Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muda huu ili niweze kuchangia hoja hii muhimu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, niungane na wenzangu kupongeza kazi nzuri inayofanyika na Wizara hii, Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wake pamoja na Kamati kwa ujumla, bajeti iliyoletwa na mapendekezo yote ni mazuri kabisa, nawaponga sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu, jambo la kwanza, napenda nikumbushe nililizungumza hili wakati nilipochangia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Ile Mbuga ya Udzungwa asilimia 80 ipo Wilaya ya Kilolo na hilo Wizara inalifahamu. Jambo la kwanza, hakuna geti hata moja la kuingia Mbuga ya Udzungwa kwa Wilaya ya Kilolo ambako ndiko asilimia 80 ilipo. Zile ofisi za TANAPA zilizopo pale Udekwa, barabara yake haijajengwa na nilisema hapa kwamba, walianzia kule Udekwa kuja pale Mahenge kwenye barabara ya lami. Wakatengeneza kilomita 14 kwenda barabarani ikaishia porini bado kilomita saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba, Wizara hii na TANAPA kwa sababu, ofisi zao ziko pale Udekwa hatuwezi kushindwa kutengeneza zile kilomita saba ili tuingie kwenye zile ofisi zao na pia ili tuweze kulifikia lile geti, kwa sababu, kwa sasa tunazunguka karibu kilomita 60 mahali ambapo tungetumia kilomita 20 kufika pale kwenye lile geti na ile barabara ya kilomita 60 yenyewe si nzuri. Kwa hiyo, napendekeza kwamba, kwa pamoja mimi niko tayari kushirikiana hata na wananchi, tutoboe ile barabara na yenyewe tutafute fedha kidogo tuweke greda tumwage kokoto, hatusemi lami lakini ifike kwenye lile geti, angalau tuwe na geti moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, Mbuga ya Udzungwa hiyo inayotumika ni asilimia 20 tu kwa sababu, kule kote kumebaki pori, asilimia 80 ya mbuga haitumiki, jambo ambalo ningependa tushirikiane ili tufungue na kama kuna haja ya kuongeza mageti mengine tuongeze, kwasababu, ile ni Mbuga kubwa na ina maeneo mengi, ambayo yangeweza kuwa na vivutio.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwa unyenyekevu sana, naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wanisikilize kwa sababu hii ni changamoto ya kipekee. Katika Kata ya Kidabaga, Kata ya Masisiwe na kidogo Kata ya Ng’ang’ange kuna changamoto ya ngedere na wale ngedere wanatoka kwenye ule mpaka na ni wengi. Wale ngedere wanavuna mahindi kama ya kwao na kuna usemi usemao ukicheka na ngedere au nyani utavuna mabua, wale watu kule sasa hivi wanashinda kule porini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilienda kwenye mikutano, watu wanafanya zamu, natakiwa niwe na mikutano miwili wa asubuhi ili wengine wahamie ngedere na wa mchana ili wengine waende warudi. Wale ngedere sio kivutio kwa sababu, kuna baadhi ya wawekezaji kule wanatoka hata Ulaya, lakini nao wanalalamika. Ngedere wale wanakula wakimaliza wanakaa hata kwenye shule za msingi na wanafanya burudani zao nyingine siwezi kusema hapa. (Makofi/Kicheko)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kitolewe kibali wavunwe. Kama kuna mahali wanaliwa wakavunwe waliwe, kwa sababu, ni wengi na wanazaliana sana. Ni changamoto kubwa sana na ningependa itatuliwe.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nyamoga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, ifike wakati sasa watu wa Maliasili waangalie, kama wenzetu hapa wachina hivi vitu vyote wanakula? Kwa nini bucha za ngedere, nyani na vitu vingine zisiwepo? Ili hao watu waje wanunue hizo nyama wapeleke huko? (Makofi)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuzungumzia suala la tembo pale Kata ya Nyanzwa pamoja na Kata ya Ruaha Mbuyuni. Kwa sasa kwa mwaka huu tu wamekufa watu 12, Kata ya Nyanzwa nane na Ruaha Mbuyuni wawili, tayari wameshauawa. Huenda nao ni ushoroba, lakini kwa kweli ni changamoto kubwa na naomba Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri wakimaliza hapa, twende pale, wameweka askari pale wanalima vitunguu tu. Tena wakati tembo akiua mtu, wanataka wananchi wachange fedha. Sasa tembo ameshaua watu wakae vikao, wachange fedha wakakodi gari ndipo wakawachukue, ndipo waende wakawaue au wakawafukuze hao Tembo.

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, inachukua muda mrefu sana nawaombeni sana haya.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba Wizara wayafanyie kazi hayo. Hata hivyo, naunga mkono hoja, ikiwa hayo niliyosema yatazingatiwa. Ahsante sana.