Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia hii nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika sekta hii ya Maliasili na Utalii. Jambo la kwanza, nawapongeza sana viongozi wa Wizara kuanzia kwa Waziri, Naibu Waziri, Watendaji wote na Wahifadhi wote wamefanya kazi nzuri sana, pamoja na changamoto ambazo zinawakabili kutokana na ugonjwa huu wa COVID 19. Hongera sana kwa kazi ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kabisa kwamba, sekta ya utalii ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, sisi sote tunajua hilo, mchango wake kwenye pato la Taifa, kwenye ajira na kwenye fedha za kigeni ni kitu muhimu sana. Hata hivyo, wengi wanasema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, lakini nafikiri kwa sasa hivi ni nchi ya nane, sio ya pili tumeshaharibu, tumeshavuruga vuruga kwa hiyo, sasa hivi Tanzania sio ya pili tena bali ni nchi ya nane.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili nchi iweze kunufaika na vivutio vya utalii vilivyopo, lazima tuchukue mikakati ya makusudi ya kuhakikisha kwamba, tunaiendeleza hii sekta ya utalii. Sasa ili kufanya hayo nitapendekeza mambo machache, lakini kwa sababu ya muda sitaweza kuyasema yote. Nataka kusema kwamba, nchi yetu ina bahati ni nchi yenye Mlima mrefu kuliko milima yote katika Afrika. Ni nchi ambayo mwanadamu wa kwanza wa kale alipatikana Tanzania. Ni nchi yenye Maziwa, ni nchi yenye bahari, yenye milima, yenye kila kitu, lakini tatizo tulilonalo hatujaweka mikakati ya kutosha ya namna ya kutumia huu utajiri ambao Mungu ametupatia. Kwa hiyo, tufike mahali tuweke mikakati ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sasa hivi nchi kumi zinazoongoza kwa utalii duniani Tanzania hatumo. Inaanza Ufaransa ambayo ina watalii milioni 89, kuna Spain milioni 82, USA milioni 79, China milioni 62, Italy milioni 61, Turkey milioni 45, Mexico milioni 41, German milioni 38, Thailand milioni 38, UK milioni 36, Tanzania hatumo wala Afrika hatumo, pamoja na utajiri wote huu tulionao. Hivyo, ni lazima tukae chini tujiulize kwa nini sisi tunakosa kuweka mikakati ya makusudi na kuweka uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo lazima tuhakikishe tunalifanya, ni kutengeneza miundombinu thabiti ya kuvutia utalii nchini. Hii Serikali wameanza kufanya vizuri, lakini hapo katikati tumeshajichanganya. Tumeamua kuchukua mapato ya utalii yale tumeyapeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Sasa tunaziacha Taasisi za Uhifadhi hazina fedha za kujenga miundombinu, halafu tunataka kujenga utalii, nani atatangaza utalii? Tutauendelezaje katika utaratibu wa namna hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kuna haja ya kukaa chini na kulitafakari, ili tuone haya Mashirika ya Hifadhi sasa yawe na mapato yake, yawekeze, yajenge miundombinu, watu waende mahali sehemu mbalimbali, wakale maisha, hapo ndio tutaijenga nchi yetu, bila kufanya hivyo hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mbozi kuna Kimondo cha aina yake, ni moja ya vimondo nane duniani, kiko pale Mbozi. Naishukuru Serikali imewekeza pale, lakini bado hatujakitangaza vya kutosha. Tunayo maji moto kule Mbozi, hatujatangaza vya kutosha. Sasa na maeneo mengine yote ya mali kale ambayo hatujayatangaza lazima tuwe na mkakati wa namna ya kutangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini tunatakiwa kufanya katika kutangaza? Tunayo TBC, Channel Two ambayo tuliweka mahususi kwa ajili ya kutangaza, lakini je. hiyo ndiyo itawafikia watalii wote tunaowahitaji? Lazima tutafute namna ya kutangaza utalii, tutumie mbinu gani, tuwekeze, bila kuwekeza hatuwezi kupata vitu. Hatuwezi kupata fedha, lazima tuwekeze kwenye matangazo ya kutosha ili kuweza kuvutia utalii. Hapa Dodoma kwa mfano, Bunge tumekaa miezi minne niambieni ni sehemu gani ambapo sisi tumeenda kula maisha, wapi? Sijapaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatujawekeza vya kutosha, kwa hiyo, lazima tuweke mkakati kuwekeza ili kusudi watu wahakikishe kwamba wanaenda kula maisha. Naomba kwa sababu, Kamati imependekeza, tuanzishe Mamlaka ya Kuendeleza Utalii. Naunga mkono hii mamlaka ni muhimu sana, ikafanye hii kazi, ikalitangaze Taifa letu, ikatangaze vivutio vyetu, tuweze kuleta maendeleo, tuweze kupata fedha nyingi, tuweze kutengeneza ajira mbalimbali kwa Watanzania, hii itakuwa ni kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imependekeza tuanzishe Mamlaka ya Misitu Tanzania badala ya kuwa Wakala. Naunga mkono, lakini nitaunga mkono tu wakimaliza tatizo lililopo Mkoa wa Songwe la matumizi ya mkaa. Walizuia wananchi kwamba, wasitumie mkaa, wasivune mkaa, lakini tunajua kabisa matumizi ya mkaa yapo, lazima yawekewe utaratibu mzuri na wananchi wa Songwe wapate sehemu hiyo, hiyo itawasaidia sana. Kwa hiyo, nitaunga mkono kama haya mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema bahati mbaya naona muda haukuwa upande wangu, lakini niwahamasishe Watanzania twende tukale maisha, ndipo tutajenga uchumi imara. Tafuta fedha, katumie, utapata maendeleo, Mungu awabariki, ahsante sana. (Makofi)