Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa mwelekeo wa bajeti uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi alisema Serikali inataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, kuelekea uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwenye hotuba hii imesema itawavutia wawekezaji waje kujenga viwanda hapa nchini, kwa mwendo wa kusubiri wawekezaji waje wajenge viwanda hatuwezi kwenda na kufikia malengo ya Taifa tuliojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda wa miaka 10 sasa kila hotuba ya Viwanda na Biashara inaeleza kuwaita wawekezaji wa kujenga viwanda, ni kwa kiasi gani tumefanikiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeeleza Mkoa wa Tabora kunajengwa kiwanda cha Tumbaku ili kutoa ajira kwa vijana na ku-process tumbaku ambapo asilimia 60 ya tumbaku inalimwa Tabora. Tuelezwe ni mipango gani ya awali iliyofanywa ili kufanikisha azima hii ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Makaa ya Mawe kwa wingi sana kule Namtumbo-Songea. Kuna Malori zaidi ya 80 hadi 100 yanabeba makaa yale kila siku na kupeleka Kenya na kwingineko. Serikali itueleze, makaa hayo yanapelekwa huko kwa utaratibu gani, tunanufaikaje na makaa hayo ili kutuongezea nishati na kuokoa misitu yetu inayoteketea kwa uchomaji wa mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora tuna misitu na mbao zenye thamani kubwa. Mbao zile zinasafirishwa kwenda nje na Mikoa mingine kutengeneza Furniture (Samani). Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha tunapata kiwanda cha mbao Mkoa wa Tabora ili vijana wa Tabora wapate ajira na mbao ya Tabora iweze kuwa na thamani zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imekuwa ni dampo la bidhaa ambazo hazina viwango kwa kila kitu, vifaa vya umeme, nguo, viatu, vifaa vya ujenzi na kadhalika. Kwa nini Serikali imeshindwa kuweka sheria za bidhaa hapa nchini? TBS wameshindwa kabisa kudhibiti bidhaa duni hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango gani wa kuhakikisha bidhaa feki, duni na dhaifu haziingii hapa nchini? Sheria ya Uwekezaji inamtaka mtu anayekuja hapa nchini kuwekeza anatakiwa kuwa na mtaji wa kuwekeza na kutoa ajira kwa wazawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itueleze, Wachina na Wahindi wanaozagaa Kariakoo na maeneo mengine wakiuza maua, karanga, mitumba na kadhalika wanaruhusiwa na nani? Serikali imeruhusu ajira za wananchi wake zichukuliwe na watu wa nje ambao wanaitwa wawekezaji, tunakwenda wapi? Ni lini Serikali itahakikisha biashara ndogondogo zote hapa nchini zinafanywa na wazawa na hivyo kuwaondoa Wachina wote waliopo Soko la Kariakoo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vilivyobinafsishwa wawekezaji wamebadilisha matumizi na kufanya magodauni, vingine havijalipiwa fedha ya kununuliwa na vingine vimeng‟olewa mashine zote zilizokuwepo. Serikali inasema nini kuhusu viwanda hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe mazao yote yanachakatwa ndani ya nchi na hivyo kuongeza thamani tofauti na sasa ambapo mazao mengi yanasafirishwa ghafi na hivyo kukosesha mapato mengi Taifa na kupoteza ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaacha kuagiza samani za maofisini kutoka China na hivyo kununua samani ndani ya nchi kutokana na mbao ya Tanzania. Hii ni aibu kubwa!