Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema. Sambamba na hilo naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na wenzangu wote kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kuandaa hotuba hii. Pia naomba niwapongeze Wizara pamoja na bajeti finyu, lakini kuna mambo ambayo tunayaona yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba niipongeze Serikali kwamba asilimia 17 ya Pato la Taifa linatokana na utalii. Sambamba na hilo, asilimia 25 ya pesa za kigeni zinatokana na utalii. Pia Sekta ya Utalii imeweza kuzalisha ajira 1,600,00, jamani hili sio dogo, lazima tuipongeze sana Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie zaidi kuhusiana na kutangaza vivutio vya utalii hasa kupitia vyombo vya habari. Ni ukweli usiopingika kwamba vyombo vya habari ni nguzo kubwa sana katika kusaidia kutangaza vivutio katika nchi yetu ili watalii wengi zaidi waweze kufika katika eneo letu. Pia vyombo vya habari ni tegemeo muhimu sana katika kukuza utalii katika nchi yetu.

Sambamba na hilo, natambua kwamba Wizara imekuwa ikijitahidi sana, lakini naomba nishauri na ushauri wangu unatokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 31 hadi 33 amebainisha kwamba Wizara imeandaa vipindi 70 vya television, vipindi 51 vya redio na makala 36 kuhusu uhifadhi na vivutio vya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi hizo, naomba niishauri Wizara kwamba, ufike wakati sasa waandae mpango mkakati kwa ajili ya Waandishi wa Habari kutangaza vivutio vya utalii Tanzania. Kama watasema labda Media Strategy for Tourism in Tanzania ili sasa ule mpango mkakati uweze kutumika kwa ajili ya kuandaa Waandishi wa Habari mbalimbali waweze kuandika habari za utalii kwamba wawe wame-specialize katika kuandika habari za utalii. Naamini kabisa kwa kuandika habari nyingi zaidi za utalii pamoja na mengi yanayofanyika, tunaona kabisa kwamba kuna electronic media imekuwa ikijitahidi, lakini basi hebu uwekwe mkazo kuwe kuna ile media strategy ili kusudi mwisho wa siku sasa katika ile strategy ambayo itakuwa inaelezea malengo, ione jinsi gani ya utekelezaji na pia iwepo bajeti maalum kwa ajili ya Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa kwamba wasanii wamekuwa engaged kwa njia moja au nyingine, sasa hebu tuone kwamba engagement ya media nayo iwe katika mtindo wake ili kusudi sasa Waandishi wa Habari waweze kuandika vizuri hizi habari za kuhusu utalii. Nafahamu kwamba kwa mfano Mashirika kama TANAPA, Ngorongoro, TFS na TAWA yamekuwa yakishirikiana na Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika kama Wizara ina mpango maalum mkakati wa kuwashirikisha Waandishi wa Habari kwa muda wote, yaani isiwe tu kwamba kwa matukio fulani au labda ndani ya mwaka no, yaani kiwe ni kitu ambacho ni endelevu. Naamini kabisa Waandishi wa Habari wakishirikishwa kwa kipindi hiki wanaweza wakaleta mafanikio makubwa sana katika kuleta tija katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Waandishi hawa wa Habari, kukiwa kuna ile media strategy lakini pia waende wakajifunze katika zile nchi ambazo zimefanikiwa zaidi katika kuvutia watalii. Kwa mfano katika Afrika wenzetu kama Misri, South Afrika, Zimbabwe, Zambia na wengineo, wameweza sana ku-advertise. Pia kuna nchi zingine za nje kwa mfano kama Ufaransa, Italia, United States, Spain wao pia wameweza sana ku-attract watalii wengi sana. Kwa hiyo nashauri kwamba ufike wakati sasa na sisi tuwe tuna Waandishi wa Habari maalum kuhusu masuala ya utalii katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua muda siyo rafiki sana, basi kwa uchache, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)