Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kukushukuru wewe kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hoja ya mawasilisho matatu yaliyofanywa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusu Hali ya Uchumi wa Mwaka 2020, Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na watumishi wote wa Wizara ya Fedha na taasisi zake zote kwa kutuandalia bajeti nzuri ya kimkakati kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba kumuita kwa jina hili; the Tanzanite super woman of our time. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu ameanza vizuri uongozi ndani ya Taifa letu kama Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita. Bajeti iliyowasilishwa siku ya tarehe 10, Juni, 2021 inadhihirisha umakini, ujasiri na weledi wake katika eneo la uchumi wa Taifa letu; pongezi nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia bajeti hii inathibitisha msemo wa wahenga unaosema mama ni nguzo na mlezi wa familia. Nayasema haya kwa sababu kuu mbili kwa siku hii ya leo kwa sababu ya muda; sisi sote Watanzania ni mashahidi kwamba chini ya uongozi thabiti wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na msaidizi wake namba moja mama Samia Suluhu Hassan, Taifa letu limehimili mtikisiko na mdororo wa uchumi wa athari ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19) kwa mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu katika taarifa iliyowasilishwa, Taifa letu ni miongoni mwa mataifa 11 tu kati ya Mataifa 45 yaliyo Chini mwa Jangwa la Sahara ambayo uchumi wetu umekuwa kwa ukuaji chanya wa asilimia 4.8. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mataifa 43 yaliyo chini ya Jangwa la Sahara ukuaji wao wa uchumi umekuwa kwa ukuaji hasi, na mataifa mawili yameona ukuaji wao wa uchumi ni sifuri. Hakika tunastahili kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuweza kuhimili mtikisiko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uhimilivu huo wa uchumi wetu haujaletwa na jambo jingine bali ni ujasiri, uthubutu wa viongozi wetu wakuu na sasa tukiongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipotuambia Watanzania tufanye kazi wapo wenzetu walitukimbia humu Bungeni tuache kupitisha bajeti, lakini kwa umakini wa viongozi wetu tulisimama imara bajeti tuliyoipitisha ndiyo hii leo inatueleza zile mbinu zote na mikakati mbalimbali tuliyoitekeleza imewezesha Taifa letu kuwa moja ya nchi chache zilizoweza kuhimili mtikisiko huu wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo limesababisha nimsifu Mheshimiwa Rais wetu, katikati ya kipindi hiki kigumu cha Corona mwaka 2020 tuliona Taifa letu likiingia katika kundi la nchi zenye hadhi ya uchumi wa kipato cha kati, miaka mitano kabla ya kipindi tulichojiwekea Watanzania kwenye Dira yetu ya Maendeleo ya Taifa. Hili nalo jambo tunasema ni jambo ambalo limeishangaza dunia tumewezaje kama Taifa, tumeweza kwa sababu tuna viongozi jasiri na sasa tuna mwanamama shupavu anayetupa miongozo ya kutenda yaliyo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu moja kubwa iliyofanikisha Taifa letu tuweze kuingia katika nchi zenye hadhi ya uchumi wa kipato cha kati ni uwekezaji kwenye miradi mikubwa ya kielelezo. Ukisoma bajeti iliyowasilishwa pamoja na Mpango wa Pili wa Maendeleo, tunaona commitment kubwa ya Serikali yetu ya kwenda kuikamilisha miradi hii ya kielelezo ambayo itaendelea kutuwezesha kufanya uchumi wetu uendelee kuwa imara. Pongezi nyingi sana kwa Rais wetu na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, commitment hii ya Mheshimiwa Rais inadhihirisha nadharia ya uwekezaji kwenye miundombinu (theory of economics of infrastructure investment) inayotuambia kwamba uwekezaji kwenye miradi mikubwa hasa ya miundombinu lazima ifanywe na Serikali yenyewe. Jambo ambalo tulisimama imara Serikali ya Chama Cha Mapinduzi tukasema tunakwenda kuwekeza kama Serikali kwa sababu tunahitaji kuona matokeo chanya ya uwekezaji wetu huu ambao tunaufanya na ambao tayari tumeshaona matumaini makubwa ndani ya uchumi wetu ulio imara kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo naomba sasa niishauri Serikali yangu. Nianze kwa kupongeza kwa kupeleka asilimia zaidi ya 37 ya bajeti nzima kwenda kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka huu 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili thamani halisi ya fedha zetu asilimia 37 zaidi ya trilioni 13 tunazozipeleka kwenye Miradi ya Maendeleo iweze kuonekana kwenye maisha halisi ya wananchi wetu naomba kushauri mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba Serikali yetu sikivu iimarishe Idara ya Mipango ya Kitaifa; Idara ya Mipango ya Kitaifa iwezeshwe ili iweze kufanya kazi yake ya tathmini na ufuatiliaji wenye tija kwa ajili ya Taifa letu. Idara hii inapendekeza iwezeshwe katika maeneo makuu matatu; eneo la kwanza iwezeshwe kwenye eneo la Rasilimali fedha, eneo la pili iwezeshwe kwenye eneo la Rasilimali watu na eneo la tatu iwezeshwe kwenye eneo la rasilimali teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu tukiiwezesha Idara hii ya Mipango ya Taifa inaweza kufanya kazi kubwa ya kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo na fedha nyingi zinazowekezwa na Serikali yetu kwenye miradi ya maendeleo. Tatizo kubwa la ndani ya Taifa letu siyo upelekaji wa fedha bali ni usimamizi, ufuatiliaji na kufanya tathimini ya fedha zile tunazozipeleka kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kushauri katika idara hii, pia niombe sana tunahitaji kufanya kubadilisha mfumo wa kitaasisi wa jinsi kazi ya ufuatiliaji na tathimini inayofanyika ndani ya Serikali yetu. Wizara ya Fedha na Mipango naomba sana muweke nguvu kwenye neno Mipango ndani ya Wizara yenu hapa ndipo kwenye kupanga mipango kwenye ufuatiliaji kuhakikisha kwamba tunahakikisha tunapata thamani halisi ya fedha inayopelekwa kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni eneo muhimu sana kwa sababu mara nyingi tumeona tukifanya ufuatiliaji baada ya miradi kukamilika. Hili jambo linapelekea fedha nyingi za Serikali kupotea, nipendekeze ikiwapendeza Serikali yetu tuwe na real time monitoring and evaluation ya miradi yote tunayopeleka fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tuanze kufuatilia…

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sekunde thelathini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kwamba kabla fedha haijapelekwa idara hii ya mipango ya kitaifa ikajiridhishe na eneo ambalo tunakwenda kuwekeza, lakini mchakato mzima wa manunuzi ukoje kwa sababu miradi mingi tunaona wanachelewesha katika eneo la manunuzi, fedha nyingi za Serikali zinapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya pia ufuatiliaji wakati wa utekelezaji naamini alichokisema Mheshimiwa Rais jana pale wakati anazindua jengo la Benki Kuu pale Mwanza, kwamba pesa iliyowekezwa ni kubwa kuliko jengo linaloonekana hatutoweza kusikia kauli hizi tena kwa sababu idara hii itafanya kazi yake inayotakiwa na thamani halisi ya fedha itaonekana.

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)