Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunipa nafasi kusimama ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Masauni, pamoja na watendaji wote kwa maandalizi mazuri, pamoja na Mawaziri wote kwa Wizara mbalimbali ambazo zilikuwa msingi wa kuandaa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kazi nzuri anayofanya. Waziri Mkuu amekuwa champion wa mazao mbalimbali ya kimkakati, utamuona kwenye mazao ya korosho, pamba, alizeti na mkonge. Katika u-champion wake umesababisha Serikali kuleta marekebisho mbalimbali ya tozo kwenye mazao hayo ili kulinda uwekezaji wa ndani na kuwawezesha wakulima. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi anazoendelea kufanya. Na kutokana na uwajibikaji wake unaoendelea, na matokeo mazuri ya bajeti iliyowasilishwa, imenifanya nikumbuke maneno aliyoyasema kwenye hotuba yake baada ya kuapishwa tarehe 19 Machi, 2021 pamoja na huzuni aliyokuwa nayo, Mheshimiwa Rais alisema yafuatayo: nanukuu “Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya yamejidhihirisha kwa kazi mbalimbali zinazoendelea. Sambamba na hilo kwenye ukurasa wa sita wa bajeti aliyowasilisha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amenukuu ahadi ya Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan ya kudumisha mazuri ya awamu zilizopita kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya. Kwa kazi zinazoendelea tumemuona kwenye ujenzi wa SGR, uwekaji wa jiwe la msingi kipande cha Mwanza – Isaka, tumemuona akishuhudia mikataba ya ujenzi wa meli tano Mwanza jioni hii. Tumemuona kwenye uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu yote haya yanadhihirisha ahadi yake ya kuendeleza mema yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala ya kuleta mengine mapya ambapo ndipo nitakapojielekeza, napenda niipongeze Serikali kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kuamua kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi zaidi ya trilioni nane kwa utaratibu wa non-cash special bond isiyotumia pesa, haijapata kutokea. Wastaafu wa nchi hii wanakwenda kupata ahueni hata sisi watoto wa wastaafu tunashukuru kwa hatua hii ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Serikali imekuja na ubunifu wa kuangalia vyanzo vingine vya mapato kwa kuwa na mtazamo wa kuja kutumia masuala ya Euro bond, pia kwa kujielekeza Serikali kufungua soko la ndani la hati fungani kwa wawekezaji wa nje, Serikali kuanzisha bima ya afya Watanzania wote, Serikali kuamua kulipa posho za madaraka kwa Watendaji wa Tarafa na Kata, Serikali kuanza kuzipa mitazamo mipya Halmashauri zetu za Majiji na Manispaa kutumia masuala ya hati fungani katika ku-finance miradi yao ambayo inakwenda kupunguza mzigo wa Hazina kutoa pesa kwa ajili ya Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee katika hilo, nipongeze ubunifu wa kupendekeza vyanzo vya mapato kuongeza Mfuko wa TARURA kwa ajili ya barabara zetu. Hapa nishukuru kwa kiasi cha bilioni nne na milioni mia tano ambazo Mkoa wetu wa Pwani tumezipokea na pendekezo la bilioni 322. Niwaombe Watanzania barabara za vijijini ni kila kitu zinasafirisha malighafi, zitawezesha viwanda vyetu, zitapunguza gharama za uzalishaji, zitawawezesha akina mama kufika kwenye vituo vya afya, zitapunguza gharama za usafirishaji. Kwa muktadha huo naomba nishukuru kwa kusema kwamba barabara ya Chalinze – Nsigi – Talawanda – Bago inakwenda kupata faida hii. Barabara ya Lugoba – Mindukene – Talawanda – Magulumatari, barabara ya Kibiti – Mkongo – Mwaseni inaenda kupata faida ya hela hizi. Barabara ya Bungu – Nyambunda; barabara ya Kimanzichana – Mkamba – Panzui – Msanga, maeneo ya Mkoa wa Pwani ndiyo maana tuna sababu ya kuunga mkono bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa sababu Serikali imekuwa sikivu. Kamati yetu ya Bajeti imependekeza mambo mengi lakini kati ya hayo pamoja na Wabunge wote Serikali imechukua zaidi ya asilimia 70 ya mapendekezo hayo. Hii inaonesha namna gani Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na timu yako, mkiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mmeweza kumshauri vizuri Mheshimiwa Rais wetu, naye amekubali mapendekezo hayo leo yapo ndani ya Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la miradi ya maji; pendekezo la kuongeza tozo kwenye masuala mazima ya mawasiliano kwa ajili ya kusaidia miradi ya maji, naomba Watanzania tuliunge mkono hili jambo kwa sababu maji nayo ni uhai, maji ni kila kitu. Sambamba na hilo, ninaomba tu kutoa ushauri kwenye suala zima la nia ya Serikali ya kufuta msamaha kwenye suala la taa za solar. Katika hili niiombe Serikali yangu Sikivu ilitazame tena hili. Kwa sababu yapo maeneo bado yanatumia umeme wa jua na bado yapo matumaini, kwa mfano maeneo ya Visiwa vya Kibiti, maeneo ya Mbwela Mashariki, Mbwela Magharibi, Maparoni, Salale na Mkuranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Visiwa vya Kwale, Koma, tuna Visiwa vya Bwejuu, Jibondo, maeneo ya Mafia bado tunasubiri umeme wa solar. Kwa hiyo niombe sana tozo hii, vifaa vyote vya umeme viendelee kusamehewa kodi ili kuweza kuwafanya Watanzania wenzetu wanaoishi visiwani waweze kupata huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa mkakati wake wa kuweza kutaka kupandisha vyeo watumishi wa Serikali. Mmetenga bilioni 400 kwenye bajeti kwa ajili ya kupandisha vyeo watumishi 92. Niwaombe tu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Mchengerwa kuzisimamia pesa hizi zitumike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo utaratibu mara nyingi maafisa utumishi wamekuwa wakichelewa kuwapandisha watumishi vyeo, badala yake hela hizi unapofika mwisho wa mwaka zinakuwa zimesalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niunge mkono hatua zote za Kiserikali za kufanya maboresho ya kodi mbalimbali zenye nia ya kulinda viwanda vyetu. Sisi Mkoa wa Pwani tunashukuru ulindaji wa viwanda vya marumaru, vipo viwili tu nchi nzima ambavyo ni kiwanda cha Keda Chalinze na kiwanda cha Goodwill Mkuranga. Tumeona namna ambavyo Serikali mmetia mguu katika marumaru inayouzwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile hiyo haitoshi kwa upande wa akina mama tunashukuru tozo mbalimbali ambazo zimeondolewa kwenye masuala ya kilimo cha mbogamboga na matunda, kwenye masuala ya usindikaji wa maziwa, kwenye masuala ya bima ya mifugo, kwenye masuala ya mazao mbalimbali ambayo ama kwa hakika tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimalizie kwa kuwapongeza Kamati yetu chini ya Mwenyekiti kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti hapa ndani. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hatua yake ya kuupa msukumo mradi wa kusindika gesi asilimia Mkoa wa Lindi, mradi wa Mchuchuma Liganga, mradi wa bomba la mafuta, yote haya ambayo yamewekewa hatua za kikodi ili miradi hii iweze kuchangia ajira kwa Watanzania, iweze kuchangia mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Balozi wa kuhamasisha kodi, nimalizie kwa kuwaomba Watanzania kulipa kodi kwa sasa hivi na hatua zinginezo. Niwaombe tuendelee kulipa kodi ni umeme, imepunguzwa sasa hivi 27,000 maeneo yote, kodi ni elimu kwa vijana wetu, Serikali imeongeza zimefikisha bilioni 500 kila kijana wa Tanzania atakayekuwa na sifa za kwenda chuo kikuu atapata mkopo, hiyo ndiyo kodi ya Watanzania. Pia kodi ni barabara kila kijiji cha nchi hii kitapata barabara. Kodi ni madawa tumeona mtazamo wa Serikali wa kumaliza maboma 8,000 na vituo vya afya 1,500 pia kuongeza madawa bilioni 263 zimetengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe wafanyabiashara, mazingira wezeshi katika bajeti hii yameainishwa, mmepunguziwa viwango mbalimbali vya kodi, mmepunguziwa urasimu mbalimbali lakini kubwa Serikali imeweza kutatua mfupa wa asilimia 15 ya gharama za sukari ya viwandani. Wafanyabiashara mmeachiwa ili kuongeza ukwasi kwa uchumi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sote kwa pamoja tumuunge mkono jemedari wetu, mweledi, mchapakazi, mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na tunakuombea dua, Mwenyezi Mungu akujalie na tunaamini utatufikisha pale panapostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)