Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ahmed Yahya Abdulwakil

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii asubuhi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali, ambayo mimi ninaiita bajeti mkombozi na ufunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwanza inafurahisha mno, kwamba bajeti hii ina malengo mazuri ya kututoa hapa tulipo na kwenda katika hatua nyingine, hili ni jambo la kupongezwa. Vijana wetu, Mawaziri wote, Naibu Waziri pamoja na timu yote imefanya kazi kubwa sana kuandaa bajeti hii ambayo leo mmetuletea mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukuza uchumi lazima kuwe na vichocheo vya uchumi ambavyo vitaufanya uchumi ule ustawi na uendelee. Dalili zinaonesha kwamba katika kipindi kifupi tu cha mama yetu Pato la Taifa limekuwa na mama yetu ameweza kujiamini kwa kutoa fedha nyingi katika miradi mikubwa ya uchumi, ambayo italeta ufufuaji wa uchumi mzuri zaidi katika siku za usoni, hongera sana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi na-declare interest kama ni mfanyabiashara na muwekezaji, na kwa bahati niliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye sekta ya biashara, viwanda na kilimo. Ni ukweli usio wazi, na niko tayari hata na Naibu Waziri kwenda kuangalia ripoti ya fedha ya urari wa biashara baina ya Bara na Zanzibar kuwa ni mbovu mno! mbovu mno! Na niko tayari wowote kwenda, kwamba asilimia 75 ya biashara iliyokuwa ikifanywa baina ya Bara, imepungua mpaka asilimia 15 na imeweza kuathiri bajeti ya SMZ kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, hiyo iko wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndugu yangu tunapendana sana, Mheshimiwa Naibu Waziri tunaweza tukaenda tukaangalia namna hali ilivyoathiri biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa nini basi, Tanzania Bara wana-influence kubwa ya kuuza bidhaa kwetu Zanzibar; kwa mfano mbao, nondo, maji, cement na biashara nyingine zozote; hiyo ni free na hiyo ni free trade markets. Nchi ndogo kama yetu, ya Zanzibar yenye population ya watu 1,500,000 tu, sisi ukitaka tusitake tunategemea soko la Tanzania Bara. Na ukiangalia kwa upevu niliokuwa nao kwamba, hata miaka 100 nyuma, Zanzibar ilikuwa inategemea biashara (trade).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii bajeti iliyokuja ya kuondoa ondoa vikwazo vidogo vidogo tumeifurahia na tunaipongeza. Lakini la msingi, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri naomba na hapa kidogo unitolee macho. Umefika wakati kwa makusudi na kwa malengo mazuri, iundwe tume ya fedha ya pamoja, jambo ambalo mama nalo amelisisitiza hilo. Hii yote itaondoa minong’ono midogo midogo baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, na unalijua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi mimi kwa jumla naunga mkono. Lakini la mwisho ni kwamba, katika ufanyaji wa biashara, nchi yoyote duniani haiogopi wafanyabiashara. Kwa mfano kampuni kubwa za Marekani kama vile Amazon, Boeing na nyingine zote, hizi zote zipo karibu na nchi au Serikali husika. Muhimu tu zile kodi zinalipwa na wale watu wathaminiwe, pasiwe na woga baina ya wafanyabiashara na Serikali, hawa ndio wenye engine ya uchumi wa nchi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache mimi naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Mama amejizatiti na yuko kazini, na yote haya yatafanikiwa ikiwa tutakuwa tuna umoja na umoja wetu inshallah, Mwenyezi Mungu ataujaalia udumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)