Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Ussi Salum Pondeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chumbuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi niwe miongoni wa wachangiaji wa hotuba hii nzuri ya Wizara ya Nishati ambayo kusema kweli inafanya vizuri. Pia nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake, pamoja na Naibu Waziri lakini na watendaji wote wa TANESCO kiujumla wao wanafanya kazi moja nzuri sana ambayo wote tunaikubali. Kiukweli ni wizara ambayo kwa kiasi kikubwa imetutoa tongo machoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina jambo moja ambalo nataka nilielezee au nimpe ujumbe Mheshimiwa Waziri. Kuna tatizo ambalo lipo muda mrefu baina ya TANESCO na ZECO kuhusiana na bei ya umeme. Mimi ni mjumbe wa Kamati na mara nyingi nimekuwa nikilisema hili lakini utaratibu wake au hatua zake zinavyochukuliwa zinachukua muda kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nimeamua kulisema hapa kama jambo mahsusi, ambalo nataka niiambie Serikali yangu na Mheshimiwa Waziri, tatizo ambalo lipo hapa ZECO wanauziwa umeme na TANESCO kwa bei ya Sh.160.4 kwa KV moja. Hata hivyo, kutokana na uchumi wa Zanzibar, ZECO wanasema hawawezi kununua kwa bei hiyo, wana uwezo wa kununua KV moja kwa Sh.130. Hili suala limekuwa linakaliwa vikao muda mrefu bila kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo ninaloliona mimi mpaka nikaamua kulizungumzia hapa, kama mtakumbuka ndani ya miaka miwili, mitatu nyuma kuna jambo lilikuwa kubwa zaidi katika mambo ya umeme baina ya ZECO na TANESCO. Hayati Rais aliyepita wa Awamu ya Tano, Dkt. Joseph John Pombe Magufuli aliweza kutufutia Zanzibar deni la shilingi bilioni 22 kitu ambacho leo ukiwauliza Wazanzibar mnamkumbuka vipi Dkt. John Pombe Magufuli basi moja ya jambo ambalo Wazanzibar wataendelea kumkumbuka ni hili la kutufutia deni. Leo hii linakuja jambo lingine dogo hili la bei, kwa nini Waziri usiwaambie watendaji wako wakakaa na watendaji wa kule wakaangalia jinsi ya kulimaliza mapema suala hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, deni lile lilikuwepo mwanzo ambalo lilikuwa linaleta zogo na tafrani humu ndani ya Bunge, kama unakumbuka TANESCO wakija kwenye Kamati yetu tukiwauliza mna madeni mangapi wanasema ZECO tunaidai shilngi bilioni 132; ZECO ukiwauliza wanasema sisi tunadaiwa shilingi bilioni 22 ambazo Hayati Dkt. John Joseph Magufuli alizifuta. Hii ni kwa sababu ZECO walifika mahali wakawa wanalipa current bill tu lakini hawalipi VAT mwisho wa siku TANESCO wanaandika VAT pembeni, hapa tunarudi kulekule. ZECO wanasema tunalipa shilingi 130, TANESCO wanasema shilingi 160.4 baada ya miezi sita na miaka miwili mbele TANESCO watasema wanaidai ZECO shilingi bilioni 54 na ZECO watasema sisi tunadaiwa shilingi bilioni 12. Hili sio jambo zuri na uwezo wa kulitatua Waziri wa Nishati wa Tanzania Bara Mheshimiwa Dkt. Benard Kalemani anao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine zuri ambalo namuamini Waziri, miradi mikubwa na mizuri ya kimkakati ambayo tunaendelea kuisimamia sisi kama wanakamati lakini kwa miongozo yake mambo yanaenda vizuri nashangaa jambo hili dogo linachukua muda mrefu. Kuna Bodi nzuri ya Mzee Kyaruzi sisi tunamuamini kwa uzoefu na maadili aliyokuwa nayo na uwezo aliokuwa nao kiasi cha kuaminiwa zaidi ya vipindi viwili maana yake hili si jambo la kuchukua zaidi ya miezi miwili, mitatu. Hata hivyo, namuamini Waziri na naamini atakapo-windup anaweza akatuletea jibu moja zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kwa sababu nilisema nina jambo moja mahsusi, mimi katika Jimbo la Msalala nina interest zangu pale lakini nataka niwaambie watu wa REA mpaka leo vijiji 32 tu ndiyo vimepata umeme na vijiji 63 havijapata umeme. Jambo hili linatupa shida na sijui kwa nini wakati uwezo wa kupeleka umeme pale upo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba nisichukue muda wako. (Makofi)