Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza kabisa na mimi nitumie fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri wanazofanya. Kwa kweli mnyonge mnyongeni haki yake mpeni; wanafanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa harakaharaka; kwanza katika Mkoa wangu wa Simiyu. Mkoa wangu unaitwa jina la Simiyu, maana yake ni mto. Kuna Mto unaitwa Simiyu, hauna maana yoyote. Ni mto ambao mvua zikinyesha unapata maji, mvua zikikatika kwa muda mchache mto unakauka. Hauingizi shughuli yoyote ya kiuchumi, hauna chochote kiutalii, hauna tija yoyote. Isipokuwa tu tuliita Simiyu, ilikuwa ni vita vya makao makuu ya mkoa, yatakuwa Maswa na wapi, kuna wenzetu wakaamua kubadilisha jina badala ya kuuita Mkoa wa Maswa ukawa Mkoa wa Simiyu ili kuchengesha tu Makao Makuu ya Mkoa. Sasa vita hivyo vimeisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Game Reserve inaitwa Maswa Game Reserve; kwa nini Mkoa huu usiitwe Mkoa wa Maswa tuka-promote hiyo game reserve, tukai-market, tukau-market mkoa wetu. Najua sikuwepo wakati wa michakato hii, sikuwa Mbunge na nadhani ningekuwa Mbunge pangechimbika. Hata kama makao makuu yangekwenda sehemu nyingine, lakini mkoa ule ungeitwa Mkoa wa Maswa tuka-promote Game Reserve ya Maswa kuliko mto ambao unakausha maji na usiyokuwa na maana yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ruvuma wame-promote mto wao, una maana na historia. Kilimanjaro kuna Mlima Kilimanjaro; Manyara wana Mbuga ya Manyara; Katavi kuna Mbuga ya Katavi; hata huko Chato mnataka leo tuweke Mkoa wa Chato, uitwe Burigi. Ni hilo tu nimesema nianze nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la ng’ombe kwenda kwenye hifadhi. Control ya ng’ombe kwenda kwenye hifadhi, wewe ni shahidi, inahitaji brain ya mtu mmoja tu. Just the brain of one person; anaswaga ng’ombe hata 5,000 wanakwenda sehemu fulani. Kwa hiyo decision ya ng’ombe kwenda kwenye hifadhi ni ya binadamu, tena mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali tunapo-charge kila ng’ombe, yaani adhabu inakwenda kwa ng’ombe mmojammoja, hiyo hapana. Hebu turudi tujipange upya tufikirie adhabu. Hivi kwani adhabu ya mtu ambaye anaendesha gari ndogo aka-overspeed na anayeendesha gari kubwa adhabu yake ni tofauti? Au kusema unaendesha basi, basi wewe kwa sababu umebeba watu wengi ukivunja sheria ina maana adhabu yake inakuwa ni tofauti na gari ndogo? Adhabu ni adhabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anapoingiza ng’ombe wengi kwa sababu discretion ni ya mtu mmoja, basi adhabu iangaliwe, kama alivyozungumza Mbunge wa Kiteto hapo, aadhibiwe aliyewapeleka ng’ombe, lakini siyo ku-charge gharama ya ng’ombe mmoja mmoja. Huo kwa kweli ni uonevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nimesikia na wewe umekuwa balozi wa kutetea mjusi. Huyu mjusi ambaye yuko Ujerumani ambaye ni dinosaur, juhudi hizo…

NAIBU SPIKA: Nani huyo kanitunukia ubalozi? Maana sina taarifa.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa mama Riziki Lulida amekunukia.

NAIBU SPIKA: Ahaa, amenitunikia? Nilikuwa sina habari.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, amekutunikia, u-champion wa kutetea yule mjusi arudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niseme hivi; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sisi ni wajumbe au tuseme ni member wa Umoja wa Mataifa. Sisi ni member state, tuko katika mikataba ya Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, UNESCO inasimamia masuala yote ya elimu pamoja na haya masuala ya maliasili. Mwaka 1970 tuliingia mkataba ambao unajulikana kwa jina la Convention on the Means of Prohibiting and Preventing the Illicit Import, Export and Transfer of Ownership of Cultural Property. Huu mkataba tuliuingia Paris tarehe 14, Novemba mwaka 1970 na nia ni kulinda maliasili za nchi hizi wanachama.

Mheshimiwa Naibu Spika, UNESCO ndio anayesimamia masuala yote ya ulinzi wa hizi mali za urithi katika nchi husika. Sisi tumeanza juhudi za kufuatilia mjusi huyu toka mwaka 2005. Cha kushangaza Wizara ya Maliasili badala ya kwenda UNESCO kupeleka malalamiko kule kwa sababu UNESCO ina tume yake hapa nchini na tume hiyo ndiyo yenye kazi ya kwenda kupeleka hizi hoja kule UNESCO kuishtaki Serikali ya Ujerumani ili iweze kuturudishia mjusi wetu, lakini badala yake Wizara ya Maliasili inaongea na watu wa museum (makumbusho) ambayo inahifadhi mjusi yule.

Mheshimiwa Naibu Spika, yule anayehifadhi mjusi ni mtu ambaye tunaweza tukasema labda ni mwizi. Haiwezekani wewe unadai kitu chako cha wizi, badala ya kwenda mahakamani kuomba kitu chako unakwenda kwa mwizi kwenda kujadili naye akurudishie hicho kitu. Naomba nikwambie, Kamati za Bunge zitakwenda huko, watakwenda watu wa maliasili watapokelewa vizuri na balozi, watapokelewa vizuri na watu wa museums, watakwenda watamwona mjusi lakini hakuna chochote kitakachofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali, tunaomba Wizara waongee na Tume ya UNESCO waandike barua kwenda kwenye tume ambayo itakwenda kwenye vikao vinavyokubalika kisheria kutokana na mkataba wa mwaka 1970, tudai officially mjusi huyu arudishwe. Atarudishwa kwa gharama ya Serikali ya Ujerumani na atakuja kupangwa na kuwa assembled kwa gharama ya Ujerumani. Naomba hilo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri.

NAIBU SPIKA: Muda wako umeshakwisha Mheshimiwa Nyongo.