Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia kwenye sekta hii ya nishati. Nami niungane na wote waliompongeza Waziri, Naibu na timu yake kwa juhudi na kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nitaomba kwa kweli niache yale ya kitaifa niende kwenye Jimbo la Butiama. Butiama ndiko alikozaliwa Baba wa Taifa na tunasema tunamuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kazi nzuri aliyowafanyia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sisi tunaishukuru Serikali hususan Serikali ya Awamu ya Tano na Sita kwa kujitahidi kuona kwamba vijiji vyote vinafikiwa na umeme. Ninavyo vijiji 59 na kwa kweli vyote kwa tafsiri ya access, kufikiwa vimefikiwa. Changamoto tuliyonayo ni huko kufikiwa walikokuona wananchi na wote wanatamani wapate umeme. Wakati fulani mtani wangu mmoja aliwahi kuongea hapa kadri tunavyopanua huduma ndivyo watu wanavyotamani na ni kweli kwamba kila mtu sasa anataka apate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, pale Butiama pamoja na kuwa na vijiji 59, vyenye vitongoji 370 ni vitongoji 147 vilivyofikiwa sawa na asilimia 40; vitongoji 223 havijafikiwa sawa na asilimia 60. Hata kwenye hivyo vijiji na vitongoji vyake unakuta wamegusa center tu. Kwa mfano, ninayo Kata moja maarufu ya Nyamimange, Tarafa ya Kiagata kuna vitongoji 10 lakini vitongoji vyenye umeme ni vitatu tu; Kiagata Madukani, Kewancha na Serengeti ndiyo vyenye umeme lakini vitongoji saba vifuatavyo Isangura, Kebwasi, Nyamihuru, Sania, Mtakuja, Masongo, Mamititu havina umeme na hali iko hivyo karibu kwenye vijiji vingine vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hali kama hii haiwaridhishi wananchi wanaona kama wameachwa lakini hali inakuwa mbaya zaidi pale taasisi za umma zinazohudumiwa wananchi wengi hazifikishiwi umeme kama hospitali, vituo vya afya, zahanati na shule. Ni vizuri tukatambua tunapokwenda kwenye REA III round II wajue kwamba bado wana kazi kubwa sana huko Butiama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru juzi tumepewa orodha ya majina ya wakandarasi watakaohudumia majimbo na wilaya zetu. Kwa Butiama sijui ni bahati mbaya au nini tumepewa mkandarasi anaitwa Giza Cable Industries. Sasa nimemtafuta tangu juzi simu yake inasema haipatikani jina lenyewe walilochagua wala halitii matumaini. Bora angeita Nuru au Mwanga yeye kaita Giza na hapatikani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wananchi wengine wanalipia umeme lakini hawaunganishiwi, hili nalo ni tatizo mwenzangu amelisema asubuhi. Ninaye mwananchi hapa Mama Omari wa Kitongoji cha Kohoko kule Nyamikoma amelipia nguzo mbili Sh.551,147.32 tangu tarehe 10/04 lakini hawajasogeza nguzo wala hawajachimba mashimo na hakuna kinachoendelea wakiulizwa wanasema tatizo ni mita. Sasa kama tatizo ni mita walikuwa na sababu gani ya kumtaka mwananchi huyu alipie.

Mheshimiwa Spika, lipo hili tatizo la kukatikakatika umeme hili limesemwa na Wabunge wengi. Kule majimboni wameweka ma-group ya WhatsApp haya watu wanazungumza umeme unavyokatika mpaka wanatumia maneno yanayofedhehesha Shirika letu. Nakumbuka wakati fulani nikiwa pale Simiyu na hata Butiama naona yanaendelea mambo ya kukatika kwa umeme, wanasema umeme wa TANESCO unavyokatika utafikiri mwanamuziki Fally Ipupa.

Sasa nikajiuliza Fally Ipupa ni nani nilikuwa sijamjua, kwamba umeme unavyokatikakatika ni kama Fally Ipupa au wengine wana-comment yamekata umeme yaani badala ya wamekata wanasema yamekata umeme, yamerudisha, yamekata tena yaani namna umeme unavyokatika unakera wananchi mpaka wanasema utafiriki kuna mtoto anajifunza namna ya kuwasha na kuzima. Mheshimiwa Kalemani tunajua unafanya kazi kubwa sana lakini tuombe wataalamu walioko mikoani na kwenye wilaya pengine hawatusaidii vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona nimepigiwa kengele basi mimi nishukuru kwa nafasi hii, naunga mkono hoja nikiamini kwamba haya niliyoyasea yatafanyiwa kazi. (Makofi)