Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti yao. Nianze kwa kuwaomba sana Wizara waanze kuyafanyia kazi mambo ambayo yalifanyiwa mjadala kati yao na Washika Dau kwa maana ya Wafanyabiashara wa Utalii, lakini na mawasilisho ya Vyama vya Wafanyakazi wanaojihusisha kwenye biashara hii ya utalii kama ma-guide, ma-porter na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na maslahi ya wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye utalii, ma-porter, ma-guide na wapishi. Kundi hili ni kundi kubwa la vijana lililojiajiri kwenye kazi ngumu hii ya utalii, lakini hawana mikataba wengi wao, lakini pia hawana bima za afya, wanakwenda kule kwenye baridi sana. Ningeiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuandaa hata mfumo wa kuwa na pensheni kwa watu ambao hawako kwenye sekta rasmi, lakini wanaopata kipato kama hawa ambao wanajihusisha na biashara ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia hao watu wanahitaji elimu kubwa, kwa nature ya biashara ya utalii, mfanyabiashara yule akishawapokea wageni huwa mara nyingi wanakabidhiwa kwa hawa waongoza utalii. Sio wote wana utashi wa kutosha, naomba sana Wizara iangalie uwezekano wa kuwapa elimu ya mara kwa mara na semina za mara kwa mara hasa kuhusu mambo muhimu ya nchi yetu ikiwa na takwimu, kwa sababu hawa ni mabalozi muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu sana kuhusiana na ada zetu kwenye mbuga zetu na maeneo yetu ya utalii pamoja na viwanja vyetu vya ndege. Kama kichocheo muhimu cha utalii naomba Wizara ifanye utafiti wa kutosha kulinganisha bei hizi pamoja na maeneo mengine ili kuweza kufanya maamuzi sahihi. Kama ilivyo kwenye halmashauri zilizopo kule Geita zinapata CSR kutoka kwenye machimbo yale, katika Mkoa wa Kilimanjaro halmashauri zinazozunguka kwa mfano Mlima Kilimanjaro, tungependa sana na sisi tuwe tunapata kipato fulani kwa ajili ya kusaidia halmashauri zile ambazo zinazunguka mlima ule na ambazo zinafanya kazi kubwa ya kulinda mazingira maeneo yale. Nimeona wenzetu wa Geita wanapata kipato kizuri sana, lakini kwetu naona suala hilo halipo. Tunaomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba suala hili liliwasilishwa na wafanyabiashara suala la sera hasa kwenye suala la kodi, naomba Serikali ifanyie kazi hasa kwenye eneo la kukata rufaa hasa wafanyabiashara wanapokuwa wana matatizo kwenye kodi. Katika sheria ile kuna kifungu cha 16 ambacho kinapingana kabisa ambacho kinasema ukikata rufaa kwa Kamishna lazima iwe suala linalohusu Civil Concern. Sasa kipengele hiki kinapingana kabisa na kipengere kifungu cha 7 na kifungu cha 53 ambacho kinatoa haki ya rufaa. Wafanyabiashara waliwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri, naomba nilitilie msisitizo ili basi marekebisho yaweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii imepigwa sana kipindi hiki cha Corona, lakini imetupa mafunzo mawili. Funzo la kwanza ni kuweza kuweka record zetu sawa ili baadaye tuweze kutoa stimulus ikiwezekana na stimulus siyo lazima iwe kwa kutoa fedha hata kwa kuwapunguzia gharama kwa kipindi ambacho kitakuja cha utalii. Hata kuhuisha leseni zao kwa sababu walikata leseni kipindi ambacho hawakufanya biashara. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana hilo liweze kuzingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuangalia masoko mapya, kipindi cha Corona tumeweza kupata soko jipya la Urusi, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa ni lugha, wenzangu wameshataja. Ni vizuri tuanze kuchunguza masoko mapya na tuhakikishe tunafanya kazi ya kujua lugha hizo za Kichina, Kirusi na za maeneo mengine ili tuweze kupata masoko hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la helicopter ya Uokozi, Rescue helicopter. Pale Kilimanjaro ilikuwa inafanyika na mfanyabiashara binafsi. Ilikuwa ina tija sana na ni chanzo cha mapato, lakini kutokana na hali hii ya COVID yule bwana ameshindwa kujiendesha. Ni vizuri Wizara iangalie chanzo hiki cha mapato, iweze kununua helicopter ya uokozi ambayo itakuwa inalipiwa kwa wale ambao wanakwenda kupanda mlima ili mtu akipata tatizo basi huduma ile ambayo imeshazoeleka, imeshatangazwa iweze kuwepo na ni chanzo cha mapato kwa ndugu zetu wa Wizara ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi kabisa naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.