Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru kwa dhati wewe binafsi, ninamshukuru Mheshimiwa Spika na Naibu Spika, kwa kuongoza na kusimamia vema Mkutano huu wa Bajeti na mahususi majadiliano ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa usikivu na uchangiaji makini kwa hoja za maandishi na kwa kuzungumza katika Bunge lako Tukufu. Natambua na kuthamini dhamira na nia njema iliyotawala mjadala ambao kimsingi ulilenga kuboresha mikakati na mbinu za kisekta zitakazotekelezwa katika mwaka wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Dalaly Kafumu, Mbunge wa Igunga, Makamu wake Mheshimiwa Vicky Paschal Kamata Likwelile, Mbunge wa Viti Maalum kwa ushauri na mwongozo ambao umechangia katika kuboresha mipango ya kuendeleza sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru pia Mheshimiwa Anthony Calist Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini, Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa maoni yenye kulenga kujenga, kutoa chachu na hivyo kupanua mawazo katika kuinua ufanisi wa sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa pongezi nyingi za utendaji wa Wizara na taasisi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Sisi kama Wizara tunaahidi kuendeleza jitihada zetu ili kuleta mafanikio endelevu. Aidha, tumepokea ushauri na michango mingi yenye chachu na changamoto ambazo kwetu tunazichukulia kuwa fursa muhimu katika kuleta maendeleo endelevu kwa sekta ya viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo sana, viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa na uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasilisho haya yanatambua na kuzingatia pia, hoja mbalimbali za Sekta yangu yaliyojitokeza wakati wa kujadili na kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais na pia Wizara zilizonitangulia kuwasilisha bajeti zao hapa Bungeni. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa, ushauri wenu na maelekezo ya Bunge hili katika kujadili bajeti ya sekta hii, tutayazingatia na kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mrejesho na utekelezaji wake.
Aidha, kutokana na muda mfupi nilionao katika kuhitimisha hoja za bajeti hii, maelezo na majibu ya kina ya michango mbalimbali yameandaliwa na yatawasilishwa rasmi kabla ya bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajielekeza katika kujibu na kufafanua hoja mbalimbali zilizojitokeza napenda kutambua michango ya jumla ya Waheshimiwa Wabunge 117 ambapo kati yao Wabunge 64 wamechangia kwa kuongea moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 53 wamechangia kwa maandishi, ahsante sana msiondolewe hapo.
Baada ya maelezo hayo naomba sasa nijielekeze katika kujibu na kutoa maelezo kwa hoja mbalimbali zilizojitokeza wakati wa mjadala wa bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo napenda niyakatae, niweke kumbukumbu sawa! Wizara yangu tangu nikabidhiwe, siwasemei walionitangulia, it is not business as usual. Wizara yangu tangu nikabidhiwe kuna mabadiliko na hata Mzee Komu nikutume Mheshimiwa Dkt. Komu, nenda kamuulize Mwenyekiti wa Tanzania Private Sector Foundation kwamba Mheshimiwa Mwijage mnamuonaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza katika mambo yatakayotekelezwa kwamba nitapigana kufa na kupona kuhakikisha Watanzania wote wanashiriki kwenye uwekezaji, this is not business as usual! Nimekaa na wataalam wangu, nina Profesa mmoja nguli wa uchumi, nina Profesa mmoja ana Ph.D. ya Uhandisi, mainjinia na wataalam wengine. Tumefanya kazi, ngoja niwaoneshe. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkakati, ngoja niwaambie bwana! Wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Nimesimamia mimi na wataalam wangu tumetengeneza mkakati ambao Mheshimiwa Bashe anaulilia unaitwa Cotton to Cloth Value Chain Strategy, mkakati huu kazi nimeimaliza tarehe 2 Mei, Mheshimiwa Kabwe Zitto nihurumie nimefanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetengeneza Mkakati tarehe 2 Mei nimeuzindua, nimesafiri usiku kuja hapa. Mkakati unaitwa Sunflower Sector Development Strategy. Natoa maelekezo Wizara yangu naomba mlete mikakati hii muiweke kwenye pigeon holes kabla Waziri wa Fedha na Mipango hajawasilisha, watu wanafanya kazi! it is not business as usual any more. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, tumetengeneza Mkakati unaitwa Leather Sector Development Strategy. Mheshimiwa Mabula anapozungumza kiwanda cha Leather cha Mwanza, nimekwenda Kashenamboni nikakuta kiwanda kile ambacho ukikiangalia unamkumbuka Mwalimu, mtu anaweka makatapila na matrekita, inatia uchungu. Nimetengeza mkakati wa ngozi. Nimemfuata mwekezaji wa ngozi ambaye alikuja hapa akizungushwa, amekwenda kuwekeza Kigali. Nambembeleza arudi hapa mnasema sijafanya kazi. it is not business as usual. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwaambie, unajua kuna mambo unapaswa kumwambia mtu usije ukamwambia mtu wa kwetu kwamba hufanyi kazi au hujaenda shule. Ukitaka kumuudhi mtu wa kwetu mwambie hujaenda shule, ndiyo maana nimekuja na mambo haya, ngoja niwaeleze, tumetengeneza mkakati, huu ni mkakati unalenga watu wa Lindi, Value Chain Road Map for Pulses, tarehe 2 Mei, ninao wafanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Faida, naingia saa mbili ofisini natoka saa nne usiku, is not a matter of writing, watu wanaumia na ndiyo maana Mheshimiwa Rais, akaweka Makatibu wawili wote ni nguli. Tunazungumza usiku na mchana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwaambie it is not business as usual tumemshawishi mwekezaji toka Singapore, tarehe 23 mwezi wa kwanza nilikwenda Morogoro katika mradi wa AGOA nilikuta watu wa Mazava wanahangaika, hawana mahali pa kufanyia kazi, nikawauliza nikiwapa eneo mtafanyaje, wakasema tutaajiri watu 7000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezindua eneo la Star City Economic Zone, ninatengeneza shed tatu, kuna watu wako tayari ku-rellocate kutoka China na Pakstani kuja kuwekeza katika sekta ya nguo, wewe unasema business as usual, haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo, niende kwenye suala la pili ambalo nasema na lenyewe siyo sawa. Watu wanasema hatuna mikakati, aah! Mikakati tunayo, kuna mkakati mwingine mdogo unaitwa Development Strategy for Tanzania Textile and Apparel February 2016, italetwa brother Chei. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, we trying to do everything, soma mkakati wa Integrated Industrial Development Strategy 2025, soma hotuba yangu page 24 imeeleza tutafanya nini. Tutawekeza kwenye fertilizer na kwenye petrochemicals. Nimjibu Mheshimiwa Hawa Ghasia, Ferrostaal sasa hivi wako na matarajio, wako Kilwa wanaangalia kujenga kituo cha kuunganisha gesi, kutengeneza mbolea ya gesi kwa kushirikiana na Minjingu. Mtu wa HELM A.G. ambaye anategemea kuwekeza Msanga Mkuu matatizo yake kwa nini hajaanza ni kwa sababu anataka uthibitisho wa maandiko kwamba gesi itapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshatoa suluhisho la kitaalam na gesi itapatikana, mamlaka zitaamua na watu wa Mtwara mtatengeneza mbolea. Waheshimiwa Wabunge niwaambie mambo ya Mtwara, mbolea ya Mtwara ikianza zinazalishwa tani nyingi za mbolea, tutaweza kupata mbolea, muwe na subira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Hawa Ghasia Mbunge wa Mtwara Vijijini. Mheshimiwa Mbunge huyu nilikwenda Misri nilimwakilisha Mheshimiwa Rais kwenye business forum, Business for Africa, nikakutana na mwekezaji anataka kutengeneza Kiwanda cha sulphur, nikamwambia nitampa kiwanja bure yule mwekezaji. Kiwanja mimi Mtwara nimekipata wapi. nikazungumza na Mbunge Mheshimiwa Hawa Ghasia ametoa eneo ambako huyu mwekezaji ataweka kiwanda. Mwekezaji huyu ametoka Misri, amepanda ndege, amekuja hapa, asubuhi ameonekana. Mheshimiwa nakuomba na katika Mstari huo hayuko peke yake, Mheshimiwa Bashe ametoa ekari 200 Nzega kujenga Special Economic Zone. Mheshimiwa Prosper Mbena ametoa eneo Morogoro Kusini. Waheshimiwa Wabunge tufuate namna hiyo, tutengeneze maeneo tutaweka utaratibu wa kuyaendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo yaliyokuwa yananikereketa, ngoja niendelee kujibu hoja zenu. Eeee! Mtu hawezi kusema we are trying to do everything, we will end up doing nothing, siyo kweli. Katika mkakati tumezungumza ni mbolea, ni mazao ya kilimo, halafu niwaeleze, ukisoma page 24 na ukasoma jedwali namba 16(c) inaeleza na nichukue fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Nsanzugwanko na Mheshimiwa Nswanzugwanko usimame uwaambie watu kama siyo mimi Kigoma Sugar, mradi wa kulima miwa kwa ajili ya kiwanda cha sukari ungeanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nazungumza sukari soma jedwali namba 16, wananchi wa Mbeya kuna mtu ametoka Marekani anataka kuweka kiwanda wanamzungusha, nimesharipoti kwenye mamlaka. Anataka kutengeneza tani nyingi za sukari halafu unasema you are trying to do everything, you end up doing nothing, usiniambie hivyo siwezi kukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende kwenye majibu ya jumla. Hakuna tofauti ya takwimu, Mheshimiwa Komu hakuna tofauti ya takwimu. Mheshimiwa Komu, Waziri mwenzangu lakini wewe ni Kivuli, hapa mwenzako aliyetoa hoja ndani ya Kamati yenu, tulipoletewa pesa nyingi kwenye General Tyre hoja ilitolewa na amerudia hapa. Ninyi ndiyo mlimwambia toa pesa hizi, nenda mkajitafakari muweke pesa zinazostahili. Tukatoka kwenye mamilioni yaliyopangwa tukabakiza shilingi milioni 150.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo General Tyre ninachokwenda kufanya nitaleta watafiti nguli waanze General Tyre kwa mtazamo mpya ikiwemo mawazo ya Mheshimiwa Lema, amesema hapa mmemsikia. Sasa Mheshimiwa Komu kuna mtu mmoja ameniambia kwamba Mheshimiwa Komu alipokuwa akisoma ile speech ukimwangalia inaonekana mambo aliyokuwa anasoma alikuwa hakubaliani nayo. Haya ulikuwa hukubaliani nayo. (Makofi)
Kwa hizo takwimu Kamati ni kwamba ilipanga milioni 150, huwezi kujenga kiwanda cha General Tyre kwa shilingi bilioni mbili. Ameshatangaza tajiri namba moja Social Security zote amesema Arusha nenda muone Waziri wa Viwanda awaambie pesa zenu mtaweka wapi muache kutengeneza majengo tu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Kivuli mwenzangu, huwa unanishauri na unayonishauri hapa uyasemi. Ananishauri vizuri sana huyu lakini akija hapa anabadilika, kwa hiyo mimi sina matatizo nayo, takwimu zangu ziko sawa sawa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda tunavyolenga vipo page 24 nimeshavisema na vimezungumzwa kwenye Integrated Industrial Develoment Strategy. Hakuna kitu chochote ambacho hatukusema. Kama alivyosema pacha wangu kwamba ukitaka mali utaipata shambani, lakini ili upate tija yapitishe kiwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini, anakuja ndugu yangu anasema Mwijage unataka kujenga viwanda kila mahali, ndiyo nataka kujenga viwanda kila mahali. Sifichi, wala sipepesi macho nitavijenga kila mahali. Kiwanda cha kuchakata asali ni dola 40,000, Tabora ni asilimia 36 tu ya asali ya Tabora inachakatwa. Mimi hapa nina order za asali kwenda Oman, siwezi kuzipata. Katavi asali yenu yote haichakatwi. Ni Mbunge gani anaweza kwenda benki kukopa dola 40,000 akanyimwa. Nani anaweza kunyimwa? Nakushukuru, unajua tatizo la Mheshimiwa Lema anachangia mambo mazuri ukiondoa yale aliyoyafuta halafu anatoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nunua kiwanda watakukumbuka. Uzuri wa viwanda, kwa nini mimi napenda viwanda vidogo, unaweza kufanya biashara ya apples au mvinyo wa zabibu, meli ikifika Dar es Salaam unauza kontena bila kuliona, unaweka pesa yako hapa unakwenda Kilimanjaro unashusha mvinyo. Lakini ukitengeneza kiwanda wewe mwenyewe unafaidi na jirani anafaidi. Ndiyo maana Mheshimiwa Magufuli anasema tujenge viwanda, ufaidi wewe mwenye mtaji na jirani afaidi. Mama nipigie makofi umeipenda hiyo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kujenga viwanda hakuna itikadi, kwa hiyo tutajenga viwanda vidogo sana na tutajenga viwanda vya kati. Niwasimulie mfano mtakaupenda tena niwaambie ninyi rafiki zangu, Mheshimiwa Lema, ame-order kiwanda cha toothpick kwa ushauri wangu dola 28,000, ame-order kiwanda cha Tomato Souce kwa ushauri wangu, anataka kufuga samaki, mimi nina kiwanda cha kutengeneza chakula cha samaki, the best in this country. Msiogope kumiliki, watu wanaogopa kumiliki, mtu ana malori, anayaficha eti siyo ya kwangu, useme! tatizo ni kwamba uliyapataje? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, kwa hiyo ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mhamasishe watu wetu na tutajenga viwanda. Mheshimiwa Jitu Soni ninakushukuru pia. Mheshimiwa Jitu amesema kujenga Petrol Station moja ni milioni 700, hivyo ni viwanda vingi, mimi nimetoka kwenye oil industry, nawashawishi sasa wale nguli wa oil industry watoke na kundi la kwanza nalipekeka kwenye maziwa. ASAS ni nguli wa petrol amashakwenda kwenye maziwa, Oil com ameshakwenda kwenye maziwa, na nitakwenda kwa Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi, ndiyo maana nikamshukuru, nataka kuomba maeneo ya ile nuclear farm kusudi tutengeneze farm. Nina ajenda ya kwenda Musoma, nimekuwa namfuata kila siku Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, kuna shamba la Utege ili kusudi tutengeneze maziwa. Mnaweza mjiamini, mnaweza Waheshimiwa Wabunge na muwaambie wapiga kura wenu wanaweza, msipothubutu ninyi waliopo nyuma yenu hawataweza kwenda kwenya uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekti, kwamba fedha uliyopangiwa ni kidogo, katika maazimio yangu ambayo nitayaboresha kumridhisha mjukuu wangu Mbunge wa Kigoma amesema uyaboreshe babu, nikasema nitayaboresha. Nitamuwekea kile anachopenda afurahi. Sasa mjukuu kama anapenda kitu mpe.
Katika maelezo yangu nimesema viwanda vitajengwa na sekta binafsi. Kitu kingine niwaambie, maelekezo ya Mheshimiwa Rais anasema tunaanza na viwanda vilivyopo, vizalishe maximum capacity. Kwenye ripoti yangu nimezungumza, viwanda vingi vinazalisha below 40 per cent.
Mheshimwia Mwenyekiti, mtu anaishangaa TANELEC, Mheshimiwa Rais alipokwenda Monduli ile ziara ya kwanza ya Jeshi, Mkuu wa Mkoa ambaye na yeye ni mjukuu wangu wa Arusha, akamfuata akamlalamikia TANELEC. Mheshimwia Rais kwa utaratibu wake akamwambia anayeshughulika na viwanda ni Mheshimiwa Mwijage, akaja na watu wa TANELEC. Mimi lile nikalipeleka kwa Mheshimiwa Muhongo, tatizo la TANELEC ni sawa na East African Cable. Tumetengeneza umeme kwa Mpango wa REA II karibu kilometa 45,000 lakini hakuna waya ulinunuliwa hapa, East African Cable inatengeneza cable zile zile, haijauza kwa miezi 36. Lakini huwezi kunilaumu mimi ndiyo naanza sasa nije nione mtu anaziagiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema katika hotuba yangu kwamba nitakuwa mboni ya kuhakikisha Wizara yoyote, Mtendaji yeyote, Shirika lolote la Umma linalokiuka nitawasemea na mnajua nitawasemea wapi. (Makofi)
Kuhusu mipango ya Wizara haiunganiki siyo kweli, huyu ni Waziri mwenzangu wa Kilimo, ni pacha wangu, hata juzi Mheshimiwa Mtolea wakati tunahangaika namna gani tulipeleke jembe kwenye makumbusho, tumekutana mimi nilikuwa chairman na chini yangu walikuwepo Makatibu Wakuu watano. Wawili kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Makatibu Wakuu watatu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Tunajadili namna gani tunaweza kupata zana za kilimo, kuzitoa huko tuzitoako, kwa riba nafuu, tukapeleka kwenye vituo ili kusudi jembe libaki kwenye bendara ya chama na watakaokwenda makaburini mlikute basi mambo yawe mazuri Mheshimiwa Mtolea.
Kwa hiyo usiwe na wasiwasi, tunafanya kazi kwa kuunganisha Wizara, lakini kama alivyozungumza mrithi wangu Mheshimiwa Kalemani ni kwamba mimi bila nishati sifanyi lolote, bila barabara sifanyi lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachumi mnaelewa. Kuna kitu kinaitwa production cost na transaction cost. Transaction cost ni zile gharama za miundombinu, unaweza kuzalisha kwa gharama ndogo lakini kama usafiri ni mbaya bidhaa itafika sokoni imeshakuwa mbaya. Ninawategemea watu wa miundombinu na tunafanya kazi wote na ndiyo maana wanasema bajeti ya viwanda ni trilioni 29 kwa sababu sasa tunatengeneza mazingira wezeshi. Miundombinu wezeshi, ni pamoja na maji umeme, barabara na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa Bagamoyo. Bagamoyo haiwezi kufanya kazi mpaka Kidunda ifanye kazi, litatatengenezwa birika lingine la kuchuja maji, kwa hiyo we are connected, we are related and intergrated. Kwa hiyo, kwamba hatuna mahusiano, hatukuunganika haiwezekani, brother. Mheshimiwa Rais, ana Mawaziri 19 kwenye cabinet, anatuona na ana simu zetu kila wakati tunazungumza, sisi ni timu moja inayokwenda kwa kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini miradi ya Mchuchuma na Liganga, Engaruka Soda, General Tyre, miradi ya Ngaka inaitwa kuwa ni miradi ya kimkakati. Akaniuliza rafiki yangu, ninampenda sana Mheshimiwa Hussein Bashe, ana michango ya kiuchokozi, amenikumbusha zama zangu nikikaa pale, nilikuwa na michango ya namna hiyo muulize Mheshimiwa Ngeleja. Nilikuwa naweza kutetemesha microphone, ananiuliza uniambie comperative advantage.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi hii kuna comperative advantage, kuna competitive na absolute advantage zote zimeunganishwa hapo. (Makofi)
Kuhusu General Tyre siyo kwa ufahari, General Tyre sina shida na matairi, nataka General Tyre irudi nyuma ichochee kilimo cha mpira Pemba na Unguja, ichochee Morogoro, ichochee Tanga tulime mpira. Lakini General Tyre tuna advantage, tuna population inayokua vijana wa sasa kila mtu akipata mshahara kwa kwanza anapeleka ile salary slip kwenda kununua gari. Niwaambie nimewahi kuwa Mtafiti Msaidizi wa Benki ya Dunia kuangalia usalama wa barabarani, percent kubwa ya hatari za barabarani zinasababishwa na matairi mabovu.
Mheshimiwwa Mwenyekiti, nimeshwamwambia mtu wa TBS, na nitawaonesha show kama mnapenda show, watu wakienda na video mnasema wanakwenda na video, wasipokwenda nazo mnasema business as usual. Nimemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa TBS, tutakagua matairi yote hata kama ni mapya, kama hayana siku ya kutengenezwa na siku ya ku-expire tutakwenda kuyateketeza. Piga makofi na hiyo mbona hampigi makofi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuambizane, kwa hiyo General Tyre,
comparative advantage, tuliyonayo tuna watu wanaweza kulima mpira, but the comperative advantage we
have, we have a young population itakayopenda kuendesha magari. That is the comparative advantage,
comparative advantage nyingine tuna ardhi, Mheshimiwa Lema amenipa heka
200. Hauwezi kupata heka 200 Ulaya, utaipata wapi? Kwa hiyo, tutaangalia
comparative, competitive na ikibidi tuangalie absolute advantage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampenda Mheshimiwa Bashe, nililazimika kwenda kusoma Michael Potter, Tom
Peter na Charles Andy kuangalia hivyo vitu vinazungumzaje. Kwa hiyo hii iko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchuchuma na Liganga ina maneno. Tunataka chuma pale, ndicho kiwanda mama.
Lakini chuma ya Liganga inasema ukiweza ku-extract yale madini mengine, unapata faidi nyingine.
Ukasema Mheshimiwa Bashe kwamba kuna makando kando ameyaona CAG. CAG alipokuja kuona makando kando
mimi nilishayaona. Tarehe 23 Januari niliwaita watu wa NDC wakafanya presentation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno nilikuwa nayasikia nikiwa kijiweni, nikawauliza, Katibu Mkuu
ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa NDC wakati anaanza kazi, akaita timu ya wataalam kutoka nje ya
Wizara yangu, wameandika ripoti nzuri, tutaweka sawa, tuondoe makando kando, lakini mkakati wa
Mchuchuma na Liganga uweze kuendelea. Ukitaka kuujua mradi huu muulize Mheshimiwa Dkt. Dalaly
Kafumu, akueleze, ni mradi muhimu. Lakini kuja kumpata huyu mtu haikuchukua siku moja imechukua
miaka mingi, kuna mtu mmoja mshindani alisema naapa Mchuchuma na Liganga haitafanya kazi, kwa
sababu yeye ana migodi sehemu zingine za dunia hii.

Kwa hiyo tupigane Watanzania, kama mtu atakuwa na makandokando tuyaondoe. Watu wa kwetu wanasema
osangile amazi, oshorome eboga yaani unafukia kinyesi kusudi uchukue mboga uende, ukikataa utakula
chakula bila mboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini viwanda vilikufa, ngoja niwasimulie mlichangia siku mbili siyo
mchezo. Kwenye kitabu changu ukurasa wa nane aya ya 14, nimezungumza ngoja niende taratibu
mnisikie. Mfumo wa kiuchumi ulikuwa mfumo hodhi, ndiyo maana viwanda vilikufa. Huwezi kununua raw
materials mpaka upewe kibali na Kamati Kuu tumemaliza hiyo sasa ni soko huru. Kutozingatia
viashiria vya nguvu za soko katika kuendesha uchumi wa viwanda, ndiyo maana vilikufa, lakini
msisahau lilikuja lile wimbi la globalization (utandawazi), ule upepo tusingeweza kuuzuia na ninyi
mnajua madhara ya
upepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana upepo ulitaka kupita hapa, alhamdulillah Mwenyezi Mungu akatuokoa upepo ulikuwa umekuja vibaya, upepo ulikuwa umekuja vibaya kwa hiyo huwezi kuzuia upepo. Mpaka akatokea jamaa mmoja akazuia mafuriko kwa mikono, ni mambo ya ajabu ajabu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine viwanda vililenga kukidhi mahitaji ya ndani, viwanda vililenga kukidhi mahitaji ya ndani tu sasa tumekataa, ni import substitution cum export promotion, nimesema kwenye hotuba yangu wazalishaji wa Tanzania nitawalinda lakini msibweteke, nitawalinda wasibwete walenge kuzalisha katika soko la dunia, hata tairi tutakazozizalisha zitakuwa zinalenga dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni menejimenti ambazo hazikuzingatia ujuzi pamoja na study, na technical know who, iliingia pale. Nataka niwaeleze ninayoyajua bila kuwaficha kitu. Mtoto wa shangazi unampa kazi mambo yanaharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuyumba kwa uchumi wa Taifa hili, kulikosababishwa na kuyumba kwa uchumi wa dunia, ukumbuke oil crisis ya miaka 70 lakini msisahau na nichukue fursa hii kuwashukuru Watanzania mliokuja kupigana vita ya Kagera hadithi ingekuwa nyingine, vita ya Kagera ilitusumbua, wengine mikanda haijawahi kufunguliwa, kwa hiyo na yenyewe ilituyumbisha. Viwanda vikayumba tukaingia kwenye mgao wa sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze Watanzania haya mnayajua ila mnataka kujifanya hamyajui. Ujenzi na uendeshaji wa viwanda ulitawaliwa zaidi na matakwa au matashi ya kisiasa bila kuzingatia zaidi nguvu ya soko. Kwa hiyo, viwanda tutakavyovijenga, nimeeleza kwenye hotuba yangu itazingatia upatikanaji wa malighafi, soko na teknolojia, lakini na utulivu. Ngoja niwaambie research moja imefanyika, nazungumza na watu mbalimbali Morogoro iko juu katika disciplined labor force worldwide Tanzania nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitawaambia mambo yote disciplined work force Tanzania wanasema iko Morogoro, mtoto wa Kiluguru anashuka na mzigo anapanda na mzigo, anaweza kufanyakazi. Lakini ukimchukua mtu kwenye pool table brother amepiga pool table miaka mitatu, umuweke kiwandani saa sita hajazungumza Simba na Yanga au kigodoro, hawezi kufanya kazi. Habari ndiyo hiyo, tutazingatia mambo yote hayo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji mdogo, under capitalization mtaielewa hiyo, nalo lilikuwa tatizo, utamaduni wa utegemezi wa wahisani kupita kiasi. Donor over dependence syndrome, mmemsikia Mzee Magufuli, anasema hata kama ugali nakula bila mboga ni wa kwangu. Donor over dependence syndrome amelisema Mheshimiwa Magufuli, kwamba itabidi tutembee kwa nguvu zetu na haya yalituangusha, wanakuletea kiwanda wanachotaka kukuletea siyo kile unachokihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahusiano ya kisekta na uratibu wa Wizara nimeyazungumza sina tatizo nayo, kuna vikao vingi vinahusika, dhana kuwa Serikali haina sera na mikakati endelevu kutoka awamu moja hadi nyingine hapana, wenzangu wamelizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vision 2025, ilipokuwa inaandikwa akiwemo Mheshimiwa Profesa Mark Mwandosya, alikuwa bosi wangu mimi nikiwa Meneja wa gas, nilikuwa namuona anaandika imemalizika 1996, haijaanza leo ni Mzee Mkapa huyo. Tunapozungumza sustainable industry development strategy ya 2011/2015 alikuwa Mzee Kikwete, kwa hiyo kuna uendelevu, kinachowasumbua watu ni kutokusikiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza hizi nyimbo zina mafundisho yake, kwa nini Rais wetu anaitwa tinga tinga? Ni kwa sababu yeye ni kama tingatinga, tingatinga likifanya kazi baada ya masaa fulani hufanyiwa service tena kwa gharama kubwa, likimaliza kufanyiwa service linafanya kazi kama jipya, kwa hiyo wanaona kwamba ni mpya lakini ndiyo tabia ya tingatinga, ametoka service brother kwa hiyo tunachapa mwendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera zipo zimeandikwa na zote nimekuja nazo ni hizi hapa, sustainable industry development policy ya 1999 inakwenda mpaka mwaka 2020, Rais alikuwa Mzee Mkapa, ngoja niwaoneshe Integrated Industry Development Strategic ya 2011, Rais alikuwa Mzee Kikwete, kwa hiyo kuna uendelevu, ndiyo tabia ya magari makubwa, likiharibika gari kubwa huwa linafanyiwa service linarudi barabarani utadhani gari jipya, gali kubwa halitupwi, CCM ni gari kubwa, huwezi kulitupa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie SIDO. Wanasema SIDO imetengewa Mikoa mitano tu, hapana siyo hivyo, SIDO haijatengewa Mikoa mitano tu, hiyo Mikoa iliyotajwa ikiwemo Arusha tunaweka vitu vinaitwa incubator. Watanzania wakiwemo wanafunzi watakaoonekana na ubunifu, tutawapeleka pale, watawekwa kiatamizi, wataangalia utaalam wao, Canada na India watatusaidia waki-graduate, tukiona wanaweza wanakwenda mtaani, itakuwa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, zimeandikwa hapo, kwa hiyo pale ni center.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa yote, nitahakikisha kunakuwa SIDO na niwaambie, najadiliana na TAMISEMI Maafisa Biashara wa Wilaya nataka wapewe mamlaka zaidi siyo kukata leseni tu. Wawe wanawafundisha watu namna ya kufanya biashara na ujasiriamali, waingie hata kwenye mikutano ile ya Halmashauri ile Menejimenti ya Halmashauri waingie pale, wafanye kazi, hakuna kwenda kukusanya leseni, unakusanya leseni biashara mtu ulimfundisha? Hiyo tutaizuia, tukubaliane hapa waende wafanye kazi na SIDO atakuwa coordinator wangu, yaani Meneja wa SIDO wa Mkoa, anaripoti kwa Minister moja kwa moja na mambo yanakwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaagiza SIDO watengeneze catalogue za mitambo yote midogo midogo ya milioni kumi, milioni ishirini, milioni thelathini, muwaoneshe Waheshimiwa Wabunge wakawaoneshe wananchi wao namna ya kuchakata maziwa, asali, kuchakata mihogo, kama ndugu yangu Mheshimiwa Bilago wa Kigoma nimemuonesha mtambo wa kuchakata muhogo, unahitaji shilingi milioni12 unatengenezwa Morogoro pale, unachakata muhogo. Kwa hiyo, ndugu zangu vitu vipo ni jukumu la SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya Mchuchuma na Liganga na CAG nimeishaizungumzia.
Kuhusu umuhimu wa NDC katika ujenzi wa viwanda nchini. NDC ni kutambua fursa, mimi bwana mkisema napendelea kwetu basi mtanilaumu tu, nirudi tena kuwapongeza watu wa kwetu Kigoma. Watu wa Kigoma wanafanya kazi nzuri, Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma na uongozi wao wa Mkoa wameanzisha utaratibu wametambua kaya laki moja, kila kaya ilime mawese heka moja, watengeneze ekari laki moja na nimewaahidi mniombee nidumu kwenye cheo hiki, nitawaletea wawekezaji wawekeze katika kiwanda cha mafuta ya mawese. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndivyo inapaswa kuwa siyo kazi ya Serikali, kwa hiyo ndugu zangu kazi ya NDC niwaeleze watu wa Kigoma, wako Kibaha - Pwani, wanatengeneza shamba la ekari 4,000 na outgrowers watazalisha tani 60,000, mahitaji ya sasa ya mafuta ni 400,000 wanatengeneza 60,000 nimewaagiza waende Mbeya, nimewaagiza waende Rukwa, nimewaagiza waje Kigoma. Mtaalam wa mbegu za miwese nimeishampata anaitwa Mushobozi, anafanya kazi na Koffi Annan yuko Arusha, aje awatengenezee mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anakuambia business as usual haiwezekani it is not business as usual, ngoja niwaambie, kuna mambo mawili napaswa niyazungumze nimetulia, moja la rafiki yangu Mheshimiwa Sungura. Mheshimiwa Sungura amezungumza maneno makali. Ubora wa vyakula niwasihi msinunue chakula chochote ambacho hakina alama ya TBS, maneno aliyoyasema Mheshimiwa Sungura siyo ya kuchekea, msinunue chakula ambacho hakina alama ya TBS kwamba mtu anachukua chakula sijui anaugua figo, sijui anakwenda kumsubiri Mungu amchukue siyo habari nzuri, kwa hiyo hilo naisemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu utendaji wa CBE, CBE inasaidia kufundisha vijana wetu, CBE ninaisimamia, CBE nitaisimamia, tuhuma alizozisema ndugu yangu Mheshimiwa Waitara, watu hao waliniletea taarifa Ijumaa ile iliyopita nikazichukua mwenyewe nikazipeleka ofisini, nikampa Katibu Mkuu, nikamwambia mambo ya kufanya. Mambo ya kufanya ni pamoja na kumhusisha CAG, lakini mambo mengine ni ya kimamlaka zaidi, ni ya PCCB ni ya Polisi, nikayaancha kule. Waziri hawezi kwenda kupeleleza, na yule msichana aliyeko gerezani tangu mwaka 2012 aitwaye Rose ni mahabusu siyo mfugwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema mahabusu huwa hanyimwi mshahara, mimi sijawahi kwenda shule ya sheria na kwa umri huu sitegemei kwenda kwenye shule ya sheria lakini niwahakikishie kitu kimoja, nitaisimamia CBE.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie CBE mnisikie sasa, wasionijua wakawaulize niliosoma nao shule. Nitahakikisha CBE inakuwa shule ya viwango, kuanzia muonekano, ukimuona mwanafunzi wa CBE anapita utasema yule anasoma marketing, yule ni mtawala, hakuna mtepesho, hakuna mtu anavaa kama anakwenda kwenye vigodoro, CBE nitahakikisha naiweka kwenye viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengine nimeishaweka wataalam Mheshimiwa Waitara tulia. Tukitoka hapa nitakwenda niwaone wajukuu zangu huko. Suala la kuangua mayai Mheshimiwa Waitara wewe una pesa za kununua incubator, incubator ya mayai ya shilingi milioni 20 inatosha ndugu zangu wa kule, nitasaidiana na wewe kutafuta eneo, tutengeneze eneo katika mpango wa Mitaa Mheshimiwa Waitara mimi sina ugonvi na wewe, kuniacha kwenye chama hiki haujakosea, nitakwenda kushughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliochangia bajeti yangu. Nimshukuru Mheshimiwa Omary Mgumba, mfano wake wa korosho ulikuwa mzuri sana. Ametoa literature ya korosho, lakini tatizo la korosho watu wa korosho, mimi nimepewa maelekezo na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mimi na Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi tutakaa chini, matatizo mnayo wenyewe. Wamarekani wametoa order ya korosho tani 15,000 wako tayari kununua kwa bei zaidi ya 40,000 kwa kilo iliyokobolewa lakini kwa masharti, kwamba lazima ikobolewe na wananchi, the poor mnaowatetea
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nasikia za Chama chenu cha Ushirika zinakataa, imeishafika kwa Mheshimiwa Mwigulu na ninyi mtaitwa wadau na nimezungumza hata na makampuni yanayohusika ORAM walinifuata, nilizungumza hapa wadau wa korosho walinifuata, tutakaa chini jioni tujadiliane twende mbele. Hii sayansi ya korosho ina mambo mengi, ngoja niwaambie sayansi ya korosho, wameniambia kwamba unaweza ukaona korosho iliyotoka Tanzania tani 150,000 korosho iliyotoka Tanzania India, unakuta ni 250,000 nimeyaona. Kwa hiyo, ukubali Shekhe nakushukuru kwa nipigia makofi, mtu akisema business as usual mkatalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hoja binafsi moja moja, nimeishamshukuru Mheshimiwa Omary Mgumba, lakini kuna watu akiwemo Mheshimiwa Nsanzigwanko, wamezungumzia suala hili, suala la ease of doing business. Kama wazungu wakirudi leo, kutupima kwenye wepesi wa kufanya biashara, Tanzania hali imebadilika, mojawapo ya eneo tulilokuwa tunapimwa ni wepesi wa kupata viwanja vya kuwekeza. Kwenye bajeti yangu nimeshukuru TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, wamefanya kazi nzuri. Mimi nimepewa hekta 800 kwa kazi ya Mheshimiwa Dkt. Ndugulile na Mheshimiwa Lukuvi, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisha mwambia Mheshimiwa Muhongo tutoe bomba la gesi kutoka Mbagala, likatishe moja kwa moja liende Kigamboni. Tunaendelea nahangaika, sasa aliyenichekesha kwenye ease of doing business ni rafiki yangu Mheshimiwa Kubenea, akataka kuzungumza Omukajunguti, akasema nimesoma kitabu chote Mwijage hajazungumza Kagera, usinichonganishe. Watu wa Kagera wanajua kwamba Mwijage alilelewa na bibi yake, na bibi yake Mwijage Mko Omwami alimfundisha hadithi 1002, hadithi moja inasema hivi, bibi yangu aliniambia mwanangu ukiamka asubuhi kwanza unawe uso. Uso wangu mimi ni Kagera na wala simfichi mtu, kwa hiyo Omukajunguti itajengwa, tutaishughulikia Omukajunguti, maua yatatoka pale, ufugaji wa samaki nitajisahauje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini utaratibu siyo kukimbilia haya, nataka niondoe kwanza mambo ya kwanza, Bagamoyo wananidai pesa sijazilipa nikachukue Omukajunguti niongeze nitaongeza matatizo. Lengo letu kwenye SEZ tutalipa maeneo tuliyopewa kwanza, tukishamaliza tunatafuta wawekezaji kwenye yale maeneo yenye vivutio, kuna watu wanataka ku-relocate kuja Tanzania. Tunataka tuyachukue yale, tuya-service hata kwa kukopa pesa, pesa tutakazopata twende kwenye maeneo mengine, wengine wanasema Mwijage mmekamata maeneo mengi, we are not aiming for the next election, we are aiming for the next generation. Tunakamata maeneo watakaokuja miaka 50 chama ni hiki hiki, watakwenda kwenye hayo maeneo watajenga. Kwa hiyo ndio mpango mzima. It is not for next election, it is for next generation.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vietnam nimewaandikia wana Special Economic Zone 150, lakini Vietnam ni moja ya saba ya nchi yetu. Sasa ndugu yangu mimi naota kesho kutwa, ningependa vijana wakija wakiwa wanaangalia waseme alikuwepo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles John Mwijage. Kwa hiyo hilo nimelijibu kwa hiyo ease of doing business tunaijua, na mojawapo ya ease of doing business ni katika kutoa haki. Mheshimiwa Rais ameliona, ametoa pesa za kutosha katika Mahakama kusudi ipunguze, ninacho hiki kitabu, na nimeagiza kiwekwe kwenye website ya Wizara yangu, utakisoma hiki tunapimwa vipi, lakini ndugu zangu wasikudanganye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza na Mmarekani mmoja juzi, baada ya hotuba yangu imejadiliwa nchi nzima, na CTI wameijadili. Mmarekani amenipigia simu akasema Mwijage, yote uliyoandika ni bure nikasema eeh bure. Akasema you didn’t include important element nikamwambia what? Akasema peace, amani yetu inatusaidia kufunika haya mapungufu lakini hatutabweteka, haya mapungufu tutayaondoa, na akaniambia kitu kimoja, Tanzania katika Afrika ndiyo nchi ambayo inatembelewa na Marais wengi wa Marekani wastaafu, hawawezi kwenda mahali pengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Msigwa nakushukuru sana, kwa hiyo fedha ya General Tyre nimeishaijibu, dira ya maendeleo ya Taifa kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kipato cha kati imetimiza miaka 21 bila mageuzi nimeisha lizungumzia. Kitu kimoja ambacho watu hawaelewi, kuna ule mpango wa kuanzia mwaka 2010, mpaka 2025 kipande cha kwanza ilikuwa ni kuondoa vikwazo. Vikwazo vimeondoka, sasa tunakwenda kwenye kujenga uchumi wa viwanda, tukimaliza tunakwenda kwenye ushindani. Kwa hiyo, kazi imeondoka sasa hapa kama ni ndege tunaanza mwendo wa kupaa, tumeshatenga maeneo, nimewaeleza taarifa za ukweli kuna viwanda vina-relocate, vina-relocate kutoka Asia kuja hapa, someni majedwali yangu nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu niingie Ofisini nimekutana na makampuni zaidi ya 32, kuna kampuni inaitwa Goodwill inakuja Mkulanga, muulize Mheshimiwa Mbunge wa Mkuranga, kuna Kampuni inaitwa Goodwill inakuja Mkuranga, itatengeneza kiwanda cha vigae kitakachozalisha square mita 80,000 kwa siku, production ya mwaka itaweza ku-generate dola milioni 150. Lakini kuna kiwanda ambacho mimi niliwezesha kupata ardhi Mkuranga Mzee Lukuvi nitakushukuru mara mia moja, kile kiwanda kitatengeneza ajira za watu 20,000 Mbunge wa Mkuranga anajua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shamba Mkuranga ndio maana nakwenda kule kwa hiyo kazi inafanyika. Kwamba tumefanya nini, basi tulikuwa tunatoka kwenye runway sasa tunapaa, na tukipaa tunakwenda, kwa hiyo muwe na imani. Lakini nimezungumza kwenye mipango ya kazi yangu, kwamba nawaomba tukubaliane twende safari, asitokee mtu akawa na mashaka. Tukifika njiani mkaona tunapotea mniambie tunapotea na niwahakikishie, hii hotuba na michango yenu, kuna michango imeandikwa ya maandishi inastahili kuandikiwa kitabu. Wale ambao michango yenu itakuwa ina mapungufu, nitawarudishia mui-edit vizuri, nitaweka picha zenu pale na nitaandika majina yenu, mchango wa Mbunge fulani ili kusudi muweze kuona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuangalia suala la Omukajunguti, nimelijibu, uwanja wa ndege utajengwa Serikali isuke upya taasisi zinazoshugulikia viwanda, biashara na uwekezaji ili kuziba mianya ya ukwapuaji fedha za umma ambazo zingetumika kuendeleza sector ya viwanda, ushauri huo naupokea na nitaufanyia kazi.
Kwa hiyo, mwaka 2016/2017 Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, haijaweka bayana mkakati wa Serikali wa kufufua viwanda 33 vilivyobinafsishwa na kufa. Ngoja niwaambie, viwanda vilivyopo lazima vifanye kazi, na bidhaa mnaziona madukani, lakini vile vilivyokufa vina njia mbili.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vile vilivyokufa vina njia mbili, ama ukirudishe ama ukiendeleze na namna ya kukiendeleza tafuta mbia mwenzako. Kwa nini tunavitafuta ni kwa sababu mikataba ya mauziano inasema hivyo lakini faida nyingine vile viwanda vina miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi kuliko kwenda kupasua misitu kuweza kujenga sehemu mpya.
Suala la korosho nimelizungumzia, tutakaa chini tulizungumzie, viwanda vya Mwalimu tutavifufua, Serikali itimize ahadi ya Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliahidi wakati wa kampeni kuwa kiwanda cha kubangua korosho kitaanzishwa eneo la Mkuranga. Tutakapomaliza matatizo ya korosho na kile kiwanda kitaweza kufanya kazi. Sunshine wako tayari kutengeneza viwanda wana kiwanda kimoja Mtama, wanataka kwenda Nachingwea wako tayari kwenda kokote, lakini muondoe yale matatizo ya msingi yaliyopo kwenye sekta hiyo.
Serikali iwezeshe vijana wasio na ajira ili wasiwe wanatanga tanga, kwa kushirikiana na TAMISEMI tunatenga maeneo, hapa ni mshukuru Mheshimiwa Azzan Zungu, nakubaliana naye mipango ya kurasimisha sekta isiyo rasmi inafanyika na njia mojawapo ni hiyo. Leo nimezungumza na Mheshimiwa Mangungu wa Mbagala, wameshanitegea eneo, nikitoka hapa nakwenda kukutana na Mheshimiwa Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam tukaangalie eneo tutaanzia pale. Kwa hiyo, Mikoa yote imeshaambiwa kutenga maeneo na tunawalenga Vijana. Watu wa BRELA na TRA tutaangalia namna ya kuondoa mambo ya TIN, kumlipisha mtu kabla ili watu waweze kurasimisha shughuli yao. Tutafuata maelekezo yenu ambayo mmetupa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Kioo Mbagala, nitatoa maelezo kwa kuandika. Katika miaka 1970 NDC imechukua eneo la hekta 350, Mbunge wa Nyamagana tuonane, nitakupa maelekezo namna ya eneo hili, tuko tayari kulitoa kwa ajili ya Halmashauri kama mtaona kwamba mtalifanyia kazi vizuri, lakini tafuta wawekezaji tuweze kulifanyia kazi sina tatizo nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya chai navishughulikia, nimemaliza cha Lushoto, nitakwenda Lupembe na Mheshimiwa Spika aliyemaliza kipindi chake anafuatilia suala hilo.
Mheshimiwa James Millya suala la Diamond, Tanzanite kule tunalishughulikia nimeshamaliza kulipa pesa zilizokuwa zimebaki zote, kwa hiyo tutakwenda kuangalia namna gani ya kutengeneza Special Economic Zone.
Mheshimiwa Adadi Rajab nimekukubalia kwamba tukutane kesho kutwa leta wawekezaji wako, tuweze kwenda mbele na mpango wa kuwekeza kwenye matunda.
Mheshimiwa Kasuku Samson aliuliza je, viwanda dira ya Rais au ya nchi? Hii ni sera ya CCM hilo sina tatizo nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti,wakulima wa Dodoma wasaidiwe kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika karanga na alizeti. Mheshimiwa George Malima Lubeleje tutafanya hivyo, nimekubaliana na Serengeti waende waanzie kwenye Jimbo la Mtera, watachukua hekari nyingi wawafundishe wale wakulima wa kawaida watumie matrekta wazalishe mtama, tunawahakikishia kwamba mtama utauzwa Serengeti, kutoka kwa bwana kibajaji kule Mtera, kwa hiyo Mbunge wa Mtera pamoja na swali lako hili, uje unione nitakuunganisha na mtaalam wa Serengeti walime mtama kwako, mwezi wa saba nitakwenda kukagua hilo shamba tulime. Tutawachukua mmoja mmoja muwe na imani tunakwenda ili mradi safari ianze.
Kambi Rasmi ya Upinzani wanasema wafanyabiashara wadogo kuelekezwa katika viwanda badala ya kuonekana kero, tutafanya hivyo sina matatizo.
Kuhusu kuiwezesha SIDO isogeze huduma zaidi Wilayani hadi vijijini, huo ndiyo mpango wangu na itategemea bajeti na Mheshimiwa Elias John Kwandikwa wa Ushetu Wizara isimamie SIDO ili vijana wapate ajira, nitaisimamia SIDO, ipo chini yangu tunaanza na centre kubwa zile tano, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge mtembelee SIDO mkaone mambo, kuna mambo mazuri sana.
Kuna hoja kuhusu SIDO itoe elimu zaidi kwa viwanda vidogo ili Watanzania wengi wavianzishe, tutafanikiwa tukiwekeza kwenye viwanda, mchezo upo kwenye viwanda. Baba Mchungaji Mheshimiwa Msigwa mnihukumu kwa viwanda vidogo. Viwanda vya wakubwa vinatumia teknolojia kubwa haviajiri watu wengi, kwa hiyo nitavihimiza hivi nawashukuru sana kwa mchango wenu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kupigiwa kengele michango yote nimeizingatia, natafuta mchango wa Mheshimiwa Msigwa ambaye alitaka kuona kama ninaweza kumwonesha 40 percent. Mimi leo ndiyo ninaomba bajeti, ninamaliza Ilani ya Chama ya 2010-2015 sasa naanza ya 2015-2020. Kwa hiyo niko year zero nina take off, huwezi kunihukumu leo kwamba nimetengeneza wangapi? Lakini nimeandika kwenye maelezo yangu kwamba tutatafuta wajihi wa kila kiwanda na kila kampuni. Lengo la kutafuta profile za kila kampuni ni kuweza kubainisha at every stage kwamba watu wangapi wameweza kupatiwa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumeanzisha viwanda? Tumeanzisha viwanda kwa sababu vinaweza kutoa ajira, na ndiyo maana tunalenga viwanda vinavyotumia watu wengi. Mheshimiwa Msigwa akasema Mwijage ninazungumza kama ninapiga kampeni. Nimesema kazi yangu kubwa itakuwa kuhamasisha Watanzania wakubali hii dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu, inahitaji mhamasishaji na mhamasishaji aliyepewa ni mimi, sasa Mzee Msigwa unauliza makofi polisi? Ndiyo kazi yake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafute masoko ya matunda nje ya nchi. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Raza, amekubaliana na mimi atanisaidia kunipatia masoko ya mazao na masoko ya mazao ya matunda yako Oman. Walikuja watu wa Oman Waziri wa Oman nilizunguka naye mjini, watu wake wakaniuliza, Mheshimiwa Waziri, nikasema naam, wanazungumza kiswahili wa Oman, wakasema mnanunua na ninyi matunda kutoka Mombasa? Matunda ya Muheza yanauzwa Mombasa kwa hiyo watu wa Oman wakadhani matunda ninayanunua kutoka Mombasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, soko lipo ninamshukuru Mheshimiwa Raza na TANTRADE nawapa jukumu, lakini Watanzania mchangamke kufanya biashara inawezekana. Tatizo kubwa la Watanzania walio wengi wanaogopa kumiliki, mtu anapita kwenye nyumba yake anaangalia huku, eti wasimwone ana nyumba, kwenye gari lake hawezi kulipanda, anapanda gari nyingine, gari yake inapita. Mmiliki, msiogope kumiliki ili mradi mmiliki kihalali ndiyo utaweza kufaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutumia fursa za uanachama wa Jumuiya za Kikanda angalia takwimu zangu, Tanzania tumeuza mno East Africa, tumeuza mno SADC, tunakwenda COMESA. Kwa hiyo, Watanzania tujiamini na nitaendelea kuhamasisha mambo ya Kikanda ya bilateral, kikanda, kieneo na ninyi msiogope, Watanzania msiogope kwenda Southern Sudan sasa hivi mchangamkie fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania kuna wakati tulikuwa tunashangilia fursa, location advantage, haina maana, ushishangilie fursa, ichangamkie fursa. Katika hilo ndiyo maana viwanda vidogo, viwanda vya kati, tunataka kuanzisha mashindano ya kimkoa ningependa kuona mtu analeta sembe imekuwa packed kwenye mfuko, anasema sembe safi kutoka Ileje, mchele mzuri kutoka Mbarali, tushindane Kiwilaya na tushindane Kimkoa, hii ni asali nzuri ya kutoka Katavi, hilo haliwezekani mpaka muweze kuyahamasisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kusaidia wahitimu kusajili makampuni. Nitaliangalia hili tuweze kuangalia namna gani tunaweza kuwasaidia wahitimu hata ikibidi kuwasajili siku wanafanya mtihani, lakini lazima tuzingatie sheria, na kama kuna vikwazo mtaweza kuondoa ninyi mnaopitisha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumaliza tatizo la sekta ndogo ya sukari. Kigoma Sugar amepewa na watu wa Kigoma niwashukuru tena, hekta 47,000; akifanya kazi mpiganie kwa namna yoyote asikwamishwe na mtu yeyote na mimi nitawasaidia. Atazalisha tani 120,000; RAK wameomba ardhi watazalisha zaidi ya tani 60,000; Kagera Sugar anataka kupanua mpaka tani 120,000; lakini Oman wamesema wanataka watumie facilities za Kagera Sugar wazalishe tani 180,000 kama alivyosema Mheshimiwa Zitto Kabwe tunaweza kuzalisha tani 1,500,000 tukapata mamilioni mengi ya pesa. Kwa hiyo hili tatizo la sukari ni suala la muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze muazime uzoefu wa Wabunge wa Bunge la Kumi, Taifa lilikuwa linasumbuliwa na sekta ya mafuta namna hii, kwa hiyo kinachokuja tutakuwa na coordinated importation kwani kuna suala la quality, kuna suala la quantity, kuna suala la price, ulikuwepo udanganyifu kwa hiyo udanganyifu unakwisha wanaoshangaa kwa nini Mheshimiwa Rais anasema ndiyo, akishamaliza kusema mwenye nyumba sasa mje muone watoto watakavyofanya tutalishughulikia hili, kwa hiyo itakuwa na coordinated importation na msiwe na wasiwasi hakuna Ramadhani sijui sukari itakosa hakuna, kuna wengine sijui Mikoa gani huko, wanachagua maduka mawili ya kata kuuza sukari, sukari itauzwa kila duka na itakuwepo sukari ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka mwenye sukari, na ukitaka mambo yakuendee vizuri hakikisha sukari inakwenda kwa wananchi, distribute kusudi tuone kwamba hakuna sukari. Lakini sukari ndiyo ilikuwa inakwamisha viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni waambie siri moja, waulize wawekezaji, Kigoma Sugar, muulize hata RAK, Mheshimiwa Jitu Soni anataka kutengeneza kiwanda cha sukari kwenye Halmashauri yake cha kuzalisha tani 50, Abdul Salim aliyekuwa Mbunge wa Kilombero, anataka kutengeneza kiwanda cha tani 50, siyo gharama kubwa ni shilingi bilioni mbili tu unakwenda Benki unaweka guarantee ninakudhamini, wewe Mbunge mimi nitakosa kukudhamini? Ndiyo faida ya Ubunge mnakopa. Msiogope kukopa huwezi kuwekeza kwa pesa yako mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo usinipigie kengele, baada ya kuzungumza yote hayo, nimeahidi kwamba mengine yote nitaweza kuyaweka kwenye kitabu vizuri, niwashukuru wote mliochangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kutoa hoja.