Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai na ametufanya leo hapa tumetokea tupo wazima katika kuangalia mustakabali wa Taifa letu, napenda kukushukuru na wewe kwa kunipa nafasi hii nafasi ya kwanza ili kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, kuna msemo wa Kiswahili unasema kwamba “penye nia pana njia” na msemo huu penye nia pana njia nimeuona kwa macho yangu katika mwaka 1984, mwaka 1984 wakati ule Mzee Mwinyi anakuja kugombea Urais wa Zanzibar, anakuja kutambulishwa kwamba ni Rais wa Zanzibar basi alizungumza neno moja ambalo mpaka leo linatumika na hakuna mtu ambaye anaweza akalisahau. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi hicho tukiweka foleni za makopo kwa ajili ya kupanga foleni ya mchele pengine wiki, wiki mbili mwezi lakini alivyokuja yeye akasema kwamba anachotaka mtu ataweka tui jikoni halafu atakwenda dukani kununua mchele ili aje apike wali wake, kwa maana hiyo limekuja limetoka na limekuja likatokezea mtu anakwenda kuchagua mchele kwa kunusa na tui lipo jikoni au maji yapo jikoni unakwenda dukani. Sasa ni sawa kwakuwa kulikuwa na nia na njia ikapatikana na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema kwamba ataendelea na kazi zote ambazo zilizoanza katika Awamu ya Tano na yeye atazikamilisha katika Awamu hii ya Sita.

Mheshimiwa Spika lakini pia amepanga kuboresha mazingira ya biashara na pia ukusanyaji wa Kodi na Watanzania tunatakiwa tuhamasike ili tuweze kulipa kodi na pia tutoe ushirikiano mzuri kwake maana yake penye nia pana njia na hapo pia tunaweza tukaja tukabaini tukapata tena ule wali nazi kama kwa mzee Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu leo nitakwenda fungu Na. 10 lakini pia nitagusia Fungu Na. 7 ambapo kuna usimamizi wa TRA kwa msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Spika, Fungu Na. 10 hili ni Tume ya pamoja ya fedha, katika Tume hii ya pamoja ya fedha Kamati wamesema kwamba imepewa majukumu maalum, jukumu moja ni kufungua hiyo akaunti ya pamoja. Lakini jukumu lingine ambalo kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 134(2)(b) inasema kuchunguza kwa wakati wote mfumo wa shughuli za fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili.

Mheshimiwa Spika, ninazungumzia huo mfumo wa ushirikiano wa kifedha kati ya Serikali mbili, na mahali ninapoanzia, naanzia na TRA tunafahamu wote kwamba VAT ni asilimia 18 kwa Tanzania Bara, lakini VAT kwa Zanzibar ni asilimia 15 ina maana kwamba kuna tofauti ya asilimia tatu ya VAT. Sasa tunatumia huduma za pamoja kwa mfano ukifanya muamala wa kibenki unakatwa asilimia 18 ukifanyia kule Zanzibar ulipaswa ukatwe asilimia 15 lakini unakatwa asilimia 18 kwa sababu mifumo inayokusanya ni mifumo ya TRA ndio inayokusanya hayo mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kule Zanzibar zina kwenda asilimia 15 lakini huku alizokatwa mteja ni asilimia 18 sasa mimi nilikuwa ninajiuliza hii asilimia tatu huwa inakwenda wapi? Na mifumo hii ya kifedha kama haitokaa sawa ina maana kwamba moja kwa moja inaweza ikaleta matatizo sasa tokea umeanza mwaka wa fedha uliopita ambao huu tunaomalizia ina maana kwamba kule Zanzibar wamekatwa asilimia 18 lakini zilizopelekwa ZRB ni asilimia 15 sasa nilikuwa ninauliza hii asilimia tatu hizi fedha zimekwenda wapi? Kwa hiyo, nilikuwa ninamuuliza Msajili wa Hazina lakini pia na TRA hizi ni fedha ambazo zipo na hili fungu namba 10 ndilo linaloshughulikia mifumo hii ya pamoja ya kifedha kwa hiyo waje watupe majibu ya hili, na kwa sababu hatutaki liendelee kwa mwaka huu tayari tumeshaliacha limeshakuwa ni mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunaenda huko mbele kule Zanzibar VAT asilimia 15 huku asilimia 18 inayokatwa ni asilimia 18 lakini inayopelekwa ZRB na TRA ni asilimia 15 kwa hiyo, kwanza atueleze asilimia hii tatu inakwenda wapi. Na kingine waje watuambie solution katika hili kwa sababu haliwezi kuachwa likaendelea na wao ndio tuliwapa watutafutie ufumbuzi huo.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo jingine baada ya mitandao ya simu kuanza kukatwa katika mwaka 2009 mpaka mwaka 2015 zimekatwa fedha za VAT na exercise duty katika miamala ya simu, fedha hizi ni bilioni 14.7, Bilioni14.7 na pia kuna fedha nyingine ambayo minara yake ipo Zanzibar, minara ipo Zanzibar ambayo Kampuni ya HTT company imetoa fedha imelipa kwa TRA bilioni 1.7 lakini fedha hizi bado zipo TRA.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna VAT tangu mwaka 2011 ya bilioni 11.8 ambazo fedha hizo zinafanya ujumla kuwa ni bilioni 28.1 fedha hizi kwa masikitiko makubwa zipo TRA, ZRB hazikupelekwa. TRA alikusanya kwa niaba ya ZRB kwa hiyo hakuzipeleka. Lakini hazina ilichukua juhudi na ikasema kwamba hizi fedha zirudishwe wakati wa Kamishna Charles Kichele na kule Amour Amir walikubaliana kwamba hizi fedha zitapelekwa.

Mheshimiwa Spika, lakini hizi fedha mpaka sasa hivi tunavyozungumza bado hazijapelekwa, sasa nilikuwa ninajiuliza Hazina tayari mmeshasema kwamba hivi fedha zipelekwe, TRA ana mabawa gani ya kuikatalia Hazina kutopelekwa hizi fedha? Kwa hiyo, nilikuwa niiombe Serikali na kwa kuwa Charles Kichele wakati huo ndio yeye alikuwa anajua hili jambo sasa hivi ni CAG lakini Kamishna aliyekuwepo sasa hivi naye pia anafahamu juu ya hizi fedha kwa hiyo ilikuwa tunaomba hizo fedha zipelekwe.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine lalamiko la TRA kutopeleka hizi fedha wanasema wakati huo ilikuwa hakuna sheria ya marejesho lakini pia wakati huo ilikuwa hakuna fedha za kumshikia mwenzako hakuna sheria ya kumshikia mwenzako fedha kwa hiyo nilikuwa niiombe Serikali ijaribu kuliangalia hili suala na tunaeleza hapa katika fungu namba 10 suala hili pengine kama hatutopata majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri au ya Serikali tunataka pia kuzuia shilingi kutokana na suala hili, kwa sababu haiwezekani TRA ikatae jambo la Hazina na kulifanyika reconciliation kumefanyika auditing kila kitu kilifanyika na kikakamilika na walikubaliana lakini mpaka sasa hivi fedha hazijaenda.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia fungu Na. 10 kupitia fungu Na. 7 wakae hili jambo walishughulikie hili jambo liweze kutatuliwa hasa hili la kodi katika miamala VAT asilimia 18 na 15 hapa kama hatutoweka sawa litaendelea na fedha hizo zitaendelea zitakuja kuwa nyingi tutajiuliza je ni za kampuni ya simu ni za wananchi au ni za ZRB hiyo asilimia tatu. Kwa hiyo, patakuja kuleta utata huko mbele na baadaye itaweza ikazusha sito fahamu lakini kutokana na lengo la hili fungu namba 10 Tume ya pamoja wao wanatakiwa wachunguze kwa wakati wote mfumo wa shughuli za fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mahusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali hizi mbili kwa hiyo kazi hii ni ya Kikatiba na sisi tunawaambia hilo jambo waende wakalifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)