Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana kwa Jimbo letu na kwa Mkoa wetu wa Kilimanjaro. Nawashukuru na nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Katibu Mkuu wake kwa kuwa wenye mwamko chanya katika kushughulika na matatizo yetu kwenye mikoa yetu hasa sisi ambao tunapakana na hifadhi na tunasimamiwa na TFS ambayo imekuwa inanyanyasa sana watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kuzungumza jambo moja hili la nusu mile na natumaini limezungumziwa vizuri sana, nusu mile ni kitu ambacho kwetu kinatuuma kwa sababu kama mnajua kwamba ardhi yetu kule Kilimanjaro ni ndogo, lakini pia ukiwa unapakana na msitu huu unaozunguka Mlima Kilimanjaro unakuta kwamba fursa iliyopo ni kuokota kuni, kukata majani, kuweka mizinga ya nyuki na kadhalika. Mwanzoni tuliruhusiwa kuingia hadi nusu mile hiyo, lakini baadae TFS wakang’ang’ania kuchukua hata eneo hilo, walikuwa wanaturuhusu hata angalau wanawake waingie kukata kuni na kuchukua majini, lakini sasa hawaruhusiwi. Naomba hilo jambo lifikiriwe na nimeshazungumza pamoja na Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu, naamini kwamba litakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nazungumzia kuhusu stimulus package kwa sekta hii muhimu ya utalii. Naamini kwamba wengi wanaelewa jinsi ambavyo watu wameathirika; mahoteli yameathirika, hayajatengeneza fedha, yametengeneza hasara kwa muda mrefu na hawa tour operators pia wametengeneza hasara. Hivyo nafikiria itafaa kujua ni namna gani ya kuweza kuwanusuru kwa kuwapa muda kama wana mikopo, kama wana tozo wanadaiwa kwenye vitalu au kwenye maeneo yao wanayoshughulika nayo, Serikali iweze kuona ni namna gani ya kuwanusuru kwa kuwapa muda mrefu wa kulipa au kuwasamehe kwa maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme pia kwamba kuna tatizo baada ya hilo na kama ikiwezekana naamini linawezekana kama tukilifikiria vyema, tukijua hii ni sekta muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni issue ya tour operators; niliwahi kuzungumza kuhusu tour operators hapa. Tour operators wameunda jumuiya yao kule kwetu Kilimanjaro kupandisha watalii mlimani. Wameunda hii jumuiya ili kui-serve na kui-regulate; waweze kujiwekea discipline na namna gani wanapandisha watu na nidhamu katika kushughulikia watalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa walikuwa wanafikiri kwamba ni vizuri ili waweze kujadiliana vizuri malipo yao na tour operators waweze kupata au waweze kupewa fursa ya kujadiliana na wawekezaji wa tour operators na pia kujichagua wenyewe nani anapandisha huyu kwa vile anajua Kiswahili, Kifaransa na kadhalika. Kwa hiyo tunaomba kwamba tour operators wapewe mwongozo huo wa kutumia jumuiya hiyo ili waweze kupandisha watu/watalii mlimani wakiwa wamekaa vizuri na mtalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, watalii hawarudi kwa sababu hawawi-treated properly, lakini wakitumia jumuiya hiyo ambayo ni wataalam watawaweza wakawa-treat na wale ambao wanafanya mambo ambayo siyo ya kinidhamu, wakashughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni suala zima la utalii wa vivutio vya kiasilia. Watu wanasema kwamba kivutio cha kiasilia hapa Tanzania ni Mmasai tu, kumbe kuna vivutio vingi, kuna mahandaki, kule kwetu Mamba, Komakundi kuna mahandaki ambayo ukiingia utashangaa, utafikiri upo mahali tofauti kabisa, kule Tanga - Amboni; sio Amboni, watu wamechimba kujificha wakati wa vita, kuna mengi ya namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi pia kuna vivutio kwa mfano, namna watu walivyokuwa wanafua vyuma asilia, uhunzi kule kwetu watu wanafua, wanatumia namna ambayo ni teknolojia ambayo ni ya kizamani lakini watalii wakiona wanashangaa ni kitu gani kinafanyika. Kwa hiyo, nashauri, tusing’ang’anie tu hifadhi ya misitu, hifadhi za wanyama na kadhalika, tuanze sasa kuunda kitengo maalum ambacho kitashughulika na vivutio asilia, vitangazwe na viorodheshwe, ni wapi utaona nini na wapi utafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)