Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya, pia kwa usikivu ambao sisi wabunge tumekuwa na mambo mengi tumelalamika kwa muda mfupi lakini kwa muda mchache aliokaa madarakani tumeona ameanza kutekeleza kila Mbunge hapa amepata milioni mia tano kwenye jimbo, hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hongera sana Mheshimiwa Waziri umeanza vizuri na mimi kama Mbunge mzoefu kidogo nadhani mishale mikubwa tutakupiga Bunge lijalo, hakuna Mbunge ambaye hajaridhia na hajaridhika na Mpango huu wa Bajeti uliowasilisha kwetu. Tunaimani kama sasa utausimamia na kuyatekeleza yale ambayo umeyazungumza kwa kauli yako utakuwa umetubeba sana sisi Wabunge ambao bado tunahitaji kuendelea kuwa kwenye Bunge hili kipindi cha mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana katika suala la kupandisha na kuwachukua Waheshimiwa Madiwani kuwaweka kwenye bajeti ya Serikali. Mheshimiwa Waziri mimi ni zao la Diwani, mimi kuingia humu nimefanya kazi nzuri na ya mateso nikiwa kama Diwani, lakini baadaye nimepanda kuja huku Mheshimiwa Waziri umefanya kazi kubwa sana Diwani awe na mshahara unaotambulika na Serikali siyo hisani za Wakurugenzi, umetuheshimisha hata mizinga kule kwenye Baraza la Madiwani kwa Madiwani wetu na ninakushukuru leo Serikali imewatambua na kuwaweka kwenye mpango sasa mtalipwa mshahara kama mtumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulitekeleze na ikikupendeza sitaki kutamka kiwango bado mshahara wa madiwani ni mdogo sana ukilinganisha na majukumu yao kwa hiyo ukafikirie sitaki utamke ni shilingi ngapi kwenye windup, lakini…

T A A R I F A

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msukuma kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cecilia Paresso.

MHE. CECILIA DANIEL PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nataka nimpe taarifa mchangiaji kwamba kilichoridhiwa siyo mshahara ni posho badala ya kulipwa na halmashauri sasa inalipwa na Serikali Kuu, ukiongea habari ya mshahara ni habari nyingine ambayo ina utaratibu wake itakuja kuwa na makato yake, itakuja kuwa na pension na mambo mengi. Kwa hiyo kinacholipwa ni posho siyo mshahara. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Hilo moja, labda lingine ni kwamba, kwa sababu umetawaja wale wa kwangu, wale wakwangu hawahusiki kwenye mpango huo maana sisi ni jiji na tunaweza kujilipa wenyewe. Kwa hiyo, wale wapo vizuri Mheshimiwa Musukuma usiwe na wasiwasi.(Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, watanisaidia kuwaambia wale ambao wapo jirani na Jiji la Mbeya message yangu itafika. Mheshimiwa nilindie muda wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru iwavyo vyovyote vile kama taarifa ilivyotolewa, lakini naishukuru Serikali iwe posho, iwe mshahara iwavyo vyovyote ni jambo la msingi Mheshimiwa endelea kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwenye faini ya bodaboda, nataka nikuambie katika kitu ambacho Mungu atakukumbuka kukuongezea hata siku zako za uhai wako ni suala la faini ya bodaboda. Mimi nilikuwa najiuliza wachumi wetu mpo namna gani inawezekanaje faini ya bodaboda anayebeba watu wawili unamlinganisha faini na basi la watu 65. Mimi nilikuwa nashauri Mheshimiwa Waziri hata hiyo elfu kumi bado ni nyingi, tungeweka hata elfu mbili, lengo letu siyo faini!

WABUNGE FULANI: Aaah!

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mnabisha nini Waheshimiwa Wabunge.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilindie muda wangu, lengo siyo faini lengo letu ni kuwawezesha watu watoke kwenye bodaboda wanunue magari, hakuna mtu anapenda kuendesha bodaboda miaka mitano, miaka kumi anaumia kifua, kwa hiyo mimi nadhani bado mimi kama Mbunge nashauri hata hiyo elfu kumi umeanza vizuri, lakini tufikirie kwenda hata kwenye elfu mbili hata buku kwani kuna shida gani nchi ina pesa nyingi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia kuhusiana na suala la machinga, Mheshimiwa Waziri katika jambo ambalo nakuomba sana Mheshimiwa Waziri hamna tajiri yeyote anaanza kuwa tajiri bila kuhangaika huku chini. Machinga ni mtu muhimu sana Mheshimiwa Waziri na mimi niliona Dar es Salaam ni sehemu ambayo Watanzania wote tunaitegemea nilienda tu hizi siku mbili tatu nikazungukia kule Kariakoo baada ya kuona Mkuu wa Mkoa mmoja anasema tunaondoa machinga, nyinyi Waheshimwa Wabunge kama mnakumbuka Wabunge wenzangu wa CCM katika raha tuliyoipata kwenye uchaguzi wa 2020 ni pamoja na machinga kutuunga mkono, kwa sababu tuliwawezesha walikuwa busy na kazi zao hawakusikiliza mambo ya kudanganywa danganywa na wanasiasa ambao hawana mwelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo anasimama mtu mmoja anasema tuondoe machinga tuwarudishe vijijini, nendeni mkafanye research Dar es Salaam machinga wengi sasa hivi waliopo huko mitaani wengi wana degree moja na wengine degree mbili wameamua kujiajiri, pili, unapom- disturb machinga usidhani unamuharibia maisha yeye watu wengi waliopo kule kwanza tuliwaambia wanunue vitambulisho ili wafanye biashara yao kwa uhuru na Serikali imechuma bilioni 43 halafu leo gafla mtu mmoja anasema tuwatoe machinga unapomuharibia mtu biashara mnaharibia taasisi za kifedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wapo pale tayari wana mikopo, wamekopa, wamekopeshwa wanafanya biashara yao wanamarejesho eti tunathamini magari, kwani Mheshimiwa Waziri tuna shida gani tukisema magari yasiingie Kariakoo ili iwe center ya biashara watu wafanye biashara yao kwa uhuru wasibugudhiwe. Hii kitu Mheshimiwa Waziri mimi huwa najiuliza hivi mnaona faida gani magari yaingie elfu moja ambayo hayalipii au kuachia machinga wafanye biashara kwa uhuru kama tulivyowaahidi halafu nyie mkusanye kodi. Machinga ndiyo anafanya research ya biashara Tanzania nzima nyie wote wenye degree hapa hakuna mtu anafanya research ya biashara machinga hauzi kitu ambacho hakinunuliwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara ndiyo watu wanaowategemea leo mtu mmoja anasimama ndiyo maana huwa najiuliza tunao Wachumi nchi hii au tuna vicheche tu, maana siwaelewi kabisa. Kwa hiyo niwaombe sana mliangalie wasisumbuliwe hawa watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma hebu usiwaite watalaam wetu vicheche tafadhali, ondoa hilo neno kwa sababu wamesoma ili watusaidie na haya yote tunayoipongeza Serikali wachumi wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaliondoa, lakini wafanyekazi kwa ufasaha wadhihirishe yale waliyoyasoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nimeona kwenye kodi za wachimbaji wadogo unapendekeza kuongeza kodi Mheshimiwa Waziri nikushauri kumbuka kabla hatujarekebisha kodi za wachimbaji wadogo Serikali ilikuwa inakusanya bilioni 168 baada ya marekebisho ya sheria tupo bilioni 544. Ukiongeza kodi ukiwanyima faida wafanyabiashara ya elfu mbili, elfu tatu utaongeza utoroshaji hutapata hela hii, nikuombe sana ondoa hayo mawazo ya kuongeza hiyo asilimia tatu sijui asilimia saba tufikirie zaidi kupunguza kwa sababu tunaona tunawekeza mpaka viwanda vikubwa hapa halafu tunaongeza masuala ya kodi siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nazungumza kwa upole sana kwa sababu Mheshimiwa Ndumbaro ni Waziri ambaye ni rafiki yangu kuhusu suala la Ng’ombe. Mimi nipo humu Bungeni nimeshuhudia mawaziri wawili Mzee Magembe alikaa pale na rafiki yangu ndugu yangu Mpina na juzi amelizungumza kwa uchungu kuisumbua Ng’ombe sidhani kama tunafanya sahihi hata kutuchaji tu elfu hamsini Ng’ombe ikikamatwa kwenye maliasili kule mbugani haifai, kwa sababu Ng’ombe haina uharibifu wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tufanye ulinganisho, tembo akienda kula mahindi hana faini Ng’ombe akienda kula majani anafaini kwa sababu gani? tufikirie kuondoa hii faini Ng’ombe anaenda kula majani na hii ni roho mbaya kwa wataalam Ng’ombe akiingia kula majani aharibu miti na mwisho wa siku majani mnayachoma moto sasa sielewi mnajenga viwanda vya kuchinja wapi kule Dar es Salaam na sehemu zingine machinjio za kimataifa halafu Ng’ombe mnazipiga vita mnataka kuchinja fisi au mnachinja vituo gani.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana Mhehimiwa Waziri tuondoe faini haiwezekani twende hata kitaalam tu kwamba kama ni sahihi kumkamata mtu ana Ng’ombe ukaichaji laki moja au elfu hamsini wakati thamani ya Ng’ombe ni laki mbili hebu tujaribu ma-traffic wakikamata VX wakuchaji milioni mia nusu ya bei uliyonunulia mbona tutayakimbia magari. Nifikirie sana Waziri kukushauri kwamba tuondoe hizi kodi ambazo zinaonea watu na tuache Ng’ombe ya Mtanzania itembee na uhuru popote ambapo itataka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho nimemsikia Mheshimiwa Rais jana ameelekeza kwa uzuri tu, kwamba dhahabu ziingine kutoka Kongo na sehemu zingine, ni kweli, lakini Mheshimiwa Waziri naujua udhaifu tulionao naomba uzungumze na watu wako wa TRA wasisumbue wafanyabiashara. Wafanyabiashara wanapeana taarifa kuliko hata mitandao ya simu akikamatwa mmoja tu, wanaambizana wote hawaji na tunafungua viwanda tunategemea material kutoka Kongo ambapo kuna dhahabu ambazo hazina utaratibu. Kwa hiyo nikuombe sana tuwape uhuru wafanyabiashara na wasisumbuliwe na mambo ya polisi na mambo ya TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana. (Makofi)