Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na namshukuru Mungu kwa kuendelea kunipa uwezo wa kushiriki katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu, mama ambaye ameufahamu wajibu wake kwa nafasi aliyopewa kwa kuwaangalia wanawake wa Tanzania kwamba wana upungufu wa damu na hivyo kuweza kuhamasisha katika Mkoa wa Dodoma na watu wamekwenda kujitolea damu. Tunaamini kwamba mama yetu Mama Samia Suluhu ataendelea kutambua na mikoa mingine kwamba wanawake wengi wanakufa kila siku kwa ajili ya upungufu wa damu pale wanapokwenda kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi hizo, sasa naomba nijikite katika kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Afya. Natokea Mkoa wa Mwanza ambapo tuna Wilaya ya Ilemela ambayo bado ni changa ilianzishwa mwaka 2012. Kwa masikitiko makubwa sana Wilaya ya Ilemela hakuna Hospitali ya Wilaya. Kwa bahati mbaya sana Halmashauri ya Ilemela wakati imekatwa kutoka kwenye Halmashauri ya Jiji la Nyamagana iliomba shilingi milioni 300. Baada ya kupatiwa fedha hizo Halmashauri hii imeweza kutumia shilingi milioni 193 kuanzisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana kwa kuanza na jengo la emergence. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilipokuwa nikitazama kwenye vitabu mbalimbali vya bajeti ya Wizara ya Afya sijaona ni wapi ambapo Serikali imetenga pesa kwa ajili ya kuweza kutusaidia Wilaya ya Ilemela kujenga majengo yetu ya Hospitali ya Wilaya ya Ilemela. Hivyo basi, namuomba Waziri wa Afya, dada yangu pale, aweze kutusaidia kiasi ambacho kimeombwa na Halmashauri ya Ilemela shilingi bilioni mbili na milioni mia tatu kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ilemela. Nitamuomba Waziri wetu wa Afya anaporudi kujibu hoja basi atusaidie kutueleza ametenga kiasi gani au Serikali imetenga kiasi gani kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea suala la upungufu wa dawa. Tumeona katika Mkoa wa Mwanza limefunguliwa duka la MSD, lakini kwa masikitiko makubwa sana dawa katika lile duka hakuna. Namuomba Waziri aweze kufanya uchunguzi kwamba katika hilo duka ni dawa gani zimepelekwa au hizi dawa zimeishia wapi. Yawezekana dawa zimepelekwa lakini zimebaki zina-hang somewhere na hazijaweza kufika katika hili duka la MSD ambalo limefunguliwa pale katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, Mkoa wa Mwanza hakuna mashine za CT-Scan. Watu wengi wamekuwa wakifa kutokana na matatizo ya ubongo. Tunafahamu kabisa CT-Scan ina uwezo wa kutambua mgonjwa ana matatizo gani kwenye kichwa ili kuweza kuepuka mgonjwa kupata stroke. Tumeweza kuwa na wagonjwa wengi sana ambao wanapata stroke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri atakapokuja aje na majibu sahihi tena ya uhakika kwamba katika Mkoa wa Mwanza hususani Hospitali ya Bugando ambayo imesemekana kwamba kuna CT-Scan lakini ninao uhakika wa asilimia mia moja, hata sasa hivi Waziri akisema tupande ndege twende Mwanza au twende kwa basi au kwa gari gani lakini twende Mwanza sasa hivi tukakague Hospitali ya Bugando CT-Scan hakuna. Naomba sana Wizara yetu iweze kuwa makini katika kuangalia vifaa ambavyo vinakuwa vinapelekwa je vimefika au havijafika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukazia kuomba CT-Scan katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Sekou-Toure. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy aliahidi na kusema kwamba CT-Scan itapelekwa mara moja iwezekanavyo. Hivyo basi, nakuomba Waziri wakati ukiangalia bajeti yako utusaidie pale Mwanza utupelekee CT-Scan katika Hospitali yetu ya Rufaa pale Mwanza ya Sekou- Toure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza inazo kata 19. Mheshimiwa Rais alitoa ari kwamba kuwepo na vituo vya afya katika kila kata, lakini pawepo na zahanati katika kila kijiji. Kwa masikitiko makubwa sana Wilaya ya Ilemela tunazo kata kumi na tisa lakini tuna vituo vya afya vitatu kikiwepo Kituo cha Sangabuye, Bugogwa pamoja na Karume. Kwa bahati mbaya hivi vituo vyote vitatu havina hadhi ya kuitwa vituo vya afya. Ukiangalia katika Kituo cha Karume hakina huduma nzuri, vitanda hakuna, kuna vitanda viwili tu, hakuna kitanda cha akina mama kujifungulia, huduma ya kufanyiwa upasuaji akina mama pia hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Ummy kwa kuwa na wewe ni mwanamama na unafahamu kabisa kina mama tunapopata matatizo wakati wa kujifungua, utusaidie. Kwa kuwa umesema akina mama wengi wanapoteza maisha wakati wakipata haki yao ya msingi ya kutuletea watoto hapa duniani, naomba utusaidie basi kutuboreshea vituo vya afya hivi vichache tu ambavyo vipo katika Wilaya ya Ilemela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namuomba pia Waziri aweze kuisaidia Halmashauri ya Ilemela kwani ni change, kila inapotenga pesa kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma bora za afya haiwezi kufanikiwa kwa sababu inakuwa ina majukumu mengi na hivyo kuielemea halmashauri. Hivyo, namuomba Waziri aweze kutusaidia basi Wilaya ya Ilemela tuondokane na hivi vituo vitatu basi walau atuongezee vituo viwili ili tuweze kusogeza huduma karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia leo nilikuwa sina mengi sana lakini naongelea pia kuhusiana na suala zima la Benki ya Wanawake. Naomba Serikali iweze kuiangalia hii Benki ya Wanawake. Mheshimiwa Mbunge ambaye amechangia katika hili suala la huduma ya Benki ya Wanawake amesema kwamba Serikali imetenga shilingi milioni 900, ninasita mimi katika kusoma bajeti ya Serikali, nimeona Serikali imetenga shilingi milioni 500 tu na siyo shilingi milioni 900. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri Ummy aliwahi kusema kwamba atatoa shilingi bilioni mbili kila mwaka. Kwa mwaka huu wa fedha kama Serikali imetenga shilingi milioni 500 tu sioni kama tutafikia malengo ya kuweza kuiendeleza Benki hii ya Wanawake hapa Tanzania. Ukiangalia benki hii sasa hivi ina mtaji wa shilingi bilioni 20 tu peke yake. Kwa hiyo, kama katika mwaka huu watafanikiwa kuongeza hizo shilingi milioni 500 ambazo zimetengwa bado benki hii haiwezi kuwasaidia wanawake. Hakuna matawi mengi hapa nchini, kuna matawi machache sana ambayo yako kwenye mikoa michache nadhani ni mitano au nane...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.