Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais nikiwa kama mtu ambaye nimekulia sehemu ya maisha yangu Wizara ya Mambo ya Nje. Mheshimiwa Rais ndiye mwanadiplomasia namba moja. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amethibitisha kwa vitendo kuwa mwanadiplomasia namba moja; kwanza, kwa ziara zake za Kenya na Uganda. Nilishasema hapa, kule Kenya imesaidia sana ziara ile kufungua milango hasa kwa sisi ambao tunalima mahindi, lakini pia Kenya nasi tunafanya biashara nyingi mbalimbali. Nampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Mheshimiwa Rais pia ameendelea kuzungumza na kushiriki mikutano mbalimbali online ya Kimataifa. Ameshazungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani, pia amezungumza na Rais wa Benki ya Dunia, amezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, hayo ni sehemu ya ule udiplomasia namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa nini? Kwa sababu ukienda katika bajeti yetu, katika “C” na “D”, ambayo inaelezea kwamba sehemu ya bajeti yetu itatokana pia na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo na mikopo ya ndani na nje. Takribani shilingi trilioni saba itatokana na mikopo pamoja na misaada. Sasa ili upate mikopo hii na misaada ambayo inatengeneza asilimia 20 ya bajeti yetu, ni lazima uaminiwe na uaminike Kimataifa. Vinginevyo huwezi kupata. Hili Mheshimiwa Rais amelithibitisha kwa vitendo kwa haya ambayo nimeyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba. Katika kuchaguliwa huku, ilipita bila ya kupingwa. Kwa kuweka record sawa, mara ya mwisho Tanzania ilikuwa Makamu wa Rais mwaka 1991 na pia imewahi kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Mkutano wake wa 34 Mwaka 1979 wakati wa Salim Ahmed Salim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu gani? Kama nilivyosema bajeti yetu asilimia 20 inategemea misaada na mikopo ya riba nafuu. Sasa katika hili, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yako kwa ujumla katika Serikali. Bajeti mliyotuletea kama walivyosema wenzangu ni bajeti kweli ya wananchi, lakini katika haya Mheshimiwa Rais, ambayo anayafanya kama mwanadiplomasia namba moja, yako ambao sisi kama watendaji katika Serikali tunao wajibu ya kuyafanya ili tusimwangushe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika maelezo yako ya bajeti Mheshimiwa Waziri, umeelezea masuala ya mikopo ya riba nafuu na misaada. Masuala haya

Mheshimiwa Waziri yanakwenda na terms and conditions; masharti na vigezo lazima vizingatiwe. Sasa nakuomba na timu yako ya wataalam, katika kufanya majadiliano, tuzingatie sana terms and conditions. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana ambapo tumekusumbua sana mimi na wenzangu wa miji 45, wakiwemo akina Mheshimiwa Kanyasu na Mheshimiwa Mabula. Kwa kweli umekuwa msikivu na umelielewa lile jambo na umetuahidi hapo upo katika mazungumzo ya hatua za mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile jambo litakwenda kusaidia miji 45, siyo katika ujenzi tu wa miundombinu kwa maana ya barabara, pia unaenda kuisaidia miji hii na Halmashauri hizi katika kujenga vitega uchumi ambavyo vitakuwa ni vyanzo vya mapato. Kwa mfano, sisi Mafinga, mojawapo ya mradi ambao tumeuainisha ni kujenga soko kubwa la mazao ya misitu. Kwa maana ya kwamba katika SADC Kusini mwa Afrika, soko kubwa la mbao, milunda na nguzo, liwe pale Mafinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake, tuharakishe jambo hili ili liweze kuanza kwa wakati. Pia kwa kutoa mfano tu, mradi wa maji wa miji 28 ambao ni mkopo wa fedha wa riba nafuu kutoka India is not a grant ni mkopo ambao tutaulipa. Tunapozungumza hapa ni mwaka wa sita haujaanza kutekelezwa.

Mheshimwa Mwenyekiti, pamoja na ule udiplomasia namba moja wa Mheshimiwa Rais, yeye anatufungulia njia, nasi sasa ni wajibu wetu katika kufanya majadiliano, tuhakikishe hayo majadiliano yanazingatia terms and conditions. Kwa sababu tukimbana Mheshimiwa Waziri wa maji katika mradi wa miji 28, anasema kwamba bwana, kuna masharti ambayo kwa kweli ilibidi tukae upya na kuanza kuyafikiria upya.

Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tusimwangushe Mheshimiwa Rais, kama mwanadiplomasia namba moja. Ameshatutengenezea njia, sisi wataalam tunapokaa kujadiliana katika kuhitimisha hayo masuala ya mikopo na misaada, basi tuzingatie sana terms and conditions ambazo zitakuwa in our favor kama Taifa. Nitazungumzia pia kuhusu TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na timu yake kwa kutushirikisha sisi Wabunge (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za usafirishaji katika nchi hii hazitokani na kuwa na bei ya mafuta, gharama za usafirishaji zinatokana na ubovu wa barabara. Tukienda kukabiliana na kuhakikisha kwamba tunaondokana na ubovu wa barabara, gharama za usafirishaji zitapungua. Nitatoa mfano, kutoka Mafinga kwenda Mdaburo wakati wa mvua ambapo ni kilomita zisizozidi 50, nauli ni shilingi 10,000, lakini kutoka Dodoma kwenda Iringa ambako ni kilometa 260 nauli ni shilingi 10,000. Kwa nini kilomita 50 nauli ni shilingi 10,000 sawa sawa na kilomita 260? Ni kwa sababu barabara ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokuja na huu mpango wa TARURA, tukimshukuru Mheshimiwa Rais na hizo shilingi milioni 500 ambazo mmetushirikisha Wabunge kwa kiasi kikubwa, na hii fedha ambayo tunaipendekeza kwenye tozo za mafuta, ushauri wangu na ombi kwa Serikali, ikawe ring- fenced ili ikatuondolee kero ya barabara. Kutoka Mafinga kwenda Mgololo kilomita 80, sana sana unachoweza kufanya ni kukodi gari ya shilingi 100,000 ili ikupeleke, kwa sababu basi likienda na kurudi hizo gharama za matengenezo ni kubwa kupindukia.

Mheshimwa Mwenyekiti na waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, tukubaliane hii tozo ipite, lakini iwe ring-fenced kwa sababu inaenda kuwa mkombozi wa barabara. Gharama za nauli toka naingia hapa Bungeni; kutoka Iringa kwenda Dodoma, nauli ya basi imebaki ile ile kwa sababu barabara inapitika throughout. Kwa hiyo, ubovu wa barabara ndiyo chanzo cha gharama kubwa za usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, juzi amesema kuhusu Mchuchuma na Liganga. Hivi Rais akishasema, nini kinafuata? Ni utekelezaji. Kama tungeweza kupata kile chuma, hata hii reli ya SGR tunayojenga, wataalamu wanasema gharama zake zingepungua kwa asilimia 50. Siyo tu chuma na makaa ya mawe, kuna madini mengine. Naomba Mheshimwa Waziri na timu yako jambo hili Mheshimiwa Rais ameshasema, sisi watu wa nyanda za juu kusini, itakuwa ni mkombozi mkubwa wa uchumi, italeta speed of effect, katika uchumi siyo tu Mikoa ya nyanda za juu Kusini na Taifa zima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ukisoma bajeti, maeneo yote Mheshimiwa Waziri anasema, “napendekeza.” Kwa hiyo, niwatoe shaka wananchi. Wengi wamesema kuhusu Luku kwamba wapangaji watalipa; wengi wamesema kuhusu tozo zilizopendekezwa kwenye miamala ya simu na namna ya kulipa gharama za simu; niwatoe hofu wananchi, kazi yetu Wabunge ni kuishauri Serikali na baadaye masuala haya kabla ya kutekelezwa, yatakuja kwenye Sheria ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasi kama ambavyo bajeti ikisomwa tunapewa siku moja ya kuitafakari, pia na wananchi nao wanaitafakari. Nasi humu ndani tunatoa maoni yetu kutokana na feelings za wanachi ambao tumeshaanza kuziona. Lengo ni mwisho wa siku kukusanya mapato. Kukusanya kwa namna gani? Ndiyo wajibu wetu na wataalamu wetu wa uchumi waweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, napongeza sana suala la nyasi bandia. Nakuomba Waziri, wewe ni mwana michezo, isiishie level ya Jiji. Nakuomba pia Mheshimiwa Waziri ile 5% ambayo itapatikana Sports Betting, umesema kwamba itaenda kukuza sekta ya michezo. Hata hivyo, nina angalizo, kusema kwamba nani ata-determine, kwamba TFF ndio ata-determine mtu atakavyokuwa ameomba nyasi bandia zije kwamba ana-qualify au asi- qualify, hapana. Nashauri jambo hili liachiwe BMT. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, kiwango cha kuaminika cha TFF siyo kikubwa kama unavyodhania. Mheshimiwa Waziri kwenye hili naomba BMT ndio wapewe hiyo mandate ya kwamba kama ni Halmashauri imeomba, kama ni Jiji limeomba au kama ni taasisi au shule fulani imeomba, Baraza la Michezo la Taifa ndiyo liseme kwamba huyu apewe ama asipewe, lakini hii ambayo katika uchaguzi tu unaenda kila Mkoa, wadhamini washachukuliwa ndiyo uwape dhamana ya kwamba watupendekezee kiwanja gani kijengwe au kisijengwe, hapana. Napendekeza hiyo ibaki kwa Baraza la Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nasema nawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Kazi iendelee.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mungu awabariki sana.