Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara muhimu ya Maliasili na Utalii. Kimsingi nikiangalia michango ya Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kwamba, wote tunakiri kuna kazi kubwa sana ambayo imefanywa na Wizara hii katika ku-transform sekta ya utalii kwa maana ya kuongeza idadi ya watalii, lakini pia kuongeza pato la Taifa, lakini bado kuna kutokuridhishwa kwa Wabunge wengi kwa jinsi hali inavyoenenda katika sekta ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia michango ya Waheshimiwa Wabunge unaweza kuona kwamba, wengi wanaona kwamba, sekta hii haijatendewa haki kwa maana kwamba, kuna fursa nyingi za utalii ambazo bado hazijaguswa. Tumejikita sana kwenye utalii wa wanyamapori, lakini kuna talii za fukwe kuanzia Tanga mpaka Mtwara ambazo hazitumiki kikamilifu, tuna talii za kwenye visiwa ambazo hazitumiki kikamilifu, lakini tuna talii za kiutamaduni ambazo hazitumiki kikamilifu. Kwa hiyo, sekta hii ya utalii ikigusa maeneo yote haya naamini kabisa tunaweza kupata tija ambayo tunaitarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunaona kwamba, pato ambalo linatokana na utalii kama tunaenda ku-adapt sera ya ugatuaji wa madaraka ya D-by-D, kama tunaenda kushirikisha wafanyabiashara wadogo katika sekta ya utalii, tunaweza kwenda kuona makubwa katika sekta hii. Tatizo la sekta yetu ya utalii imehodhiwa na wafanyabiashara wachache wakubwa na hawa ndio ambao wana-drive hii sekta kwa kuweka masharti magumu ambayo wafanyabiashara wadogo katika sekta ya utalii kushindwa kuingia na kufanya biashara. Matokeo yake vijana wachache ambao tunawaelimisha kwa gharama kubwa katika sekta ya utalii wanaishia kuwa watumishi na vibarua katika sekta ya utalii na sio kama wajasiriamali katika sekta hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba kupitia Bunge lako wananchi wetu, hasa vijana wetu ambao wamesomea utalii wawekewe mazingira wezeshi ya kuingia katika sekta ya utalii kama wajasiriamali na sio kama vibarua. Ninachokiona kuna cha kujifunza kwa wenzetu, hasa nchi za Asia, kule wenzetu utalii mwingi uko katika ngazi ya familia katika ngazi ya vijiji. Huwezi kukuta mahoteli makubwa makubwa katika maeneo mengi ya vivutio, utakuta kuna bed and breakfast, utakuta kuna vi-lodge, kuna vihoteli ambavyo vinaitwa boutique kule Myanmar, Laos, Thailand hata Cambodia. Unaona kabisa jinsi gani utalii ulivyoenda kuajiri watu wengi kwa mpigo ukilinganisha na kwetu ambapo tunategemea wawekezaji wachache kuajiri vijana wengi kama vibarua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanahitaji fedha. Kitendo cha kuondoa fedha za Mfuko wa Utalii kupeleka katika Mfuko Mkuu wa Hazina, kwa kweli kwa namna mona ama nyingine imeuwa sekta ya utalii. Naomba Serikali ilitafakari tena upya kwa sababu, tuna maoni mengi ambayo tunataka Wizara hii isimamie mabadiliko katika sekta ya utalii, lakini swali, fedha wanapata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha inabidi waombe kama wengine wanavyoomba kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Hali hii haitatupelekea sababisha kuona mabadiliko yale ambayo tunayatarajia katika sekta hii ya utalii. Ombi langu, ni Serikali kuona jinsi gani inarejesha Mfuko huu wa Utalii na ili Wizara isimamie mapato haya kwa ajili ya kuwekeza kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika ku-transform utalii wetu, lakini pia katika ujenzi wa miundombinu katika mbuga zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano katika mbuga zetu ni suala la muhimu. Mtalii anayeingia Mikumi anaweza akaingia toka asubuhi mpaka jioni asitume status kwenye WhatsApp kwa sababu hakuna simu, lakini pia hata akitaka kutoka pale Mikumi kwenda Ruaha atapita pale Ng’apa, atapita Msimba, atapita Ruaha hana mawasiliano hata ya simu. Halafu tunataka mtalii huyu aende akatangaze utalii kwao? Hakuna utalii mzuri kama watu kushuhudia nini ambacho kinaendelea katika mbuga za wanyama, lakini kama hawawezi wakajirusha wenyewe kwenye status kuonesha kwamba, nini wanachokiona katika mbuga zetu, si rahisi kushawishi wengine kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nchi yetu kama ilivyo katika nchi nyingine, kasheshe la corona liliathiri sekta yetu ya utalii, lakini ilifungua fursa ya watalii kutoka nchibya Urusi ambao walikuja kutokea Zanzibar. Sasa naomba Serikali iione hii kama fursa kwa nchi za Baltic na Russia kama sehemu ya kuhamasisha utalii wa kuja moja kwa moja kutokea Zanzibar kuja Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)