Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo ada nami nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ndumbaro na Naibu wake na watendaji wote wa sekta ya maliasili kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia na kulinda rasilimali muhimu sana ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema mambo machache miongoni mwa mengi ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge. La kwanza nafikiri nifafanue tena kazi ambayo Serikali imeshafanya, nataka kuwapa tu taarifa Waheshimiwa Wabunge kwa kutambua mengi ambayo yanasemwa hapa kwamba idadi ya watu na shughuli zao zinaongezeka na wananchi sasa wamekuwa wengi sana, lakini hifadhi zimebaki vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwakumbusha kwamba Serikali ilishafanya uamuzi na imefanya uamuzi baadhi ya maamuzi ni kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kwa kutambua hilo Serikali imefuta Mapori Tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari laki 707,659.4. Haya mapori yalikuwa na GN zao yamehifadhiwa kwa mujibu wa sheria na Serikali imechukuwa jukumu la kuyafuta ili yapangwe yaweze kutumika kwa shughuli za binadamu za kilimo na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji umeshafanyika, Wizara ya Maliasili imeelekezwa na Waziri amesha-degazette, yaani ameshayaondowa kwenye orodha ya Mapori Tengefu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, baada ya hapo Serikali imeshafuta, iliagiza misitu yenye ekari 46,715, hifadhi saba za misitu ambazo zimekosa sifa kwa sababu ndani yake kuna watu, kuna shughuli za binadamu na nini, hizi nazo zimefutwa, ekari 46,715 za misiti zimefutwa ili wananchi waendeleza shughuli zao za kilimo na mifugo katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya maeneo ni yale yaliyokutwa angalau tunasema wavamizi, lakini wananchi wameingia katika maeneo hayo, wameanza kujishugulisha na shughuli mbalimbali za kibinadamu humu ndani. Kwa hiyo Serikali ilishafanya uamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, uamuzi mwingine uliofanywa pamoja na kwamba haya yameshakuwa degazetted, lakini bado Serikali ikasema hapana tuangalie tena maeneo mengine ya hifadhi za misitu 14 ili tukayapunguze na yenyewe yatumike kwa shughuli za kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naweza nikasema haya ni kwamba, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge labda shughuli za kutekeleza haya hamjaziona, lakini kama nilivyoahidi mara ya mwanzo kwamba sasa mwaka huu tumeweka bajeti wizara husika ili sasa tushirikiane na wananchi wa maeneo hayo na viongozi wa maeneo hayo, tuwaonyeshe kabisa, tunaposema hizi ekari laki saba ni zipi na watu gani watanufaika nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema misitu hii ekari 46,000 zimepunguzwa au zimefutwa ni ipi na iko katika maeneo gani. Tunaposema misitu mingine au hifadhi za misitu
14 zitapunguzwa ni maeneo gani, lakini haya naweza nikasema baadhi ya maeneo ya hifadhi ambayo tunatarajia kwenda kuyapunguza mengine yanapatikana katika maeneo ya Uliyankulu, Geita, Rwamgasa, Lwande, Usindankwe, Ushirombo, Mbogwe, Bukombe, Runzewe, Biharamulo, Kahama, Miyeze, Tongwe East, Masanza, Uyui Kigwa Rubuga na Loasi River. Haya ni baadhi ya maeneo ambayo yana hifadhi za misitu ambazo Serikali imefanya uhamuzi lazima hifadhi hizi zipunguzwe ili wananchi waendelee na shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi mwingine ni ule ambao tumekuwa tunausema mara zote kwamba Serikali ililetewa orodha ya kitaifa kwamba vijiji vipatavyo 975 inaelekea ndio vina mgogoro. Ni bahati mbaya sana hii orodha iliandikwa na Wabunge waliopita, lakini na Wakuu wa Mikoa na Wilaya, tutaileta kwenu muione hiyo orodha ya vijiji 975, kila mkoa na kila wilaya pengine ninayoyasema sio vijiji hivi. Kitaifa tulishafanya uhakiki na tukajua ni vijiji 975. Uamuzi wa Serikali ni kwamba vijiji 920 vinabaki na usajili wao lakini kuna kazi ndogo baadhi ya vijiji itafanywa ya kurekebisha mipaka, lakini haitafuta usajili wa vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji 55 vilivyobaki ndivyo tuliambiwa tuendelee kufanya utafiti, tumeshamaliza kama nilivyowaambia, tunapeleka taarifa kwenye Baraza la Mawaziri na watatupa uamuzi. Kwa hiyo, ninachotaka kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba concern yenu na sisi ndio concern yetu kama Serikali, nimeongea na mwezangu Waziri wa Maliasili, inaelekea pengine tumefanya uhakiki mara nyingi sana, wahifadhi zetu tunapofanya uhakiki maana yake ni kwamba kila hifadhi imesajiliwa kwa GN namba na mipaka inajulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine uhakiki tuliokuwa tunaufanya ulikuwa haushirikishi wananchi, kwa hiyo wapo wananchi ambao hawajui hiyo GN iliyoandikwa kwenye karatasi inatafsirika vipi kwenye ardhi. Kwa hiyo tumekubaliana, pamoja na kwamba tumeshafanya mara nyingi sana tutakuja kufanya uhakiki mpya. Tunayo maandishi hakuna mtu ambaye anania mbaya kwamba ataongezaongeza mipaka nje ya ile mipaka ambayo imetafsiriwa na imeandikwa na imeruhusiwa na GN.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunazo GN tutakuja na mimi ndio custodian ambaye ni kama msuluhishi wa mambo haya, nitaunda timu za wataalam wangu ambao wako chini ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, nitatumia GN za Maliasili, tutashirikiana na watu wa Maliasili, maana wenzangu ndio wana bajeti, tutafanya mara moja, tutakuja kuhakiki kwa mujibu wa GN na tutakapofanya, tutakapofika Uyui, Mbunge wa Uyui tutamwita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndio GN na hii ndio mipaka uthibitishe, leo kuna vifaa ambavyo ukipima hivi kinaweza kikakupa mwelekeo hata kilometa 25 hatutachukuwa muda, tutaunda timu nyingi. Kwa hiyo nataka tu niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge, mengi wamezungumza, inaelekea kwamba wananchi hawajui exactly na wala hawajawahi kushirikishwa kujua mpaka wa hifadhi hii umeanzia wapi na umeishia wapi. Hilo tunataka tulifanya safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si lazima tufanye kwa hifadhi zote, ningeomba kwa sababu tupo hapa, kila mmoja anayefikiri ana hifadhi ambayo ina mgogoro mkubwa wananchi wanataka kujua mipaka yao imeingia vipi, wakati wa kufanya uhakiki wale vijana wetu wana macho wataona na yaliyopo. Naomba kila mmoja wetu aandike hiyo hifadhi anayofikiri ihakikiwe ampe Waziri. Tukiwa hapa Bungeni maana hatuwezi kufanya zote hata ambazo hazina matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge yeyote anayefikiri wananchi wanamghasighasi sana kujua mipaka imeishia wapi tupeni hiyo hifadhi iko wapi na inaitwa nini, msitu gani hifadhi ya wanyama ipi hata kama ni national park mpeni Waziri sisi tukishapa hiyo orodha tutaunda timu, zitaanza kazi mara moja ya kufanya huo uhakiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilitaka nisimame hapa kutoa ufafanuzi wa haya ambayo yamezungumzwa sana. Ni kweli wamesema tunafanya kazi pamoja Wizara ya Ardhi, ni kweli Serikali ni moja na haya ninayoyasema tumeshazungumza na Waziri wa sekta na yupo tayari, mnamwona alivyokuwa mpole Waziri huyu, msikivu, hana shida na Naibu wake ndio yule, hana shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutayafanya haya mambo waliyoyaomba Waheshimiwa Wabunge. Tukifika tutawashirikisha Viongozi wa Mikoa wa Wilaya na wale vijiji wanaohusika lakini kama Mbunge aliyeleta ile orodha tutamshikisha na ataweza kutusaidia pengine tusihakiki maeneo yote, tukaenda kwenye kona ambayo anafikiri ina mgogoro zaidi katika pori au katika hifadhi inayohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nichangie hayo ili niwaondolee wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, tumewasikia, maneno yamesikika sana na kila leo yamekuwa yanarudiwarudiwa sana kana kwamba waliofanya uhakiki walifanya usiku au kuna watu wanaendelea kupanua hifadhi mpaka leo. Tutakuja kuhakiki kwa mujibu wa GN ambazo zimetangaza hifadhi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)