Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali iliyoko mbele yetu. Tukitambua hii ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia, niseme tu kwamba nampongeza kwa sababu kuna mambo mazuri ambayo yapo kwenye bajeti yanayoleta matumaini na mengine pia nitayashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jambo zuri ambalo nimeliona hapa na kwa nini nasema nalipongeza? Kuweka bajeti kwa ajili ya kupandisha madaraja watumishi wetu wa Umma. Hili ni jambo zuri kwa sababu watumishi wetu wa Umma ndio injini ya nchi hii. Hawa Watumishi wa Umma walisahaulika muda mrefu, hawakupanda madaraja, hawakuongezewa mishahara. Kwa hatua hii ya awali ya kuweka bajeti kwa ajili ya kupandisha madaraja, tunampogeza sana Mheshimiwa Mama Samia. Tunaomba aendelee hivyo ili huko mbele ya safari aweze kuongeza na mishahara ambayo Watumishi wa Umma muda mrefu hawajapata Nyongeza hii ya mishahara lakini hawajapanda madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwa nini nasema nampongeza? Imekuwa ni matamanio ya Madiwani muda mrefu kwa nchi nzima, nami nilikuwa Diwani. Nililvyoingia mara ya kwanza katika Bunge hili ilikuwa pia ni hoja yangu ya kuona namna bora ya kuboresha utendaji kazi wa Madiwani hapa nchini. Mama Samia ameliona tunampongeza kwa kuchukua hatua hii, kwamba sasa Madiwani walipwe na Serikali Kuu badala ya Halmashauri zetu za Wilaya ni hatua nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, twende mbali zaidi sasa, tuwajengee uwezo Madiwani, tuwape semina mbalimbali kwa sababu sasa watakuwa wametoka kwenye vile vifungo vya kuwatumikia Wakurugenzi ili wasikose posho zao, watakuwa independent, wataweza kujisimamia, kusimamia fedha zinazoenda, kusimamia miradi. Basi tujikite pia kuona namna bora ya kuwapa mafunzo ili fedha tunazopeleka katika Local Government kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo isimamiwe vizuri kwa uwezo na tuliowajengea Madiwani wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu, kuna masharti, kanuni, taratibu mbalimbali ambazo zimeondolewa, ambayo ni hatua nzuri ya kupunguza urasimu wa nchi hii. Nimeona kuna baadhi ya vitu vimeondolewa, siyo lazima vipite kwenye GN, siyo lazima sasa vikae Baraza la Mawaziri, vimempa mamlaka Waziri. Ziko tozo na adhabu na faini na misamaha mingine ambayo pia amepewa Kamishna wa TRA. Ni hatua nzuri ya kwenda kupunguza urasimu ili yale matokeo tunayoyatarajia yaweze kufikiwa. Hongera sana kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba mama alishajipambanua kwa kusema kwamba hataki kodi ambazo ni za dhuluma. Sasa tunaomba haya ambayo ameyatenda mama, watendaji wake na wasaidizi wake mkayafanye kweli kweli. Tunataka wafanyabiashara wetu ili waweze kulipa kodi, wawe na mazingira mazuri, rafiki yanayofikika, ambapo kweli watafanya biashara na watalipa kodi na uchumi wa nchi utakua na uchumi wa mtu mmoja mmoja utakua na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya ambayo anayasema mama na kuyasimamia, ninyi kama wasaidizi wake kwa maana ya Waziri na watendaji wote myasimamie kwa vitendo, ndiyo tutapata matokeo ambayo tunayakusudia. Sasa ushauri wangu uko katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kuhusu Kodi ya Majengo, tumekuwa na maelekezo na taratibu nyingi sana kuhusiana na Kodi ya Majengo. Huko nyuma, Halmashauri za Wilaya zilikuwa zinakusanya Kodi ya Jajengo, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ikachukua tozo hizi ikaipa TRA. TRA wakapambana nayo ikawashinda kwa sababu hawakuwa na uwezo lakini pia ilikuwa ni ngumu kuikusanya. Sasa leo mapendekezo yanakuja, tozo hii ya Kodi ya Majengo, ikatwe kutokana na Luku za nyumba. Unaponunua umeme, unakatwa kodi. Niwaambie kwamba, nadhani hili siyo jambo jema, linahitaji kutazamwa tena kwa upya. Kwa sababu tunajua watu wenye majengo huwa ni wachache na wanaolipa kodi mara nyingi ni wapangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamepanga. Akipanga anamlipa mwenye nyumba kodi yake, lakini suala la umeme linabaki kwake yeye mpangaji. Kwa hiyo, mwisho wa siku utekelezaji wa tozo hii inaenda kumfikia mpangaji na sio yule mwenye nyumba. Wenye nyumba ni wachache; ndiyo wapo, lakini anayenunua Luku ni yule mpangaji. Kwa hiyo, ni jambo la kutazama kwa upya ili kuhakikisha tozo hii iwafikie kweli wenye nyumba na sio wapangaji. Kwa sababu tunaelewa miji mikubwa watu wengi ni wapangaji. Miji kama Dar es Salaam watu wengi ni wapangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nyumba moja siku hizi ni utaratibu hata nyumba za biashara, kila mtu ana mita Luku yake, anajaza umeme wake mwenyewe. Sasa unaweza kukuta nyumba moja ina Luku karibia 10. Ina maana hawa wote wanatakiwa walipe kodi ya majengo, wakati wao ni wapangaji tu, mwenye nyumba yupo, anapokea kodi yake ya pango, halipi kodi nyingine yoyote. Kwa hiyo, ni vyema sana hili jambo likatazamwa kwa upya tukaondoa huu utaratibu kwa sababu unaenda kumkandamiza yule mpangaji na sio yule mwenye nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili; mnaweka ongezeko la shilingi 100 kwenye tozo za mafuta. Tunafahamu impact ya kuongeza tozo kwenye mafuta. Umeshakuwa ni utamaduni; ukiongeza tozo kwenye mafuta, kila kitu nchini kinapanda. Hii shilingi 100 tunayoongeza hapa mwezi Julai kila kitu tutakachokishika dukani kitakuwa kimepanda bei; impact yake ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa impact ya hii lazima itazamwe, naelewa lengo ni zuri, kwamba hizi fedha zipelekwe TARURA kwa ajili ya ujenzi wa barabara zetu kule vijijini; jambo jema kabisa, kwa sababu tunajua mwisho wa siku matokeo ya kuwa na barabara nzuri. Wakulima watapeleka mazao yao sokoni, barabara zitapitika, wanaotaka huduma za afya watapita kwenye barabara zinazopitika. Lakini hii impact ya pili ya kuongeza kodi ambayo itasababisha mfumuko wa bei ni lazima itazamwe kwa upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, kama utatuhakikishia you can control mfumuko wa bei, it’s okay, ni sawasawa. Kama hilo litawezekana, basi hizi fedha ambazo zitatozwa kwa ajili ya TARURA, kwa ajili ya ujenzi wa barabara zetu vijijini ziwe ring fenced kama zilivyo fedha za REA. Hapo ndiyo tutaona matokeo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri kwamba hizi fedha za TARURA ziwe ring fenced zitumike kwa makusudio hayo yaliyokusudiwa ili matokeo yake tuweze kuyaona kwa barabara zetu kupitika kwa kadri inavyotokea kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine la mwisho; umuhimu wa sekta binafsi katika kujenga uchumi. Tunatambua uchumi wa nchi sekta binafsi nayo ni muhimu sana, lazima iwekewe mazingira mazuri, mazingira wezeshi, itazamwe ili iweze kuchangia katika uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mmoja; kulikuwa kuna viwanda mbalimbali hapa nchini ambavyo vimeanzishwa na ama ni wawekezaji au ni wazawa, lakini viwanda vingine vimekufa kwa sababu ya mambo mengi ambayo yanasababisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, kulikuwa kuna viwanda vya matrela. Miaka 12 iliyopita tulikuwa tuna viwanda visivyozidi 12, lakini hivi viwanda leo vimekufa, havipo tena. Kwanza, ajira imepotea, lakini hivi viwanda havijaweza kuwa endelevu kwa sababu ya mazingira mengi na mbalimbali, na moja wapo ni kwamba haya matrela yanaagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vyema Serikali ikatazama namna gani ya kutengeneza mazuri, kwanza kwa kuhakikisha kwamba hivi vifaa vinavyokuja kutoka nje, vinavyoagizwa, kwa maana ya matrela, na yenyewe iwekewe kodi kubwa ili ku-discourage zinazotoka nje na kuweza ku-encourage viwanda vya ndani vinavyotengeneza matrela na kuhakikisha kwamba kwa kufanya hivyo maana yake tutaongeza ajira, tutachangia kwenye pato la nchi kwa maana ya uchumi, lakini kuona namna gani kwamba tunaongeza ujuzi kwa Watanzania wetu, waweze kuwa na ujuzi ambao utatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye suala hili la viwanda vya matrela; ukiagiza gari dogo unatozwa ushuru wa asilimia 25, haya matrela yakiagizwa ushuru asilimia 10. Sasa lazima tuone namna ya ku-balance. Kama zote zinakwenda asilimia 25 ili ku-discourage ili kusaidia viwanda vyetu vya ndani, na hata wakati mwingine tufikirie namna ya kutoa ruzuku kwa viwanda vya ndani kwa sababu itachangia uchumi wa nchi, ajira na kukuza pato la mtu mmojammoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.