Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi nami niweze kuchachangia bajeti hii. Jambo la kwanza nianze kabisa kwa kuunga mkono bajeti hii ambayo kwa kweli ni nzuri sana na yenye matarajio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, kwa kweli Mungu awabariki, mnafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Awamu ya Sita kwa namna alivyosikia kilio chetu, alivyosikia kelele zetu na kuamua kuja na bajeti ambayo inaenda kujibu yale yote ambayo tulimwomba. Katika bajeti hii tumefurahi kuona kwamba kwa mara ya kwanza tunakuja sasa na chanzo kingine kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vijijini na mijini. Kwa kweli tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaenda kujibu hoja kubwa iliyokuwa inawasumbua Wabunge kwa muda mrefu kwamba tunaenda kutekeleza huduma ya bima kwa wananchi wote. Wabunge hawa walikuwa wanapata shida sana, wanapigiwa simu kila kona kwa ajili ya kutoa fedha kuwasaidia wananchi kwenda kupata matibabu. Sasa hii tukiitekeleza, itatusaidia sana kujibu zile hoja zetu. La tatu ni mikopo ya elimu ya juu na ya nne ni miradi ya vielelezo ambayo inaenda kutekelezwa. Hivi vyanzo kwa kweli ni vizuri sana. Kwa namna bajeti ilivyo, kwa namna alivyoileta, kwa kweli inatia moyo sana na inaleta matumaini makubwa sana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu tulishatengeneza dira ambayo inaisha mwaka 2025 ambayo inataka maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo tuliweka vigezo vyetu. Hapa takwimu zinaonyesha mambo mbalimbali ambayo Serikali imefanya. Nataka niseme kitu kimoja, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Serikali ya Awamu ya Sita na Awamu Tano kwa kazi waliyoifanya. Kwa sababu kwa mara ya kwanza, naona kilimo kimeweza kukuwa zaidi ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Kwa sababu uchumi ulikua kwa asilimia 4.8, kilimo kilikuwa kwa asilimia 4.9. Hii ni mara ya kwanza, haijawahi kutokea. Kwa kweli hii tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaangalia pia mchango wa kilimo kwenye uchumi, umechangia asilimia 26.9. Sasa hizi fedha, nikizungumzia kilimo, tukazungumzia viwanda, ndiyo msingi mkubwa na ndiyo nguzo na ndiyo vitu ambavyo tumevipa kipaumbele katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwa mfano, viwanda vilikua kwa asilimia 4.5, mchango wake kwenye pato la Taifa ulikuwa asilimia 8.4, lakini ukiangalia mchango wa sekta nyingine; maji ilikuwa ni 0.5, umeme 0.3 na afya 1.4. Kwa hiyo, ina maana kuna sekta za muhimu ambazo zinachangia katika uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nitoe takwimu fupi. Ukiangalia ukuaji wa uchumi huu ambao tunao wa asilimia 4.8 bado wananchi wa kawaida hawawezi kuuelewa. Kwa nini? Kwa sababu mfumuko wa bei ni asilimia 3.3. Ongezeko la watu (population) ni asilimia 3.2. Ukizijumlisha kwa hesabu za kawaida unapata asilimia 6.5. Sasa kama hizo zote zinachukua asilimia 6.5 na uchumi unakuwa kwa asilimia 4.8 maana yake wananchi hawawezi kuona matokeo chanya ya ukuaji wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo basi, lazima tuweke jitihada za kuongeza ukuaji wa uchumi, ukue zaidi ya asilimia 6.5 ndipo wananchi wa kawaida tutakapokuwa tunasema uchumi umekua na wataona kweli umekua kwa sababu hata mifukoni kwao utakuwa unaonekana. Bila hivyo itakuwa haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna umaskini bado ni asilimia 25.7. Riba kwenye mabenki ni asilimia 15.75, bado riba ziko juu. Ndiyo maana nampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Awamu ya Sita kwa hotuba aliyoitoa kule Mwanza na hatua alizozisema kule Mwanza alipokuwa anafungua jengo la Benki Kuu, ndiyo msingi mkubwa wa hii bajeti. Ameagiza kwamba anataka riba kwenye mikopo ishuke na bila riba kushuka hatuwezi kujenga uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linaendanda sanjari na hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Waziri wa Fedha amesema, hii hotuba lazima tufunge mikanda, nami nakubaliana kwa sababu ametekeleza sera zote mbili, anazitumia kwa wakati mmoja katika kuhakikisha anajenga uchumi. Anatumia Government expenditure na taxation, vyote amebana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida ukibana, matokeo yake ni kwamba uchumi unaweza ukadorora. Sasa ili kusiwe na mdodoro wa uchumi lazima Benki Kuu ije na sera za fedha za kuhakikisha riba kwenye mabenki zinashuka ili kuhakikisha mzunguko wa fedha unaongezeka. Sasa hili naamini litakaa vizuri na Benki Kuu watakaa vizuri, kwa sababu kazi ya Benki Kuu ni kuangalia kila jambo ambalo Serikali inafanya na wao wanalisimamia kwa kutekeleza sera za fedha kwa kuangalia ile riba na mzunguko wa fedha. Hilo naamini wata-balance na ndiyo hapo uwekezaji na uchumi wetu utaweza kukua. Wasipofanya hivyo kutakuwa na mdororo wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya msingi ambayo nafikiri, kwa sababu hotuba hii imejibu karibu vitu vyote vingi, naomba nipendekeze mambo yafuatayo ili yamsaidie Mheshimiwa Waziri na kuhakikisha kwamba tunaenda sasa, tukimaliza hii miaka mitano, tunafika mahali pazuri zaidi. Jambo la kwanza napendekeza, Mheshimiwa Waziri ni vizuri ukarudisha ile Tume ya Mipango ambayo ilikuwepo. Kazi yake iwe sasa ni kufikiria vipaumbele, kuangalia vitu ambavyo nchi inaweza ikafanya, kuangalia namna ufuatiliaji na tathmini inavyotakiwa kufanyika ili utekelezaji wa bajeti na location ya resources ifanyike sawa sawa. Naamini hii tume itasaidia sana; na hii ndiyo takuwa na dialogue kubwa na kuwafanya watu wote waweze kushiriki katika mjadala mpana wa namna ya kujenga uchumi wa nchi yetu; (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ukiangalia sekta ya kilimo, ukiangalia viwanda, ukiangalia kwenye biashara, utaona tija bado iko chini sana. Mpaka sasa hivi hatuna chombo chochote katika nchi hii kinachozungumzia masuala ya tija, namna ya kuongeza tija, namna ya kuhakikisha kwamba tunapandisha uongezaji wa tija katika uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, nashauri mwangalie uwezekano wa wa kurudisha Baraza la Taifa la Tija ili lisaidie katika uchambuzi na kuhamasisha na kuwa na kampeni kali ya kuhamasisha na namna ya kuongeza tija katika kilimo, kwenye mifugo, uvuvi, viwanda, na kwenye huduma mbalimbali za uzalishaji. Hiyo itatusaidia sana, itatupeleka mahali ambapo ni pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, tunazungumzia ujenzi wa SGR ambao utaenda kuchochea uzalishaji na kujenga uchumi wa nchi yetu hii. Nami napendekeza ile TAZARA upande wa nyanda za juu kusini, tunaitegemea sana. TAZARA ile mpaka sasa hivi ina uwezo wa kufanya kazi vizuri, lakini hatuna mabehewa ya kutosha na hatuna menejimenti ya kutosha. Kwa hiyo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri mkaimarisha menejimenti ya lile shirika, mkaongeza mabehewa, yatachangia kwa kiwango kikubwa sana katika uchumi wa nyanda za juu kusini na hivyo tutakuwa tunaenda sambamba na huu ujenzi wa SGR ambayo tutajenga katika maeneo mengine. Nilidhani hiki ni kitu muhimu sana.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga, kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba unavyozungumzia Shirika la Reli la TAZARA halina faida tu ndani ya nchi yetu, reli ile inaunganisha Tanzania na Zambia. Hivyo uchumi wa nchi hii ya Tanzania na Zambia tuna kitu kinaitwa kwenye uchumi comparative advantage. Yale ambayo hayapatikani Tanzania, tunayapata sisi Watanzania na yale yanayopatikana Tanzania hayapatikani Zambia wanayapata Wazambia. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo lakini nataka nimwambie kwamba TAZARA ni kitu muhimu sana kwa sababu kitasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa uzalishaji wa Mikoa za nyanda za juu. Kwa hiyo, kwa kuwa ina-connect na Zambia ndiyo maana tuliomba kwamba pale Tunduma, Mpemba tutengeneze bandari kavu ili mizigo yote SADC wawe wanakuja kuichukulia pale. Ikisafirishwa mpaka pale, naamini tutakuwa tumefanya vizuri sana katika uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, nililokuwa nataka kupendekeza ni suala la kuongeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji. Nimeangalia namna fedha zilivyotengwa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwenye sekta za uzalishaji bado hatujaweka vizuri. Nafikiri Mheshimiwa Waziri mkalitafakari na kuliangalia kwa mapana na marefu. Hili litasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, ambalo nataka niseme ni kuhusu sekta jumuifu ya masuala ya fedha. Sasa hivi kuna ukwasi kwenye mabenki. Mabenki mengi hayana uwezo wa kutoa mikopo kwa sababu hawana fedha za kutosha. Hii inatokana na kwamba mabenki mengi yame- concentrate mijini, yanatoa mikopo kwa watu wachache, watu walio wengi hawajajumuishwa katika mfumo jumuifu wa masuala ya fedha (financial inclusion).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi, katika jitihada ambazo Serikali ilikuwa imechukua na mkakati huu wa kuhakikisha kwamba sasa tunatumia teknolojia; mitandao hii ambayo inayo Vodacom, sijui Tigo na nini, imewafanya wananchi walio wengi sasa waweze kuingia katika sekta jumuifu ya masuala ya fedha. Sasa basi tunapokwenda ku- charge pale, inabidi tuchukue na tahadhari kidogo kwa sababu inaweza ikarudisha nyuma wananchi wengi kuwa katika mfumo jumuifu. Madhara yake ni nini? Kume-manage uchumi ambao ni informal, ambao hauko kwenye sekta rasmi, ni kazi kubwa sana. Tukijenga uchumi ambao ni formal, kila mtu yuko included, kila mtu anaweza ku-access mikopo, kila mtu anaweza kuwekeza, hiyo itatusaidia sana katika kuweza kujenga uchumi imara na kuweza kufikia malengo yale tunayokusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema kwamba Waziri Mkuu wa Singapore alipokutana na viongozi wa Afrika baada ya kustaafu mwaka 1992 aliulizwa, unafikiri ni vitu gani nchi za Afrika zinaweza kujifunza kutoka Singapore zikaendelea kama nyie mlivyoendelea kule Singapore? Sasa yeye alisema, ningekuwa Rais ya Afrika, ningekuja na mambo saba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona bahati mbaya muda haukuwa kwangu, basi naunga mkono hoja. Nataka niseme, bajeti hii tuiunge mkono kwa kila namna, tumsaidie Rais, tuisaidie Serikali ya Awamu ya Sita, tukatekeleze miradi ya vielelezo ili tuweze kufikia malengo yanayokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)