Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nichangie katika Wizara yetu hii ya Fedha. Niungane na wenzangu kumpongeza Dkt. Mwigulu kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, yeye ni Mchumi mbobevu katika eneo hili, naamini Wizara hii ataitendea haki.

Nampongeza pia Engineer Masauni kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri. Wizara hii ndio Wizara yenye hazina ya nchi yetu na ndio inayofanya disbursement ya fedha katika Wizara zote na Mafungu yote katika sekta mbalimbali, baada ya kupitishwa na sisi Wabunge katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu kuishauri Wizara na Mawaziri, wajitahidi sana kugawa kwa uwiano fedha ambazo zimetengwa katika Wizara zetu. Wagawe kwa uwiano na kwa wakati ili kuweza kusukuma maendeleo ya nchi yetu yaweze kuendelea zaidi na zaidi.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii katika bajeti inayoishia sasa hivi mpaka mwezi Aprili yenyewe, Wizara, imeshajigawia asilimia 68.5. Kwa hiyo, naomba kuwaomba kama Wizara iangalie pia, ifanye tathmini Wizara zingine imezigawia nazo mpaka sasa Aprili, asilimia 68.5? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa mpaka mwisho wa mwaka wa bajeti, mwisho wa mwezi huu, Wizara hii itakuwa imeshajigawia asilimia 100 ya matumizi ya Wizara. Kwa hiyo, naomba sana nayo iangalie Wizara zingine nazo pia zipate hivyo hivyo, Mafungu hayo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nizungumzie kuhusu eneo la majukumu ya CAG. CAG kama controller General kazi yake ya kwanza ni kudhibiti mapato ya Serikali, matumizi ya Serikali na mali za Serikali. Kazi yake ya pili ni Auditor General ambayo ni kufanya ukaguzi wa masuala yote niliyoainisha hapo mbele. Kwanza, kuhakikisha kwamba mapato yote ya Serikali yanakusanywa na kuhifadhiwa kwa wakati kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizowekwa. La pili, matumizi ya Serikali yanafanywa kulingana na bajeti kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha. La tatu, mali za Serikali zinatunzwa kwa umakini mkubwa na kwa manufaa ya Watanzania tuliopo sasa hivi na kizazi kijacho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, CAG anapokwenda kwenye Taasisi au Wizara anakuwa kama External Auditor, lakini ndani ya Taasisi, Wizara au Halmashauri tuna wale Internal Auditors. Hawa wanakuwa accountable kwa Afisa Masuuli au returning officer wa taasisi husika. Sasa External Auditor kama CAG anapokwenda pale, anategemea sana taarifa za Internal Auditor. Hata hivyo, Internal Auditor kama kuna upungufu kwenye taasisi naye, yuko answerable kwenye Management ya Taasisi, kama atakubaliana na upungufu ule na taasisi au Afisa Masuuli, basi taarifa anazoweza kupata CAG zinaweza zikam-lead tofauti. Ndiyo matokeo haya tunayoyakuta baadaye kwamba kuna ubadhirifu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye hili, naiomba Serikali, eneo hili la Internal Auditor kama inawezekana wawe accountable moja kwa moja kwa Internal Auditor General Hazina ili kuweza kufanya kazi yao ipasavyo. Kwa sababu wengine unaweza ukakuta kwa mfano, bandari miaka ya nyuma, Internal Auditor pale waliweza kumhamisha, kwa sababu hakutaka kuendana nao wanavyotaka, wakampeleka Musoma huko wakati yeye alikuwa ni Internal Auditor wa Bandari, lakini ni kwa sababu hawakuwelewana tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri Internal Auditor angekuwa Accountable kwa Internal Auditor General kule ili taarifa zake zote awe anazipeleka kule. Pia CAG awe anazipata kule anapokwenda anaanza nazo taarifa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na utatuzi wa changamoto zinazojitokeza na kutoa ushauri kwa CAG, lakini fedha zimekuwa zikiibiwa kupotea ama kutumiwa vibaya bila kunufaisha Taifa na wananchi wake kwa ujumla. Taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Serikali zenye Hati zenye mashaka ni dhahidi kuwa zinahitaji zaidi ukaguzi wa kina au kuzipeleka katika vyombo husika kufanyiwa uchunguzi zaidi. Hata hivyo, sheria inamtaka CAG atoe ushauri.

Mheshimiwa Spika, ningependa CAG kama anakabidhiwa Sheria ya kupeleka moja kwa moja TAKUKURU, ingekuwa bora zaidi. Kwani kutoa tu taarifa ya Hati zenye mashaka peke yake, hakuna tija. Naomba kama Sheria iliyoiunda Ofisi ya CAG bado ina upungufu au inahitaji mapitio, basi ingeletwa hapa Bungeni, tuyafanyie mapitio hayo ya kuwapa nguvu zaidi Ofisi ya CAG ya uchunguzi zaidi na kushirikiana na vyombo vingine ili kuwezesha Serikali yetu kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Msajili wa Hazina, naomba nizungumzie kidogo mwishoni. Sisi kule Namtumbo kuna shamba lililokuwa la NAFCO na shamba hilo sasa hivi liko chini ya Msajili wa Hazina. Watu wakitaka kulima, lazima walipie Hazina, naamini ni kama shilingi 10,000/= hivi kwa eka. Kama Halmashauri tulishaiomba siku nyingi; liko ndani katikati au kwenye ramani ya Mji wa Namtumbo. Kwa hiyo, tunaomba sana, tufahamu hatima ya shamba lile ni nini; ili tuelewe mtaturudishia kama Halmashauri, na tungeomba hivyo au mtamweka mwekezaji kulima kama ilivyokuwa NAFCO zamani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba hilo, kwa sababu lipo shamba katikati ya ramani ya Mji wa Namtumbo. Tunaomba sana ama turudishiwe au mwone jinsi gani tunajua hatima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)