuwa inafanya kazi kubwa sana na ilikuwa inaheshimika kwa watu, ilikuwa iko busy, lakini kwa urasimu uliokuwepo Dar es Salaam, kwa sintofahamu iliyokuwepo Dar es Salaam wameifanya bandari ya Mtwara kuwa dormant. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ufuta unatoka Nanjilinji, ufuta unatoka Newala unakuja Dar es Salaam, lakini yote ni biashara tu kutaka kuleta mileage na kumkandamiza mkulima katika zao la korosho zao la ufuta, zao la kahawa zao la cocoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hayati Rais Mkapa alianzisha Mtwara Corridor kuhakikisha kuwa mazao yote ya Mkoa wa Katavi, Rukwa, Ruvuma, Mbeya, Lindi na Mtwara yote inatumia Bandari ya Mtwara. Kumetokea kidudu gani? Ameturoga nani mpaka kuifanya hii bandari isifanye kazi? Kutokana na urasimu, tunaona leo nchi zote za jirani zimekimbilia Beira Mozambique. Beira ukiiangalia inapakana na South Africa. Hivi jamani ifikie mahali tubadilike Watanzania, tusiendelee kulalamika. Tunahitaji mifumo ambayo watu wanataka kuileta Tanzania yenye maendeleo ili maendeleo haya yaonekane. Wenzetu wale waliokwenda kule, hawakwenda hivi hivi, kuna vitu tumewafanyia ambavyo havikuwafurahisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaona mkonge unatoka Tanga unapelekwa Dar es Salaam; kahawa ya Kilimanjaro inapelekwa Dar es Salaam; mazao ya Babati Mkoa wa Manyara yanapelekwa Dar es Salaam; Tanga iko wapi? Hivi leo tunazungumza Bandari ya Tanga haina mapato, siyo kwa kuwa haina mapato, Dar es Salaam pana ubadhirifu mkubwa, pana urasimu mkubwa mpaka umeifanya Bandari ya Dar es Salaam kuonekana kama ni bandari ambayo haina hadhi na heshima kwa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri wa Fedha akae na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, tujiulize maswali mengi, kwa nini inatokea hiyo hali? Tuna Kamati zetu za Bunge; Kamati ya Miundombinu, Kamati ya Bajeti, tuachane na masuala ya kukaa mezani, twende kwenye site. Unda tume itakayoonyesha kuwa inataka kuisaidia bandari. Leo bila kuwa na uchumi haiwezekani. Tunapata aibu kubwa, wenzetu wanatujadili katika Bunge letu, wanasikiliza maoni yetu, wanayafanyia kazi. Sisi tunakaa humu ndani tunaongea sana, tunatoa mawazo makubwa sana Wabunge, mawazo yetu hayafanyiwi kazi, matokeo yake ni urasimu. Urasimu huu umetufanya tuwe katika uchumi wa kati, lakini ilibidi tuwe katika uchumi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungukwa na nchi ambazo wakiitumia bandari hizi nyingine, tutatoka kiuchumi, lakini tuko wapi? Tunadhalilika, tunaaibika kwa ajili yetu wenyewe kwa sababu hatujipangi. Huwa nafika mahali najiuliza, hivi watendaji hawa wa bandari hawaoni bandari ya Mtwara kama ni bandari nzuri? Bandari ambayo ina kina? Nataka nijue kwa nini tunapata hasara na bandari? Mtwara tunakosa ajira kwa sababu hakuna kazi inayofanyika Mtwara. Ajira hamna. Tunakosa ajira Tanga; tungeifufua uchumi mkubwa sana katika mikoa hiyo miwili; Tanga na Mtwara na majirani zao wote wangeondoka kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Mheshimiwa Waziri atakapotaka ku-wind aniambie kama majibu hayana maana nataka nichukue shilingi mnijibu hapa kuna nini? Wanasema sababu za msingi kwamba hakuna makasha. Hivi kweli tumebinafsisha section ya container terminal tumewapa TICTS, kwa nini TICTS anaing’ang’ania Dar es Salaam? Kama kazi imemshinda kwa nini asije kutuambia? Tunajikuta tumekaa, makontena yamefika pale yanatolewa, rushwa zote ziko katika Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka sasa hivi, tukitoka hapa tuwe na muda maalum maana yake hatuna time frame kuwa tukitoka hapa tuliangalie Bandari ya Mtwara, tuiangalie bandari ya Lindi na Kamati zote mbili hizi ziende katika eneo. Mimi sitoi amri maana amri anayo kiti, lakini naona kabisa tuko katika muflisi mkubwa na tukiendelea hivi wageni wetu wote majirani zetu watahama katika bandari hizi na uchumi wa bandari yetu utatokomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye issue yangu ya pili ya viwanda. Tumevifunga viwanda kwa muda mrefu, hakuna maneno yanayozungumzwa humu ndani. Leo tunangojea kuletewa mafuta kutoka nje. Jiulize mbegu za pamba zinazolimwa katika mikoa ya kanda ya ziwa zinafanya kazi gani? Vile viwanda kwa nini mnavifunga mpaka leo? Kwa nini havifunguliwi? Tunajikuta tunaenda kukaa bandarini, kungojea mafuta kutoka nje, aibu hii kwa nchi hii itaisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Mtaka ameonyesha uzalendo wa hali ya juu sana kutaka kufufua zao la Alizeti. Nami kama mwanamke na wanawake wote Tanzania nzima tumuunge mkono Mheshimiwa Mtaka, wanawake wote Tanzania nzima tulime angalau eka mbili za alizeti ili kuhakikisha aibu hii ya kuagizia mafuta nje itokomee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka ni-declare interest, mimi mwenyewe ni mlimaji wa alizeti. Nalima alizeti, Lindi inastawi alizeti, tukitoka hapa ni kwenda Lindi kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Baada ya miaka miwili Tanzania hii hakuna tena kuagizia mafuta ya chakula kutoka nje. Mafuta ya chakula yatoke hapa hapa, kila Mbunge atoke hapa akiwa na neno moja; tunakwenda kulima Alizeti. Hakuna tena Mbunge kwenda kule, hapana; aonyeshe mfano; hawa Wabunge wote waonyeshe mfano, kila mmoja awe na eka tano tano katika eneo lake, alime Alizeti. Hii isiwe hoja ya Mheshimiwa Riziki, iwe hoja ya Kitaifa ili tukitoka hapa tuwe na legacy.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RUZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)