Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote, nikishukuru Chama changu kwa yote, lakini pia nimshukuru mume wangu David Kafulila ambaye pamoja na mimi kuwa mama ametambua ninayo nafasi ya kulitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye mjadala. Tunajadili Mpango, lakini niseme kwamba mipango siyo tatizo katika Taifa, Taifa hili hatuna umaskini wa mipango, ila tuna tatizo la utekelezaji wa mipango. Tumeshakuwa na mipango mingi, ukiangalia kuanzia mwaka 1981 mpaka 1986 tumekuwa na Mpango mwingine kuanzia mwaka 1987 mpaka mwaka 2002, huu ulikuwa ni Mpango wa kumi na miaka mitano ambao ulikuwa umelenga kwamba mpaka kufikia mwaka 2002 Tanzania iwe nchi ambayo itakuwa ina mfumo wa ujamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukaja kuwa na Mpango mwingine wa miaka 25 kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2025 ambao lengo lake lilikuwa ikifika mwaka 2025, Tanzania iwe ni nchi yenye uchumi wa kati na mipango mingine mingi iliyofuata. Hata hivyo, hii mipango haitekelezeki na haitekelezeki kwa sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza, ni mfumo mbovu tulionao katika Taifa hili na sababu ya pili ni ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi zote ambazo tumeshafatana nazo katika masuala ya maendeleo kuanzia mwaka 1963; Malaysia, Singapore, Korea Kusini, nchi zote hizi mpaka hivi sasa zimeshakuwa wahisani wetu na zimekuwa wahisani wetu kwa sababu mipango yetu inashindwa kutekelezeka. Nimetangulia kwa kusema kwamba sababu kubwa ni mfumo mbovu, lakini pia na ufisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo mbovu kwa maana gani? Kwa sababu ya muda nitazungumzia kwenye suala la elimu kwenye suala la mfumo mbovu. Leo hii tunazungumzia elimu bure, ni suala ambalo naamini kabisa kwamba Watanzania na wazazi wote wa nchi hii wamelifurahia, lakini tunazungumzia elimu bure wakati huo huo kuna changamoto nyingi. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri anasema hivi bado zimebaki changamoto ndogo ndogo pamoja na elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi changamoto ndogo ndogo zina uhusiano mkubwa na performance ya wanafunzi. Niseme hivi ni bora mngehakikisha mnaondoa hizi changamoto, halafu mkasema elimu bure. Mfano, mwaka 2015, Taasisi ya Haki Elimu ilitoa ripoti ikasema hivi; katika Taifa letu kuna upungufu wa madawati 1,170,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hesabu ya haraka haraka kama kwenye dawati moja wanakaa wanafunzi watatu watatu, inamaanisha Taifa letu kuna wanafunzi milioni tatu na ushee wanakalia mawe, kwenye nchi ambayo ni ya tano kwa idadi ya misitu Afrika nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwanafunzi anakaa kwenye mawe, mwalimu anakuja darasani kufundisha somo la historia, anaandika zama za kale za mawe, anajiuliza hizi ni za kale au ni za sasa? Ningeomba kwanza waelekeze kwenda kutatuta changamoto zilizopo kwenye mashule, halafu wakaja wakatuambia elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la utawala bora, muundo wa suala la utawala bora kwa ujumla. Mfano mzuri ni hapa Zanzibar wala siyo mbali, unapuzungumzia Zanzibar leo hii ni aibu, hivi karibuni nilimsika Donald Champ, mgombea wa Republican Marekani, anasema Afrika wanahitaji miaka 100 kuendelea kutawaliwa kwa sababu hawajajitambua. Mpaka anafikia hatua ya kusema hivyo ni kwa sababu ya mambo kama yanayoendelea Zanzibar, tunadhalilisha Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, mnaweza mkasema kwamba labda kwa sababu mpo madarakani, lakini ni hivi Marekani wamesema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa fair and free, Ulaya wakasema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa fair and free, mtasema aaa! Hao ni wa mbali, SADC hapa Kusini kwetu wamesema uchaguzi wamesema ulikuwa fair and free, AU wamesema ulikuwa fair and free. Tatizo ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 nikiwa na miaka mitatu, mlianzisha kitu kinaitwa multipartism mkimaanisha mfumo wa vyama vingi ambao mlikubaliana kwamba kila baada ya miaka mitano kutakuwa kuna utaratibu vyama vinagombea mbalimbali kinachochukua nafasi kinashika dola. Sasa niseme tu kwamba, kinachoendelea Zanzibar ni suala la kukosa ustaarabu tu na siyo vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Rais Mafuguli aweke mkono wake Zanzibar. Nasema hivi kwa sababu gani? Hata awe mzuri kiasi gani Zanzibar akiharibu hawatamwelewa, kuna msemo unasema hivi: “You cannot stand for something you don’t know and likewise it doesn’t matter how much you know about something, if you cannot stand up on it. Kinachoendelea Zanzibar kama Magufuli hataingia, maana yake ni kwamba Wazanzibari hawatamwelewa, maana ingekuwa Kilimanjaro angeingilia halafu ninyi mnahubiri kwamba hii ni nchi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Magufuli, suala la Zanzibar alitazame kwa jicho la kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ufisadi unaturudisha nyuma sana, namwomba Mheshimiwa Magufuli, kwa sababu ninaposema ufisadi namaanisha ni miongoni mwa sababu inayopelekea hii mipango tunayoijadili hapa isitekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufisadi unaoendelea sasa Mheshimiwa Magufuli anatakiwa auone na auangalie kwa ukamilifu kwa sababu huu ni muda sasa amemaliza kutumbua vipele, atumbue majibu makubwa mengine anakaa nayo mezani. Imefika wakati ni lazima tuseme, kwa sababu kinachoendelea katika Taifa hili tukikaa kimya, tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka jana, kuna ripoti ililetwa hapa, tulieni siyo ESCROW, kuna mjadala ulikuja hapa ukiachana na ESCROW, lilikuwa ni suala la mabehewa. Mwaka jana Taifa letu limeingia hasara ya bilioni 238, hizi zilikuwa ni fedha za wananchi ambao zilikwenda kununua mabehewa, matokeo yake, mabehewa yalikuwa fake. Haya siyo maneno yangu, hii ni ripoti PPRA ambayo ilileta ripoti kwenye Kamati ambayo nipo mimi. Mabehewa yanaonekana kwanza ni fake, lakini cha ajabu hata kampuni iliyopewa tenda ni kampuni ambayo haikufanyiwa due diligence kwa maana ya ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa limeingia hasara ya bilioni 238 kwa sababu ya mtu tu kuwa mzembe kuwajibika, halafu leo jipu linahamishwa mkono wa kushoto, linapelekwa mkono wa kulia. Mheshimiwa Magufuli alitumbue na jipu hili liko humu ndani, tunaye Mheshimiwa Mwakyembe, leta ripoti hapa, ripoti kuhusiana na masuala ya mabehewa, mlikataa kuileta hapa kwa nini mnaficha, kama ni safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwakyembe umeaminiwa na Serikali na Magufuli lete ripoti hapa, tusijisahaulishe haya mambo tunayakumbuka tuliona hata tukiwa nje. Tunaomba tutendeeni haki wananchi wa Tanzania kwa sababu Bunge liliazimia ripoti iletwe Bungeni, naomba ripoti iletwe hapa Bungeni na tuweze kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)