Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya na hatimaye wananchi wote watanzania wote kwa ujumla wameridhika na mwendo kasi anaokwenda nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kwamba tumuombe Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema aendelee kututumikia sisi wananchi ambao kwa sasa tunaimani kubwa sana kwa yale yote ambayo ameanza nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya hapa ndani ya Bunge, lakini vilevile amekuwa ni mwepesi pale anaposikia kuna tatizo basi anakwenda haraka sana na kwenda kulitatua tatizo lile ambalo sisi kama Wabunge huwa tunatoa miongozo humu ndani na mwisho wa siku inawezekana taarifa ikawa ya uwongo au ya kweli lakini alikuwa mtu mwepesi wa kwenda kulishugulikia tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tatu naomba niwapongeze sana mawaziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu namfahamu vizuri sana ni mchapakazi na mzalendo lakini Mheshimiwa Engineer Masauni ambaye ni kijana mwezangu tumekuwa tukifahamiana kwa kweli ni wazalendo wawili ambao wamekidhi kushika nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja tatu lakini moja nimekuwa nikilia ndani ya Bunge Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumekuwa tukipitisha bajeti kila mwaka kuhusiana na uwanja wa ndege wa Sumbawanga Mjini, uwanja ule una faida kubwa sana kwetu lakini mwaka juzi nilipiga makofi hapa nikapiga kelele na hatimaye nikaahidiwa kujengewa uwanja wa ndege na bajeti ikapita, mwaka jana vivyohivyo na mwaka huu Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu ameisema, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameitaja tena kaitaja mara mbili uwanja wa ndege wa Sumbawanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu nipate uhakika tu kutoka kwake wakati anakuja kutujibu mwaka huu ni kweli tutafanikiwa kujengewa uwanja wa ndege hilo nataka nilipate kwa sababu juzi tumeenda kumzika mzee wetu Mheshimiwa Marehemu Mzee Mzindakaya tulikuwa na Mheshimiwa Spika tumepata shida sana kutua katika uwanja ule. Na yeye mwenyewe Mheshimiwa Spika akaridhika na akaahidi ndani kwa wananchi pale kwamba kwa mwaka huu wa fedha atajitahidi kupambana kuhakikisha kwamba uwanja wa ndege ule unajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe sana kama una viwanja kumi unataka kujenga mwaka huu kiwanja namba moja kiwe kiwanja cha Sumbawanga Mjini ni aibu kubwa tunaposafiri sisi kutoka hapa mpaka Mpanda wakati Mpanda imezaliwa kutoka Mkoa wa Rukwa wana uwanja wa ndege wa lami Sumbawanga hatuna uwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Songwe wameweza kupata uwanja wa ndege kabla ya Sumbawanga kwa hiyo utaangalia kero tunayoipata sisi Wabunge, lakini na wananchi pamoja na Mheshimiwa Rais mwenyewe wakati anasafiri kuja kwenye kampeni kero kubwa…

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa!

T A A R I F A

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimpe mzungumzaji taarifa kwamba ule Mkoa wa Songwe huko Mkoa wa Mbeya na sio Mkoa wa Songwe kwa hiyo hata sisi Mkoa wa Songwe tunahitaji bado kiwanja ahsante (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hilaly.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naipokea taarifa lakini nataka niseme ukitaka kujua kero hiyo waulize viongozi waliopita Mkoa wa Rukwa wanashuka Mbeya, kutoka Mbeya uwanja wa Songwe mpaka uikute Sumbawanga kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga kuna matuta zaidi ya mia 250 na hayo matuta kwa bahati mbaya sana Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi hayuko hapa, lakini Mheshimiwa Kamwele ambaye alikuwa Waziri pale aliahidi mbele ya marehemu Mheshimiwa Rais John Pombe Mafuguli kwamba ndani ya miezi mitatu atakuwa ameondoa yale matuta, yale matuta ni kero kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukuombe kama matuta hayawezekani kuondolewa uwanja wa ndege iwe kipaumbele cha kwanza mwaka huu tujengewe uwanja wandenge ili uweze kurahisisha usafiri wa kwenda maeneo yale. Maeneo ya Rukwa yana vivutio vingi sana vya utalii lakini hatuwezi kupata watalii kuja kule wakiangalia kero ya usafiri ya kutoka Dar es salaam mpaka uikute Sumbawanga kwa hiyo utakuta unachenji karibuni mara tatu mara nne kubadilisha usafiri ili uweze kufika Sumbawanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa uzalendo wenu kwa uchapakazi wenu, kwa urafiki wenu baina nyie na mimi mwaka huu ule uwanja utajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili hoja yangu ya pili ni kuhusiana na property tax, Serikali ina nia njema sana na naunga mkono zoezi hilo lakini linanipa changamoto kidogo nikasema nijaribu kuchangia bajeti hii ni nzuri lakini nikasema nichangie kwa sababu ya wasiwasi na wasiwasi ni akili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunachaji kupitia kwenye hizi LUKU za TANESCO lakini bahati mbaya kuna nyumba nyingine kiwanja kimoja zimejengwa nyumba nne na kila nyumba moja ina LUKU ya kwake sasa sijui kama tutakuwa tunalipa property tax au tutakuwa tunalipa kila mpangaji ana lipa ile kodi nilitaka nijue nifafanulie kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimejikuta Dar es Salaam pale kuna mtu ana apartments zaidi ya 20 au 30 na kila mtu ana LUKU yake. Sasa ile property tax maana yake ni nini? Ni kodi ya jengo au ni kodi ambayo kila mpangaji anatakiwa alipe? Hilo unatakiwa unipe ufafanuzi kidogo kwa sababu nimekaa nikiwaza sana sipati majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo haliniingii akilini. Nimekuwa nikilalamika hapa Bungeni na kwenye Kamati nilipokuwepo. Kuna hawa watu wanaotengeneza LUKU kuwauzia TANESCO. Nitatoa mfano wa Kampuni wanatengeneza LUKU wanawauzia TANESCO, baadaye wanakuja kutengeneza sub meter, inatengenezwa na huyo anawauzia wananchi ambao ni wawekezaji wanaojenga apartments hizi, wale wanafunga LUKU zao wenyewe, wananunua umeme kutoka TANESCO wanawauzia wananchi wale ambao ni wapangaji, wao wananunua kwa shilingi 380 kwa uniti lakini wao wanawauzia shilingi 500 kwa uniti moja, sasa ninataka nijue je, Serikali imeruhusu wafanyabiashara kuuza umeme ambao unazalishwa na TANESCO? Ninachokijua mimi ni kwamba mfanyabiashara au mwekezaji anaweza akazalisha umeme akawauzia TANESCO na TANESCO wajibu wake ni kuwauzia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zimeibuka kampuni nyingi na kwa bahati mbaya sana kampuni hiyohiyo inatengeneza tokens inauza bila Serikali kujua. Ile kodi anayouza kwa faida anamlipa nani? Mheshimiwa Waziri wa Fedha jambo hili liangaliwe sana. Watu wa TANESCO wanafahamu na hii ndiyo biashara yao baina ya TANESCO na hao ambao wanauza umeme kwa wapangaji wadogo wadogo.

Nitakutolea mfano, mtu ana jengo lenye kama apartments kumi, ananunua umeme wa TANESCO anafunga LUKU ya TANESCO moja halafu anachukua sub meter anafunga. Wale waliofungiwa sub meter wananunua tena token ambazo Serikali au TANESCO hawafaidiki na chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo kuna vitu viwili kwanza wanavunja sheria, lakini la pili, wanatengeneza faida. Je, ile faida tunawajibikaje sisi kama Serikali tunapata wapi kodi kutokana na hilo jambo? Mheshimiwa Waziri nikuombe, kama utapata nafasi mniite niwaeleze kwa sababu jambo hili nimekuwa nikilifuatilia sana ni wakwepaji wakubwa wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu lingine ni kwamba kwenye nyumba hizi nyingine kama National Housing, tunafungulia luku za TANESCO ambazo kila mwananchi aliyepanga atalipa moja kwa moja property tax kupitia luku. Je, hawa waliofungiwa sub meters wanamlipa nani hiyo kodi ya pango? Tunaijua? Hatuijui! Ipo kwenye mfumo? Haipo kwenye mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo nataka niseme liangalie hili, TANESCO wanafahamu tatizo hili na tumekuwa tukihoji sana, nani kawapa leseni ya kuuza hizo tokens? Na watengenezaji wapo. Wale wafuatilieni muone miaka mitano hii hiyo biashara waliyokuwa wanaifanya wamemlipa nani kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niipongeze Serikali imeweza kuangalia Madiwani wakasema wanaweza wakalipwa moja kwa moja kutoka Wizarani. Tumeangalia Makatibu Tarafa, tutawalipa laki moja kutoka Wizarani, lakini tumeacha changamoto moja ya Watendaji wa Kata ambao na wenyewe tumewaongezea posho shilingi laki moja, lakini umetoa maelekezo kwamba shilingi laki moja hizi zitalipwa moja kwa moja na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kutengeneza tatizo lingine. Watakopwa wale jamaa mpaka mwisho, na hakuna Mtendaji wa Kata atakwenda kumfuata Mkurugenzi wake akadai malimbikizo ya madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninataka niseme kwamba huu mfumo ambao tumeuanzisha mwanzo kwamba Madiwani watalipwa moja kwa moja kutoka Hazina na Makatibu Tarafa watalipwa posho ya shilingi laki moja, na Watendaji ambao tumewaongezea shilingi laki moja walipwe moja kwa moja kupitia Hazina. Tukiwaruhusu wapewe na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani hizo hela hawatazipata kamwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, hilo ninakuomba kwamba kama kuna uwezekano basi na hizi posho za Watendaji wa Kata zihamishiwe moja kwa moja Hazina ili waweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ulikuwa ni huo. Lakini kubwa ni suala la TANESCO na LUKU na hizi sub meters ambazo zinasambazwa kwenye apartments nani anawajibika katika hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)