Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kuunga mkono hoja ili lolote likitokea huko mbele basi niwe kwenye safe side. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa muda huu mfupi ili na mimi niweze kusema kidogo tu wakati huo nikimuachia Mheshimiwa Waziri nafasi ya kueleza na kuweka commitment za Serikali kwenye maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa shukrani, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai, afya na nimshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuniona mimi kijana na akaamua kunipa majukumu haya makubwa. Nimhakikishie tu kwamba kwa niaba ya vijana wenzangu ambao tunaendelea kutumika katika nafasi hizi hatutamuangusha yeye wala Watanzania katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwashukuru viongozi wa Kitaifa, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Kipekee kabisa nikushukuru wewe kwa jinsi unavyotuongoza na kutujenga sisi Wabunge na hasa sisi Wabunge vijana na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wapo humu kwa ushirikiano mkubwa ambao wanatupatia kama Wabunge, lakini mimi kwa nafasi yangu kama kiongozi kwenye nafasi ya Uwaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri wa Wizara yetu ya Nishati kwa kuendelea kuwa kiongozi, jemedari shupavu na aliyekakamaa kabisa na kutufikisha hapa ambapo wengi tunaogopa tunadhani hatutafika, lakini kwa maelekezo ya wakubwa wetu na yeye Wizara yetu imeendelea kufanya kazi ambazo Watanzania wanazitegemea. Pia niwashukuru watendaji wengine wote wa Wizara yetu ambao kwa kweli mengi tunayoyasema na kuyafanya hapa ni yale ambayo wao wametushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipowashukuru wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini walioamua kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa kunipa mimi kura za kutosha na kunituma kijana wao kuja kutumikia Taifa katika maeneo haya. Nimshukuru pia mke wangu kwa kuendelea kunivumilia na kunipa nafasi ya kufanya majukumu haya, lakini na familia kwa ujumla na maisha yanaendelea vema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitazungumzia maeneo matatu tu, kwa haraka haraka, maeneo mawili ni ya ufafanuzi mdogo na Mheshimiwa Waziri atakuja kumalizia. Eneo la kwanza Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia kuhusu kukatika kwa umeme. Sababu za kukatika kwa umeme zitaelezwa, lakini mimi niseme tumejipanga kupitia bajeti tunayoomba mbele yenu lakini tumejipanga kufanya yafuatayo kwa uchache wake ili kuhakikisha basi umeme unakuwa haukatiki mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza tutarekebisha miundombinu kama ambavyo tumekuwa tukifanya, tutaendelea kupanua wigo wa kurekebisha miundombinu. Pia tutasogeza vituo vya kupoza umeme karibia na watumiaji ili kupunguza ule wigo wa umeme kupotea na vimetajwa kwenye bajeti yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tutafunga vifaa mbalimbali vya kitaalam vya kuhimili vitishio vya kiasili kama radi, mvua na vitu kama hivyo nitavitaja baadaye kitaalam. Pia tunaweka njia ile ya kupitisha umeme salama kwa kuendelea kufyekea yale maeneo ili yasipate madhara ya miti kuangukia nguzo na nyaya za umeme.

Mheshimiwa Spika, la mwisho siyo kwa umuhimu kuendelea kuwasimamia watumishi tunaofanya nao kazi na hasa wale wachache ambao ni wazembe, wanaosababisha upotevu wa umeme na kuonekana kwamba umeme unakatika pengine bila sababu za msingi. Hivi juzi mmeona hatua ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu alizichukua pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu katika kuhakikisha kwamba watumishi wanakuwa waadilifu na wanatumika vizuri kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nataka nizungumzie kidogo tu ni kuhusu miradi ya REA. Kwa nini miradi ya REA mingine imekuwa ikichelewa kukamilika? Sababu zipo nyingi lakini mimi nitaje kidogo tu, mojawapo ni ile kuongezeka kwa wigo wa kazi ambayo mkandarasi amekuwa amepewa mara ya kwanza. Alipewa vijiji sita lakini tumefika site tumekuta vijiji vinavyohitaji umeme zaidi ni kama tisa au kumi kwa vyovyote vile ule muda wa awali tunajikuta tunatakiwa kuongeza ili kukamilisha yale ambayo yanatakiwa kufanyika.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ambalo ni la kuelezeka ni pale ambapo baadhi ya maeneo yanakuwa hayafikiki labda ni kwenye mapori, hifadhi au hali ya hewa ya mvua basi hapapitiki kwa sababu ya miundombinu kuchukuliwa na maji tunajikuta tunachelewa katika maeneo hayo. La tatu ambalo pia linatokea ni mkandarasi kujikuta ana kazi nyingi na mwisho wa siku ikawa ni ngumu kuzimaliza kwa wakati aliopewa kwa sababu pengine ya usimamizi kuwa mgumu kidogo na hilo pia tutalizungumza kwamba tumechukua hatua.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme kama alivyosema mwenzangu mmoja lakini kama alivyowahi kusema kiongozi wetu mstaafu wa Mkoa wa Kagera Mama yetu Prof. Tibaijuka kwamba kadri unavyopanua zaidi ndivyo watu wanavyokuwa na hamu zaidi. Sasa Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita zimeendelea kupanua wigo wa kupata umeme. Katika kupanua wigo wa kupata umeme wananchi wamekuwa wakiuhitaji sana na matumizi yamekuwa ni makubwa na hiyo sasa inapelekea pengine umeme usionekane wa kutosha lakini jitihada za Serikali ni wazi kabisa mambo yataendelea kuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo naomba nilizungumzie, mimi kwa nafasi yangu ya Unaibu Waziri na kwa jinsi tunavyofanya kazi katika michango mbalimbali iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge nimeona tunayo mambo kama 15 ambayo tunatakiwa kujivunia lakini pia yatakuwa ni chachu ya sisi kuendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania wanapata nishati ya umeme katika maeneo yaliyopo na umeme wa uhakika, sahihi, kila wakati na kwa gharama nafuu. Mambo hayo nikiyataja kwa haraka haraka tu, naamini dakika zilizobaki zitanitosha kuyajata hayo mambo 15; la kwanza ni bajeti ya Wizara ya Nishati kuwa na fedha ya maendeleo asilimia 98.9, hii fedha nyingine ni asilimia moja tu. Kwa hiyo, Wizara ya Nishati tumejipanga mkitupitishia kama ambavyo nitaomba mwishoni kufanya kazi kwa fedha tuliyopewa asilimia 98, tunaamini tutafika mbali kabisa.

Mheshimiwa Spika, lakini tumejipanga kuendelea kusimamia bora rasilimaliwatu na rasilimali fedha kama ambavyo imekuwa ikifanyika. Pia tunahakikisha kwamba tunafikisha ile adhma ya kuwa na umeme unaotosha kwa Watanzania wote. Kwa sasa tunao uwezo wa kuzalisha megawatt karibu 1,602, lakini jana usiku ndio tumekuwa na matumizi ya juu megawatt 1,201, kwa hiyo bado tuna kama megawatt 400. Sasa miundombinu ya kuzifikisha hizo zote kwa Watanzania ndiyo ambayo tunaomba sasa mtusaidie ili tuweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoomba kwamba naomba…

SPIKA: Bado dakika tano.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, eneo la nne ni kuendelea kuzalisha umeme katika miradi mbalimbali mkubwa sana ukiwa wa Mwalimu Nyerere, lakini pia tunayo Rusumo, tumesaini mkataba mwingine wa Malagarasi na tunaamini kwamba tutakuwa katika nafasi nzuri na miradi mingine. Pia tunahakikisha tutapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobakia takribani kama 1,500 kabla ya mwezi Disemba 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuboresha miundombinu yetu ya umeme kwa kufunga vifaa mbalimbali nilivyokuwa navisema, tunafunga surge arrester, combi unit, auto recloser socket breaker, AVR wameitaja hapa asubuhi na vitu vingine kama lightning arrester, tunahakikisha kwamba sasa umeme ukishakuwepo unaweza kuhimili hayo mambo ambayo ni ya kina naturally yanayoweza kuja kuzuia umeme wetu usiwe wa uhakika.

Pia tumejitahidi kutoa kazi nyingi kwa wakandarasi kidogo kidogo ili mkandarasi awe na wigo mdogo wa kufanya kazi na kumaliza, lakini tukiwa tunajenga uwezo wa watu wetu wa ndani kuweza kila mmoja kupata kazi na kumaliza kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tunahakikisha kwamba hakuna anayeuziwa nguzo, Mheshimiwa Waziri atakuja kulisisitiza na kuliweka vizuri. Pia tunaunganisha wateja kwa gharama ya shilingi 27,000 peke yake, Mheshimiwa Waziri atakuja kulisema.

Mheshimiwa Spika, lakini tutahakikisha kwamba katika hiki kipindi cha kupeleka umeme kwenye awamu ya tatu, mzunguko wa pili, tunafungua madawati ya malipo katika maeneo ya wananchi wenyewe. Mtu asifunge safari kufuata sehemu ya kwenda kulipia kilometa 20, 30; madawati ya wenzetu wa TANESCO yatakuwa katika Kijiji au kitongoji ambapo mradi unafanyika. Ilishaelezwa Mheshimiwa Waziri naamini atakumbushia kwamba tutaruhusu hata kulipa kidogo kidogo kwa utaratibu ambao mwananchi atakuwa anaweza ili mwisho wa siku ile shilingi 27,000 iweze kufikia hatua ambayo sasa anaweza kila mmoja akaimudu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunafurahi kwamba TPDC imefanya kazi kubwa, asilimia 60 ya umeme tunaouzalisha unatokana na gesi yetu tunayozalisha ambayo inasimamiwa na TPDC. Hilo ni jambo la kujivunia sana.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunalo bomba la mafuta limezungumzwa hapa, tunazo fursa kedekede zitakazo kuja. Pia tunafikisha Gridi ya Taifa katika maeneo ambayo hayakuwa na grid, Mkoa wa Kagera ikiwemo, imeshafika Nyakanazi, Mkoa wa Kigoma tutakwenda mpaka Katavi na ni katika muda mfupi sana tutakuwa tumekamilisha yote hayo.

Mheshimiwa Spika, mawili ya mwisho, Wizara imehakikisha inaweka utaratibu mzuri kabisa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri kuhakikisha mkandarasi anampata Mbunge na Mbunge anampata mkandarasi. Tunaamini hilo ni sehemu kubwa ambayo itatuwezesha kujadiliana, kushauriana na kusimamiana vizuri kabisa ili muda utakapofika basi yale tunayo yaahidi yaweze kuwa yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho japo siyo kwa umuhimu ninashukuru kwamba wakati haya yote ninayoyasema yanatokea, mimi ni Naibu Waziri kwa hiyo nitakuwa na mimi ninajivunia na historia itakuwa imeandikwa kwangu mimi, kwa familia, lakini na kwa Watanzania wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzetu mtupitishie bajeti yetu, siyo ndogo ni kubwa, lakini itaweza kufanya yale ambayo mtatuagiza kuyafanya kwa moyo thabiti kama ambavyo mmetusifia na kutusemea vizuri tangu mnaanza na kwa kuendelea kutumwa bila kuchoka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania basi wanakipata kile ambacho wanakitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WABUNGE FULANI: Kazi Iendelee.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)