Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na wenzangu. Kwanza nianze sana kwa kumshukuru Rais wetu mpendwa wa Awamu ya Sita Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti ambayo imegusa na imetii mahitaji ya Watanzania walio wengi, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili nimpongeze sana ndugu yangu Waziri Mwigulu kwa bajeti hii nzuri pamoja na Naibu Waziri Engineer wetu na Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii. Kwa kweli Mwigulu tembea kifua mbele na wasaidizi wako bajeti hii imewagusa sana Watanzania, tunakupongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nilipenda niliseme; Waheshimiwa Wabunge wengi tupo hapa, tupo mchanganyiko; wapo vijana na kandalika. Ombi langu, mna mipango mingi mbele ya safari. Katika mipango mliyonayo sasa tumuache mama Rais wetu, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wafanye kazi yao, ninyi subirini mpaka 2029 ndipo muendelee na mipango mingine ambayo mnayo huko mbele nadhani mmenielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumuombe Mheshimiwa Waziri na timu yake, kwamba fedha hizi ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezijadili hapa tuombe ziende kwa wakati ili zikafanye shughuli ya maendeleo katika maeneo yetu na katika majimbo yetu. Kwa mfano Wabunge walisema hapa, na mimi nalisema, kwamba yapo madeni ya wazabuni ziende zikalipe. Zipo return za VAT za muda mrefu za wafanyabiashara, mwende mkalipe ili nao walipe madeni ambayo wanadaiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile iko miradi ya maji ambayo Rais wetu na Wizara hii mmedhamiria kumtua mama ndoo kichwani. Sasa kuna miradi ile ya miji 28, na katika miji 28 na Makambaku ipo; mradi ambao fedha inatokana na mkopo nafuu kutoka Serikali ya India; sijajua tumekwamba wapi kwa sababu imechukua muda mrefu. Tuombe, wananchi wana mategemeo makubwa, mkalitatue hili ili kandarasi wawe site waweze kufanyakazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ziko fidia ambazo wananchi wamekuwa wakidai. wakiwemo na wa Jimbo langu la Makambaku. Niombe, maana wewe ndiwe bwana kihenge; nikuombe Waziri na timu yako mtoe hizi za fidia ili wananchi waweze kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la afya na barabara nakadhalika. Kwanza kuna kile wanasema kishika uchumba; nikushukuru Mheshimiwa Waziri kupitia Rais wetu, tumeshapata kwenye majimbo zaidi ya milioni tayari 500 ziko kule, tunakupongeza sana. Kwamba hivi sasa tukirudi au kabla; kwamba TARURA, ukiacha bajeti waliyokuwa nayo tayari milioni 500 wameongezewa. Kwamba pamoja na hili la shilingi mia za mafuta nakadhalika tuna imani zitaongeza maendeleo makubwa upande wa barabara na zitatatua changamoto ambazo zinakumba katika maeneo yetu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko fedha nyingi ambazo tayari hivi sasa zimeenda. Fedha hizi za maendeleo ambazo ziko kwenye force account; fedha hizi Wameshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wabunge kama mlikuwa hamjui, hawaruhusiwi kujua au kushiriki kwa sababu mwongozo unasema anayetakiwa kuwepo kwenye ile force account ni mwananchi mmoja katika kijiji au katika mtaa kwa mradi ule ambao unafanywa katika sehemu ile, na engineer na watu wachache, Diwani haruhusiwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Diwani huyu ndiye badala yetu, ndio Wabunge wa eneo. Sasa Diwani huyu akiulizwa na wananchi hajui, akiulizwa anaambiwa wewe haumo kwenye kamati hii. Niombe sana Mheshimiwa Waziri, ili fedha hizi ziwe salama ni lazima Diwani aingizwe kwenye Mpango huu wa kusimamia shughuli za maendeleo katika eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nilipenda kwa leo niliseme, TANROADS wanafanyakazi nzuri sana, lakini kuna kipengele kimoja ambacho kimekuwa kandamizi kwa wafanyabiashara, nacho ni hiki; gari likiharibika barabarani au likapata ajali likadondosha oil au mafuta ya diesel au petrol barabarani adhabu yake ni kuanzia milioni 15 mpaka 40 na ushee. Adhabu hii ni kandamizi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba, kwa sababu tunasema tuwawezeshe wafanyabiashara ili waweze kufanya vizuri, ombi langu ni kwamba adhabu hii ikaangaliwe upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna watu wa EWURA wanafanyakazi nzuri kudhibiti mfumuko wa bei za mafuta nakadhalika, lakini nayo iko changamoto ambayo inatakiwa iangaliwe, ni kandamizi kwa wafanyabiashara. Kwa mfano basi linapoingia kujaza mafuta kwenye kituo anatakiwa ashushe abiria, kwamba asijaze mafuta akiwa na abiria. Akipatikana mwenye kituo anamjazia mafuta basi la abiria faini yake ya papo kwa papo ni milioni tatu. Hii ni sheria inayowakandamiza wafanyabiashara, niombe sana iweze kuondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo Mheshimiwa Mbunge wa Njombe Mjini, ndugu yangu Mwanyika amelizungumza sana hapa; kuhusu Mkoa wetu wa Njombe na kuhusu uwanja wa ndege. Uwanja ule ni uwanja ambao umekuwa kwenye Ilani kwa muda mrefu. tangu mwaka 2005 mpaka leo. Tunaomba; na sisi Njombe, kama alivyosema Mbunge, ni mkoa unaozalisha sana na ni mkoa tunaolima parachichi ambazo zimepata soko la dunia kwenye kilimo hiki cha parachichi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna Liganga na Mchuchuma; na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais jana alivyozungumza nyoyo za sisi wana Njombe na Watanzania yaani tumezuuzika sana. Kwamba Liganga na Mchuchuma imezungumzwa kwa miaka mingi, tatizo ni nini? Tutafute namna ya kulitatua tatizo hili la Liganga na Mchuchuma. Mheshimiwa Joseph Kamonga, Mbunge wa eneo husika amelizungumzia sana. Tatizo ni kulipa fidia za wale watu na kadhalika. Kwa hiyo tunaomba sana, Mheshimiwa Mwigulu tunakuamini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu suala la hizi benki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sekunde. Hizi benki zinatukopesha lakini riba zao ni kubwa Mheshimiwa Mwigulu. Mimi mwenyewe nimekopa juzi, kama mwezi mmoja hivi nimekopa milioni 600. Katika milioni 600 riba ni asilimia 19, hivi tunalipaje? Kipindi kilichopita nilikopa bilioni moja, milioni mia tano thelathini na mbili kwa ajili biashara zangu. Nimemaliza kulipa wamenipa barua ya kunishukuru riba peke yake wameandika kunishukuru pale milioni 918; nitawaonyesheni barua…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana mheshimiwa…

MHE. DEO K. SANGA:…milioni 918 ni bilioni nyingine. Kwa hiyo tunaomba benki waweze kupunguza riba kama ambavyo mama jana amesema ili tuweze kukopa na tuweze kufanyabiashara vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.