Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa naomba niunge mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali ya CCM inayoongozwa na Jemedari Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu kwa kufanikisha mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Tumeahidiwa dola za kimarekani 140 sawa na shilingi bilioni 324,000.4 kwa ajili ya ya utekelezaji wa mradi muhimu sana wa maji Mto Malagarasi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu utaweza kuwasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani kwa sababu mradi wa umeme wa maji gharama zake ni ndogo kuliko za mafuta ambapo Mkoa wa Kigoma tumekuwa tukitumia generator kwa muda mrefu. Kupitia mradi huu ambapo tutakuwa tunatumia maji tutaweza kupata umeme wa uhakika na vilevile utakuwa ndio ukombozi wa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na mikoa ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kuipongeza Serikali kwa miradi ya REA na kwa kutekeleza Ilani ya CCM kwa ahadi iliyotoa kwamba itaweza kuunganisha vijiji vyote kupitia miradi ya REA, naishukuru Serikali ya CCM. Sitaweza kuvitaja vijiji kwa sababu mimi ni Mbunge wa Mkoa nikianza kutaja vijiji vyote siwezi nikavimaliza, naomba vijiji vile ambavyo havijapatiwa umeme Serikali iweze kuwasimamia wakandarasi ili vijiji vile ambavyo havijapatiwa umeme viweze kupatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali kwa sababu kwa muda mrefu tumekuwa tukishauri kuhusu hifadhi ya mafuta ya dharura. Kwa kuwa na hifadhi hii nchi itaweza kufanya biashara na nchi zinazotuzunguka, kwa kuwa mafuta mengi yanayoingia nchini yanaenda nchi za nje. Kwa hiyo, nashauri Serikali iweze kuweka vivutio na kushauri wawekezaji wale wenye maghala waweze kujenga maghala mengine kusudi mafuta yawe yanahifadhiwa na hao wafanyabiashara na hatimaye mafuta yawe yanaweza kuuzwa nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, naomba Serikali itusaidie Mkoa wa Kigoma na hasa Wilaya ya Kasulu kwa sababu idadi ya watu imeongezeka na kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu mahitaji ya kupata umeme nayo yameongezeka. Naomba Serikali ipeleke nyaya za kutosha ili wananchi waweze kupatiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja (Makofi)