Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ASHA ABDULLA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mungu kunipa uwezo leo wa kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kuweza kutoa mchango wangu mdogo kwa Wizara hii. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Ndumbaro na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii pamoja na wahifadhi kwa sababu bila wao hakuna Wizara hii. Wote wamefanya kazi nzuri sana kusaidia kunyanyua kipato katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwanzo nataka nianze kwa ile staili ya kuunganaungana, yaani nioanishe utalii huu unaofanyika bara na wa Zanzibar ili watalii wanapokuja kwa mfano huku, wanaoshukia huku moja kwa moja waambiwe vivutio vilivyokuwepo kule Zanzibar na kwa utaalam maalum ili waweze kwenda na kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, na wale wanaokwenda kule vilevile waambiwe vivutio gani vya ziada vilivyopo huku ili waje. Kwa sababu utalii wa visiwani ni tafauti na utalii wa bara; huku kuna wanyama, kule kuna samaki, fukwe nzuri na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hilo naomba lioanishwe vizuri zaidi kama tulivyoungana kwenye Muungano tukaweza kupata watoto, mpaka Kakonko tuna watoto sisi wengine, kwa hiyo na utalii uje kwa staili hizo hizo. Hilo ndilo langu la mwanzo ninalopenda kulisemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kulizungumzia ni hili la malikale na uhifadhi ambalo lina mchango mkubwa katika kuendeleza sekta hii ya utalii. Ukweli tumeona kuna sehemu hizi ambazo zimeainishwa kama zinahifadhiwa, kwa mfano Kilwa Kivinje, Songo Mnara, Bagamoyo, Kaole na Kolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, huku baadhi kwa mfano kama Kilwa Kivinje mimi mwenyewe nimeona yale majengo yanapotea kabisa. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, Wizara ifanye jitihada ya kufanya ukarabati kwa staili ileile ili haya yasiweze kupotea wala yasiweze kuvamiwa. Hasa haya ya Kilwa Kivinje ambayo nimeweza kuyaona, haya yanapotea, hata madirisha, milango, yote yanachomolewachomolewa. Kwa hiyo Wizara waliangalie jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia sasa hivi ni hili la kusafirisha baadhi ya wanyama. Nafikiri kuwe na control kwa sababu wanyama inaonekana wengi tunasafirisha tembo, chui na wengine, kwa hiyo tuwe na control ili wasije kwisha, halafu hizi tunu zikahamia huko katika nchi nyingine sisi tukawa hatuna kitu. Kwa hiyo, Wizara waongeze control katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano zamani hapo nilikuwa nasikia sana vipepeo, ndege na nini, sasa siku hizi sijasikia, hata vyura walipelekwa kule. Kwa mfano vyura kutoka Kihansi walipelekwa kule, hatusikii tena chochote. Mwisho na sisi wenyewe tutapelekwa tukazae kule huku hakutakuwa tena watoto. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu lingine ninalotaka kulizungumzia ni hili la kuhakikisha kwamba utalii wa ndani unaongezeka kwa kuwashawishi wananchi wetu kufanya hizi ziara za kutembelea vivutio mbalimbali kwa kuwawekea excursion. Kwa mfano, niliwahi kwenda Kigoma nikataka kwenda kutembelea kule kwenye wale masokwemtu, nilishindwa. Bei ya kule ilikuwa ni kali sana. Kwa hivyo angalau kwa Watanzania ambao wana midomo mirefu wale ndiyo wa kuwapeleka, wa kuwapunguzia bei ili wakasemee kwengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine kwa Wizara hii ambayo inafanya kazi vizuri, ni kwamba mshiriki kwenye makongamano ya kimataifa kwa sababu huko ndiko tutakakojiuza zaidi. Ingawaje wanatuambia wamefungua app, wachangiaji wangapi sijui wameonekana ku-click au kufanya nini, hii haitusaidii bwana. Tutoke, tuvae masks zetu, tupige sindano za COVID, twende tukaitangaze Tanzania yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi hawa watu wanavyofanya kazi hii vizuri, na huyu jamaa Waziri anavyokuwa vizuri, sina la kusema zaidi ila apewe hiyo bajeti yake aliyoomba afanye kazi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)