Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa leo kuniweka hapa.
Pili, ningependa kuwashukuru Wanamuheza ambao wakati wa kampeni niliwaomba wanilete kwenye jengo hili na wamenileta, nawashukuru sana tena sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Hotuba ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja kwa asilimia mia moja. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba hiyo ameainisha mambo chungu nzima; nilikuwa nasoma mstari kwa mstari na nilikuwa na-underline, nilipofika mwisho wa kitabu
nikakuta nime-underline mistari yote kwenye kitabu hicho. Kwa sababu kila point, kila mstari ambao nilikuwa nauona, niliuona ni wa msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hotuba hiyo, lakini ningewaomba Waheshimiwa Wabunge waangalie namna Mheshimiwa Rais alivyokuwa anai-present hotuba hiyo, seriousness aliyokuwa nayo, commitment aliyokuwa nayo siku ambayo alikuwa anaiwasilisha hotuba hiyo na baada ya hapo matendo yake baada ya hiyo hotuba! Jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameainisha matatizo ambayo sijui ameacha tatizo gani kwenye hii hotuba. Ameanzia na huduma za jamii, matatizo yote yapo pale, matatizo ya maji, umeme, barabara, kila kitu kiko pale. Tatizo moja kubwa sana ambalo wote
humu Waheshimiwa Wabunge tunalo, isipokuwa wananchi wa Muheza wanalo zaidi ni la maji.
Wanamuheza wana shida ya maji! Yapo matatizo ya umeme, lakini umeme umefanyiwa kazi kubwa sana, REA imefanya kazi kubwa sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iangalie uwezekano, utaratibu ambao umetumika kwa REA, utaratibu huo utumike kwa maji vijijini. Wananchi wana taabu, sikupata nafasi ya kuchangia jana, lakini nina hakika Waziri wa Maji yuko hapa atahakikisha kwamba, kweli suala la maji linapewa kipaumbele kwenye bajeti inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuangalia matatizo hayo; sasa hivi tunakwenda kwenye sera ya Tanzania ya viwanda. Hatuwezi kujenga viwanda bila kuangalia kwanza haya matatizo ya umeme na maji tuyashughulikie, matatizo ya barabara, hivyo viwanda vitakavyopelekwa
huko, barabara zitapita wapi. Naamini Mheshimiwa Rais kutokana na ahadi zake alizozisema, kutokana na commitment ambayo anayo kwamba ahadi alizozitoa zitatekelezeka. Tumeona ahadi zinaahidiwa nyuma, kuna barabara yangu kule ya Amani mpaka Muheza kilomita 40,
awamu mbili zilizopita zimeahidi kwa kiwango cha lami barabara hiyo, lakini hakuna lami iliyowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Amani wanavuna, sasa hivi kuna viungo, kuna chai ambapo sasa ni wakati wa kuvuna viungo hivyo, wanashindwa kuteremsha mazao hayo, wanapata taabu kila saa magari yanakwama. Naamimi kabisa kwamba Waziri wa Ujenzi yupo hapa na ataliangalia suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia suala la viwanda, Tanzania ya viwanda, lakini naamini kwamba Waziri wa Viwanda ataangalia kiwanda kipi ambacho kinatakiwa kiwe wapi na mkoa gani ambao unatoa zao gani. Tuanze kufufua viwanda ambavyo vilikuwepo kabla ya kufikiria kuanza kujenga viwanda vingine, lakini Kiwanda cha Machungwa Muheza kianze kujengwa mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga kulikuwa na viwanda chungu nzima, viwanda vimekufa pale; ningefurahi sana kuona kwamba viwanda vile vinaaza kufufuliwa na wananchi wa Mkoa wa Tanga basi wanaanza kufaidika na viwanda hiyo. Kuna mazao chungu nzima ambayo yako Tanga na ambayo naamini kabisa kwamba kama viwanda hivyo vitafufuliwa basi tutakuwa na uwezo wa kujenga uchumi wetu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kuna mambo mengi ambayo yamezunguka Tanga, hapa imezungumzwa reli ya kati tu, reli ya Tanga - Arusha mpaka Musoma hadi Nairobi imesahauliwa kabisa. Ningefurahi na ningeshukuru kama ningekiona kitu hicho kwenye Mpango huu wa Bajeti ambao unakuja. Vivyo hivyo pamoja na Bandari ya Tanga, tunazungumzia mambo ya Bandari nyingine tunaacha Bandari ya Tanga ambayo ni bandari kubwa kabisa pale, kwa nini hatuizungumzii? Naomba Waziri anayehusika aliangalie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu; Serikali imeanza vizuri kabisa. Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya elimu bure na imeanza kutekelezwa. Lazima tuwe na pa kuanzia, matatizo madogo madogo yanaweza kuwepo, lakini lazima tuweke sehemu ya kuanzia. Tumeanza vizuri na naamini wananchi wote nchi hii wamefurahi kwamba elimu imekuwa bure. Hayo matatizo ambayo yanatokea hapo yatarekebishwa. Tusiikatishe tamaa Serikali hii kwa jinsi walivyoanza, tuwaunge mkono Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna shule nyingi ambazo zinaishia darasa la kumi na mbili (form four), lakini tuna shule chache sana za Serikali za kidato cha tano na cha sita.
Umefika wakati sasa hivi Serikali iondoe ukiritimba ambao upo wa kusema kwamba lazima shule za Serikali za form five na six ziwe boarding. Tunahitaji sasa hivi iwe day, watoto wetu waweze kusoma kwa sababu sasa hivi shule zimekuwa nyingi, lakini za form five na six zimekuwa ni chache, naomba mliangalile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa Rais ameongelea suala la wawekezaji, lakini ni lazima tuangalie na tukubali kwamba maandalizi yetu ya wawekezaji not friendly, bado kuna matatizo mengi sana EPZA, TIC, bado kuna ukiritimba mkubwa sana ndiyo maana
wawekezaji wanatoka hapa wanarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Mabalozi tuna Sera ya Diplomasia ya Uchumi, tuliambiwa tulete wawekezaji, tunawaleta wawekezaji, wanarudi. Kuna leseni sijui karibu 18 mara ya mwisho nilipokwenda TIC pale au vibali ambavyo mwekezaji anatakiwa apewe. Unategemea
huyo mwekezaji atawekeza kweli, jamani tuangalie hilo suala na kama mnataka Mabalozi watekeleze kweli Economic Diplomacy, basi tuhakikishe kwamba huu ukiritimba na huu urasimu unaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la utulivu na amani, Waheshimiwa Wabunge, lazima tukubali kwamba uchaguzi huu tumeufanya kwa utulivu na amani. Kama kulitokea uvunjivu wa amani, ni kidogo, lakini kazi ambayo wamefanya vyombo vya dola ni kubwa jamani. Ninyi hamuelewi namna ya kutuliza utulivu wa amani, ni kazi kubwa, vyombo vya dola vilikuwa havilali, ni lazima tuvipongeze na tuviunge mkono vyombo vyetu jamani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Balozi muda wako umekwisha.
MHE. BALOZI. ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumalizia kwa
kusema kwamba….
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha naomba ukae tafadhali.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.