Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze mwananchi mwenzangu, Mheshimiwa Mwigulu, kwa hotuba nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ninapenda nitumie aya moja katika Surah Al-Fatiha iniongoze kwa haya ambayo nataka niyaseme. Aya hii inasema iyya qa budu-wa iyya qa nastaeen. Tunamwambia Mwenyezi Mungu kwamba wewe ndiye tunayekuabudu na wewe ndio tunayekuomba msaada.

Mheshimiwa Spika, msaada ninaouomba leo hii kwa Mwenyezi Mungu ni kwamba amuongezee busara nyingi sana mwananchi Mwigulu Nchemba, haya maneno yaliyotolewa na Wabunge basi uyapokee. Na ikiwezekana vilevile kwa kuwa umefanya vizuri sana katika hotuba hii, utupatie pia mchongo tarehe 03, Julai mambo yanakwenda kuwa namna gani, itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kupongeza hatua kadhaa ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imechukua katika masuala mazima ya ukusanyaji wa mapato pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita, lakini inatiwa doa na watu wachache pale Ministry of Finance. Watu ambao wameamua kwenda kujichotea mapesa kama vile Sakata la Mheshimiwa Waziri Mkuu lilivyoeleza.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali; fanyeni history. Fukuza kila mtu aliyemo katika mnyororo ule, hata kama ni mkubwa kiasi gani. Kwa sababu tumechoka, sisi tunaomba barabara, tunaomba dispensaries, Waziri anasema fedha zikipatikana. Fedha zinapatikana watu wamechukua. Halafu unasema kwamba fedha zikipatikana. Zipatikane mara ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Gavana wa Benki Kuu. Juzi tulimuuliza katika Kamati; wlae waliosababisha bureau de change zitumike vibaya na kuiletea Serikali hasara, hawa watu bado wako kazini? Akasema amewafukuza watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ameweza kufanya Gavana, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, unawasubirisha nini hii mijitu hii? Inatuletea tabu. Na ndiyo maana kuna baadhi ya votes (mafungu) wanaweka fedha zao mle, wanazificha mule ili wapeane maposho a vile hakuna Serikakamli. Hili suala naomba mliangalie.

Mheshimiwa Spika, na namuomba sana Mheshimiwa Mwigulu, mchango wa Kamati, hotuba ya Kamati ya Bajeti ambayo ni mjumbe, naomba aiangalie sana. Mle ndani mna madini kwelikweli; kayafanyie kazi na hakika ataboresha vizuri zaidi utaratibu wa uendeshaji wa Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda nipumue kitu kimoja new thinking katika mawazo ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge. Namba moja, nafikiri kuna kitu unakifahamu Mheshimiwa Saashisha hapa aliwahi kuwaona Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Kamishna Mkuu wa TRA, kuna kitu ambacho kimebuniwa na Watanzania, vijana hawa wa IT, kinaitwa Simply Tech kinachokwenda kujaribu kuongeza mapato katika ukusanyaji wa mapato, utoaji wa risiti, utengenezaji wa mahesabu ya mfanyabiashara lakini vilevile kwa faida ya TRA.

Mheshimiwa Spika, naomba sana hao Watanzania ambao wanakuja na kubuni mambo ambayo yanaweza yakaleta masuluhisho katika matatizo ya utoaji na upokeaji wa risiti, hebu Serikali liangalieni hili ili muweze kuona kwamba hawa vijana wetu wanachangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la TRA; TRA tumekubaliana kwamba private sector ndiyo engine ya uchumi wa nchi hii. Na tukaenda mbali, hata katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, kuonesha ni jinsi gani matatizo ya ulipaji kodi yapo.

Mheshimiwa Spika, nataka niangalie upande mmoja, kwamba wafanyabiashara wanalalamika kuhusu ucheleweshaji wa kufanyiwa tax audit. Niliwahi kulizungumza hapa. Lakini tukafikiria kwamba ni jambo jepesi, kwamba mfanyabiashara hafanyiwi tax audit hadi miaka miwili au mitatu iwe imeshapita; inatengeneza interest, inatengeneza penalties. Kiasi kwamba hata mwisho wa siku inapoletwa hesabu yake hata fedha za kulipa hana kwa sababu anakula mtaji wote.

Mheshimiwa Spika, katika utafiti mdogo niliofanya nilitembelea Mkoa wa Kikodi wa Kinondoni nikazungumza na viongozi pale. Tatizo jamani siyo TRA, tatizo ni Serikali hawataki kuwapatia wafanyakazi wa TRA idadi kamili ya wafanyakazi wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, niwape habari; Mkoa kama wa Kinondoni ambao unapokea kitu wanachoita tax returns zaidi ya 10,000, lakini ina tax auditors 24, kila tax auditor mmoja, au wote hawa kwenye tax plan watengeneze na kujibu tax cases 360; ni lini watafikia returns 10,000?

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana hata hizi fedha ambazo zinawekwa malengo ya kukusanya naziona ndogo sana. Mkiwapatia wafanyakazi wa kutosha TRA nina hakika wataweza kufanya vizuri. Kinondoni pamoja na uchache wa wafanyakazi wamepangiwa mwaka huu wakusanye bilioni 820, ninavyozungumza wameshafikia asilimia 92; kwa uchache wao. Suppose mnawapatia wafanyakazi wa kutosha?

Mheshimiwa Spika, kule kuna vitu wanaita blocks management ambapo wao wanahusika na masuala yote ya tax compliance. Kila block moja ina watu wanne mpaka watano, hebu niambie Mwananyamala kuna watu wangapi pale ambao wanafanya shughuli za kibiashara, wanafikiwaje na watu hawa wanne/watano huo ni mzaha!

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kila Mbunge akisimama anaiomba Serikali, Mheshimiwa Mwigulu naomba unisikilize, tuongezeeni wafanyakazi TRA kwa sababu tunahitaji kukusanya fedha zaidi. Idadi ambayo mmeitangaza juzi tarehe 1 Juni, eti mnakwenda kuajiri watu 48, siyo mzaha huu? Ndiyo maana shemeji yangu Kilumbe anauliza ni busara? Hivi kweli ni busara watu wanahitaji wafanyakazi mkaajiri watu 48 mnawapeleka wapi, Kinondoni au Ilala maana huko ndiyo kwenye fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hebu fanyeni kitu kimoja, Rais aliyepita Mheshimiwa Jakaya anasema huwezi kula bila kuliwa, hebu tuajiri watu tuwalipe mishahara watufanyie kazi. Tusing’ang’anie watu wachache tuwape malengo madogo wanayatimiza tunawapigia makofi, kuna fedha nyingi huko nje, returns 10,000 plus halafu kwa mwaka unashughulikia kesi 360 yawezekana vipi? Ndiyo maana watu wanapiga kelele kwamba mnawacheleweshea kuwakagua kwa sababu hakuna wafanyakazi wa kutosha.(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunazungumzia EFD machines, tena huko ndiyo kwenye matatizo. Kinondoni Region ina watu wanne halafu tunasema masuala ya kudai risiti na kutoa risiti, watu wanne kwenye mkoa mkubwa kama ule Tanzania, hakuna mkoa mkubwa Tanzania zaidi ya Kinondoni. Ni busara kweli Mheshimiwa Mwananchi mwenzangu, watu wanne EFD machines halafu huku tunasema watu hawadai risiti na hawatoi risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumza haya lakini ni mambo ambayo yanafanya hata ukusanyaji wa kodi uwe ni wa mashaka. Nina hakika kabisa Serikali sikivu kama ya Mama Samia Suluhu Hassan na Mwananchi pale pamoja na Waziri Mkuu mkienda mkikaa mkifanya caucus yenu angalieni suala la kuongeza idadi ya wafanyakazi ndani ya TRA you will never go wrong. Hiyo mtakuja kutuambia kwamba Wabunge kweli mmeiwashauri Serikali vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nimalize kwa kusema nampongeza Mwananchi na vilevile naiunga mkono hoja iliyopo mbele yetu. Ahsante sana. (Makofi)