Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutupa uhai leo kuwa wazima tukaja tukajadili mambo yenye maslahi na nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nikushukuru kunipa hii nafasi ili na mimi niweze kuchangia. Katika Ushahidi ambao ninao kwenye Bunge lako hili Tukufu, bajeti hii ya mwaka huu ni bajeti ambayo imeongoza kuwa na maoni ya Wabunge wengi. Tumepitisha bajeti nyingi sana, na kila tukipitisha tulikuwa tuna maombi kama Wabunge, lakini safari hii maombi mengi yamesikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yamesikilizwa maombi ya Wabunge wa Bunge lililopita na Wabunge wa Bunge hili la Kumi na Mbili. Kwa hiyo tunaipongeza sana hii bajeti na tunamuombea mama yetu azidi kupiga kazi ili kazi hii aifanye iende kwa wepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli bajeti hii imetaja wajibu lakini pia imetaja haki za wananchi. Kuna msemo mmoja unasema kwamba paka kama huli panya Samaki hupewi. Sasa humu ndani ametakiwa paka akamate panya kwanza, ndiyo hizi tozo ambazo zipo kwa ajili ya kuja kufanyia haya maendeleo. Sasa tusilalamike sana kwa sababu hizi tozo ni lazima ziwepo ili mambo yetu yaende vizuri. Kwa hiyo, hilo, kwamba paka asiyekula panya Samaki hapewi, tuendelee kuunga mkono jitihada ambazo zimefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni bajeti ya wananchi. Yameguswa makundi ya watu wengi; wameguswa wafanyabiashara, wameguswa wafanyakazi, wameguswa kwenye hii bajeti hata watu wetu wa bodaboda, wameguswa wanafunzi. Kila mmoja unaona kwamba amepata unafuu ndani ya hii bajeti. Kwa hiyo, hii ni bajeti ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mwanzo, kwamba hii bajeti imetokana na maoni ya Wabunge wengi sana. Sasa niende kuchangia katika jambo ambalo amelisema Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 31 alipotaja VAT ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara zikaenda Zanzibar na bidhaa zinazozalishwa Zanzibar zikaja Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze sana Serikali kwa hatua hii. Ni jambo ambalo tumelipigia kelele kwa siku nyingi sana, na tulilizungumza, lakini bado haukuonekana umuhimu. Sasa nini inakwenda kutokea; zile biashara za wafanyabiashara wadogowadogo wenye mitaji yao ambao wanakuja kuchukua bidhaa Tanzania Bara, sasa biashara zile zitafunguka na mambo yatakwenda yatakuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na taasisi za kijamii zinakuja kufanya shopping Tanzania Bara, pengine vifaa vya ujenzi; misikiti, makanisa, shule na NGOs nyingine tofautitofauti. Hizo zote zilikuwa zinapata hiyo kero kwa sababu walikuwa wakipigwa double VAT. Sasa imeondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu katika hili; ni kweli tunarudi katika mfumo wa marejesho. Lakini kama tunarudi katika mfumo wa marejesho tufanye utaratibu upi; warejesheane TRA na ZRB, isiingie Hazina katikati. Ikiingia Hazina katikati ucheleweshaji wa marejesho utatokea. Sasa hapo ndipo kwenye ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo nikuombe urudi ule utaratibu wa kurejesheana TRA na ZRB. Tukisema tunapitisha Hazina hapo kikwazo kinaweza kikaja kikatokea tena na baadaye tunaweza tukasema turudi tena katika mfumo wa zero rate. Kwa hiyo hilo nitoe ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hii tumesema ni nchi ya viwanda. Mheshimiwa Waziri, hili naomba ulisikilize vizuri; ni nchi ya viwanda. Kuna viwanda vya dawa ambavyo vinatengeneza dawa ndani ya hii nchi yetu. Na sisi tuna- import dawa, tuki-import VAT ni zero. Sasa viwanda vyetu vinanunua material (malighafi), wananunua malighafi nje, lakini ile malighafi tunaipiga kodi. Ina maana hawa hatuwaweki katika mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vifaa mfano vifungashio vya kwenye dawa sisi tuna-import, lakini mle mna kodi Mheshimiwa Waziri. Na kodi inasababishwa kwa hila moja tu; kwamba eti ukileta hicho kitu kiwe kimeshachapishwa huko nje jina la dawa. Sasa ukifika hapa ukitaka kuviosha vile vitu unaviosha vipi? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, hili tunalizungumza hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna material ya kutengenezea dripu, nayo pia yanapigwa kodi. Na kiwanda chetu kitakuwa hakiwezi kushindana, na tujue kwamba tumepewa fursa ya soko la SADC kuuza dawa, SMD. Sasa hii fursa tutaipoteza kwa sababu ya hizi kodi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kifuniko kile cha rubber cha kufungia dawa, nacho pia kinatakiwa kiwe kina jina ndiyo kiwe zero, ukikileta hakika jina ina maana kwamba tayari kinapigwa kodi. Kwa hiyo, viwanda vyetu vitashindwa kuja kushindana na dawa za nje. Ijapokuwa kwamba hatutengenezi dawa zote, lakini tuna lengo la viwanda, kwa kuwa tuna lengo la viwanda hiki kitu tukifanye. Vinginevyo tunaweza tukaja tukashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze hii bajeti, ni bajeti kweli kwamba kazi iendelee. Ni kweli bajeti kazi iendelee; imegusa miradi yote iliyokuwepo mwanzo na imechukua miradi mingine mipya. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa kufanya bajeti ya aina kama hii ambayo ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, na sisi tunasema kazi itaendelea, na sisi tutaendelea kuiunga mkono. Hii ni bajeti ambayo imetokana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Yale yaliyosemwa katika ilani tumetakuta leo humu ndani ya bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana nikasema katika historia yangu ya kuwa Mbunge, hii ni bajeti ya kwanza ambayo imebeba maoni mengi ya Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)