Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro; Naibu Waziri, Mheshimiwa Mary F. Masanja na wataalamu wa Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye Sekta ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye suala la Half Mile na umuhimu wa kufungua njia mpya za kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia maeneo ya kata za mpakani za Uru na Old Moshi; na uwepo wa mti mrefu kuliko yote Afrika katika Kijiji cha Tema Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini. Huu ni mti wenye miaka mingi zaidi duniani. Una miaka 600. Pia nitachangia kuhusiana na ongezeko la watu na wanyama wa kufuga linavyotishia hifadhi ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Half Mile ni eneo lenye upana wa kati ya 0.5 -0.8 ya mile. Eneo hili lilikuwa linatenganisha Mlima Kilimanjaro na makazi ya watu. Eneo hili kwa upande wa Majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo linajumuisha vijiji 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia inaeleza kwamba watu walianzisha makazi katika maeneo ya Mlima Kilimanjaro takribani zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Pamoja na wachaga kuwepo kwenye makazi yao miaka niliyotaja hapo juu, Mkoa wa Kilimanjaro una historia ngumu inayohusisha uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro na umiliki wa rasilimali ya ardhi ambavyo walivirithi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1921, wakoloni walipitisha Sheria ya Kuhifadhi Viumbe wa Porini (Wildlife Conservation) ambapo misitu ya Kilimanjaro ilihusika. Sheria hii iliwanyima haki wenyeji wa Kilimanjaro wasiingie msituni. Aliyeingia alionekana mharibifu na mhalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1922, Sera za Ukoloni zilimpa nguvu Gavana kuwa mmiliki wa ardhi yote. Mwaka wa 1923 wakoloni walianzisha programu ya kuwanyang’anya wananchi kwenye ardhi yao yenye rutuba na kuanzisha mashamba ya Masetla ya Wazungu. Mashamba haya yalitaifishwa kwa Azimia la Arusha la Mwaka 1967, na bado hayako mkononi mwa wananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, Wakoloni walitumia sheria kandamizi kujimilikisha ardhi ya wana Kilimanjaro na rasilimali za msitu wa Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria ya Wildlife Conservation ya 1921 na ile ya kuwanyang’anya mashamba ya 1923, wakoloni waliingiwa na huruma na kuanzisha Sheria ya Half Mile Strip mwaka wa 1941 kwa lengo la kuwapatia majirani wa Msitu Kilimanjaro huduma za mazao ya misitu kama vile dawa za asili (ngesi), mboga za majani (mnafu) miti ya kujenga nyumba, kuni na majani ya ngombe. Kiuhalisia, eneo hili liko kwenye Forest Reserve na siyo kwenye National Park.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na malengo ya kuanzishwa kwa eneo la Half Mile, tokea enzi za ukoloni, kazi za kibinaadamu zilisababisha uharibifu wa mazingira katika Half Mile na yale maeneo ya hifadhi kwa kukata miti, kupasua mbao, kuchoma misitu, kuchunga mifugo na kuendesha shughuli za kilimo ndani ya hifadhi. Hii ilitokana na kukosekana kwa usimamizi mahiri kutoka katika mamlaka husika Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uharibifu huu, Serikali ilisimamisha vijiji vyote 40 kutokutumia Half Mile Strip tokea 2004, kwa sheria iliyoanza kutumika 2005. Hii ilitokana kusainiwa kwa sheria ya kuziingiza Half Mile Strip za maeneo ya Moshi Vijijini na Rombo iliyotiwa sahihi na Marehemu Rais Mkapa 18/7/2005 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 16/9/2005.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya zuio hili, Serikali yetu iliondoa ile huruma ya Wakoloni kwa Wana Kilimanjaro ya kutumia ile Buffer Zone ya Half Mile. Siku hizi hakuna cha Half Mile tena na ukikamatwa na maaskari wa KINAPA utakuwa na bahati mbaya sana. Wapiga kura wangu wameniambia kuwa wengi wamepigwa na wameambulia vilema, wamebakwa, na wengi wamedhalilishwa kwa namna mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kunyima watu matumizi ya Half Mile, hii imesababisha umasikini mkubwa, ikiwa ni pamoja na wanyama waharibifu (needed; kama, nyani, Tembo) kuingia kwenye mashamba ya wanakijiji na kuharibu mazao. Kabla ya mwaka 2005, shughuli za wananchi kwenye Half Mile zilizuia wanyama kuingia vijiji vya mpakani na ilikuwa hakuna uharibifu wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Makamu wa Rais Dkt. Ali Mohammed Shein alipotembelea Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2008 akiambatana na Waziri wa Maliasili Mheshimiwa Prof. Jumanne Maghembe wananchi walimweleza matatizo yaliyojitokeza baada ya Serikali kuunganisha eneo la hifadhi la KINAPA na misitu ya hifadhi za asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ziara hiyo, Wizara ilikaa na kuiagiza TANAPA (kwa barua Kumb Na. CAB. 315/ 484/01/A ya tarehe 22/1/2008 ya Waziri, Mheshimiwa Prof. Maghembe kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, na barua kumb na CJA.246/374/01/42 ya tarehe 27/2/2009 ya Katibu Mkuu Dkt. Ladislaus Komba kwenda kwa Mkurugenzi wa TANAPA) wachore ramani upya na kutenga eneo la nusu mile liwe nje ya Hifadhi ya KINAPA kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelekezo hayo hapo juu na kukumbushwa mara kwa mara na wadau wa maendeleo wa mlima Kilimanjaro, hadi leo ramani hiyo haijatoka na sheria hii kandamizi kwa wananchi wa vijiji 40 vya mpaka na mlima Kilimanjaro bado inawanyanyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria kandamizi kama hii siyo nzuri na zinasababisha migogoro isiyo ya lazima baina ya wananchi na Serikali yao. Kama mwakilishi wa wananchi, hata mimi naikataa kabisa sheria kandamizi kwa wapiga kura wangu. Namwomba Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan aliangalie jambo hili kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wetu ambaye ni msikivu sana afuatilie pale wenzake walipoachia ili haki itendeke. Wana Moshi Vijijini, Vunjo na Rombo tunaomba maeneo yote ya vijiji vya mpakani vipewe fursa ya kuulinda na kuutunza mlima wao kama ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ikibadilishwa, Half Mile Strip inaweza kutumika kwa mafanikio makubwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu, Serikali ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji na kusaidia wananchi wa vijiji husika:-

(a) Kuutunza mlima;

(b) Kuwapatia wananchi huduma;

(c) Kuinua uchumi wa wananchi, Wilaya, Mkoa na Taifa; na

(d) Kukuza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ikibadilishwa, tunatarajia kupanda miti ya muda mfupi kama Cyprus, Pine, Mikaratusi na aina nyinginezo zinazokua haraka kwa ajili ya nguzo za umeme, nguzo za ujenzi wa nyumba zikiwemo ghorofa. Miradi kama hii iko Iringa. Rais akiruhusu hili, nchi nzima itanufaika kwani Kilimanjaro ina miundombinu bora ya kusafirisha hizi bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni ule wa kuiomba Wizara ifanye utafiti na kufungua njia mpya za kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia kata za mpakani huko Uru na Old Moshi. Njia hizi zinaweza kuwa fupi, na baadhi ya watalii wanaweza kuzifurahia sana. Kwa kufanya hivyo, tutaongeza uwekezaji kwenye maeneo haya, ajira na mzunguko wa pesa utaboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu ni kuhusu mti mrefu Afrika. Wagunduzi kutoka Chuo Kikuu cha Beyreuth Ujerumani wakiongozwa na Dkt. Andrew Hemp wamegundua kwamba mti mrefu (81.5m) kuliko yote Afrika uko katika Kijiji cha Tema, Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini. Mti huo unaitwa Entandrophragma Excelsum (Mkusu). Inasemekana kuwa mti huo ndiyo ulio na miaka mingi zaidi duniani (600 years).

Mheshimiwa Mwenyekiti, watafiti wa Kijerumani wameshauri kuwa mti huo unaweza kuishi zaidi kama utatunzwa na kuhifadhiwa vizuri. Ninaiomba Serikali iboreshe uhifadhi wa mti huu na kuboresha miundombinu ya barabara kuufikia, kwani hiki ni kivutio kipya cha utalii ndani na nje ya Tanzania. Barabara ya kwenda eneo hili ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa nne ni kuhusu hatari inayoikabili Hifadhi ya Ngorongoro. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilianza mwaka 1959 likiwa na wakazi 8,000. Ripoti inaonyesha kwamba sasa hivi kuna wakazi zaidi ya 100,000 na ongezeko kubwa la mifugo kama ngombe, mbuzi na kondoo katika eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli za uhifadhi kule Ngorongoro zimekuwa ngumu kutokana na migogoro baina ya binadamu wanaoishi eneo la hifadhi na wanyamapori. Wanyamapori huvamia maboma ya wafugaji na kula wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo. Vilevile kuna baadhi ya wananchi wanaolima katika eneo la hifadhi. Hii imesababisha eneo hili kushambuliwa na magugu vamizi na kuishia kupunguza eneo la malisho kwa wanyamapori na wale wa kufugwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha mifugo kimeongezeka sana na hii imesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya kuambukiza toka kwenye wanyama wanaofugwa kwenda kwa wanyamapori na kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa wanaofugwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatua stahiki hazitachukuliwa mapema, hali itakuwa tete sana miaka michache ijayo. Naishauri Serikali ichukue hatua stahiki kwa kuirekebisha Sheria ya Kuanzisha Hifadhi ya Ngorongoro. Maboresho ya sheria yalenge kulinda wanyamapori, kwani Ngorongoro ni mahsusi kwa wanyamapori. Wakazi na wanyama wa kufugwa waondolewe eneo la hifadhi na wapelekwe kwenye maeneo yao ambayo yako ya kutosha nje ya eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.