Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa sababu ya muda na mimi nianze kwa kuishukuru sana Wizara ya Nishati, nimshukuru Waziri, Naibu Waziri na Wakurugenzi wake wote ambao wanashughulika kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa kutosha. Ukweli ni kwamba TANESCO pamoja na Taasisi hii wamefanya kazi kubwa sana. Ukikumbuka toka mpango huu uanze mwaka 2014 Awamu ya Tano ilipoingia, Awamu ya Sita leo tunaendelea nayo kumekuwa na jitihada kubwa sana na wananchi wetu mahitaji yao mengi ukitoa maji, umeme na barabara na afya jambo kubwa sana wanatutazama namna gani tunapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niongelee mambo mawili tu, suala la usambazaji wa umeme, ukweli ni kwamba kazi kubwa sana imefanywa. Ukitazama scope ya kazi ambazo wanapewa wakandarasi zinakuwa ni ndogo sana kulingana na mahitaji ya maeneo husika. Kwa mfano, ukiangalia Jimbo la Nyamagana tumebahatika kupata miradi ya REA na sababu na sifa tulikuwa nazo kwamba tunayo maeneo kwenye mitaa yana sifa sawa na vijiji.

Mheshimiwa Spika, maeneo haya yalistahili na unapopata kata kwa mfano ina mitaa mitano ambayo ipo eneo moja ina zaidi ya kilometa 100 kwa mfano au 80 inapata LV kilometa zisizozidi 20 peke yake ni kuendelea kuongeza lawama kwenye Serikali. Mheshimiwa Waziri nikuombe hata tunapofanya miradi ya densification tujitahidi sana kwenda mbali ya pale tulipoanza, kama tulitoa LV kilometa 12 tusirejee tena kutoa chini ya 12 twende mbele zaidi ikiwezekana 20 na kadhalika. Sisi kwa Nyamagana nataka nikuhakikishie kwamba Mheshimiwa Waziri amefanya kazi kubwa sana na hii kazi aliyofanya imewasaidia wananchi wengi wa Jimbo la Nyamagana kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee miradi ya Peri Urban itakuwa mkombozi na kulisaidia sana Shirika la TANESCO. Kwa nini Peri Urban ifanyike kwa kasi na jana nimeona Waziri ametoa orodha ya wakandarasi wa REA naomba na orodha ya wakandarasi wa Peri Urban tuipate ili tujue scope yetu imekaaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwanza peke yake ukichukua Ilemela na Nyamagana Mheshimiwa Waziri nataka nikuhakikishie ukipeleka leo umeme wa Peri Urban malipo ya watu wake na unit wanazotumia kwa siku mpaka mwezi siyo sawa na maeneo mengine unaweza kuyalingalisha. Hatukatai umeme usiende kila sehemu lakini Waziri atakubaliana nami kuna sehemu unafunga transformer leo ya kuhudumia watu 50 miaka minne umewaunganisha watu wasiozidi kumi peke yake, hii ni hasara kwa TANESCO na lazima muangalie namna bora ya kuwasaidia mnapoweka miradi ya uzalishaji kwa haraka inasaidia sana maeneo yetu mengi.

Mheshimiwa Spika, ukienda Kata za Igoma, Kishiri, Lwanima, Buhongwa, Nyangu, Nyakabwe Mheshimiwa Waziri alitusaidia alipokua na Waziri Mkuu, lakini ukweli ni kwamba tatizo bado ni kubwa na eneo lililopata ni karibia kilometa 12 peke yake eneo lililowazi zaidi ya kilometa 32. Bado ni changamoto na wananchi wanalalamika wanaona kama tumewatenga na tumewabagua lakini ukweli ni kwamba mahitaji ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafahamu hata ukienda Ilemela pale kwa mama yangu Mheshimiwa Angeline kule kwenye Kisiwa cha Bezi bado kuna changamoto kubwa hakuna umeme na uliopo ule wa Jumeme ni kama matatizo yaliyopo hapa kwa ndugu yangu Mheshimiwa Shigongo. Mheshimiwa Waziri umefanya kazi nzuri na kubwa sukuma hapa ulipobakisha, umaligije ikazi ishile na tulole yingi lulu ihaha, mambo yanakuwa yameenda hivyo vizuri au siyo bwana, lakini ukweli ni kwamba kazi kubwa mnaifanya. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mabula ng’welage geke. (Makofi/ Kicheko)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ee welelagwa gete, welelagwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwenye hii miji tunayoitaja hata hasa kwenye majiji haya makubwa ni hizi ni fedha tumeziacha. Ukienda hata kwa Naibu Spika kule kwenye Kata za Iziwa, Itengano, Iduda hata Itende na kwenyewe ukifunga umeme wa Peri Urban una uwezo wa kuingiza hela nyingi sana Mheshimiwa Waziri na ikasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa kwa sababu ya muda kumekuwa na mjadala mkubwa sana hapa ambao unaendelea…

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa hiyo inatoka wapi endelea na taarifa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nataka kumwambia mchangiaji Mheshimiwa Mabula kwamba hata maeneo ya Kibaigwa, Kongwa na Sengerema Mjini yote yanahitaji umeme. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Hata kule Ilemela kwa Mheshimiwa Angeline Mabula pia, endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataja miradi ya Peri Urban ambayo watu wa majiji tumeomba ili ije kutusaidia kupunguza mzigo mzito. Mwananchi wa kawaida kabisa anayeishi kwenye majiji ili aunganishiwe umeme anahitaji shilingi 512,000 au shilingi 321,000 ili aweze kufikishiwa umeme kwenye eneo lake. Siyo wote waliopo mjini wana uwezo wa kumudu gharama hiyo ndiyo maana tunaomba watu wa Peri Urban. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kumekuwa na mjadala mrefu sana hapa siku mbili hizi zilizopita na uliuweka vizuri juu ya TBS kupewa zoezi la kuweka vinasaba kwenye mafuta. Nafahamu jana umetoa maelekezo mazuri sana na naomba wakati wanaandaa sheria tufikirie nje ya box, pale bandarini kuna watu wanaitwa Wakala wa Vipimo na Mizani wajibu na shughuli yao kila meli inapotoka na kuingia wanakwenda kupima idadi ya mafuta yaliyokuja, ikifika nje wanakwenda kupima.

Tunapozungumzia kupokea lita karibia laki tano na hao wote ni taasisi zilizoko chini ya Serikali kwa nini tusifikirie vizuri zaidi na Mheshimiwa Waziri hili wakalichakate, tunaweza kuwapa watu wa Wakala wa Vipimo na Mizani, watu wa TBS wakabaki na jukumu lao la kuhakiki ubora wa mali ambayo inaingia nchini kwetu, kwa sababu wamekuwa accredited na dunia wamejulikana na wanatambulika kwa kazi nzuri. Kwa hivyo, nataka niliache kwako, sheria zinapokuja tuzitafakari na tuone namna ya kuziweka vizuri ili tujue sehemu ya kutokea. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja asilimia mia. (Makofi)