Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hii; Katibu pamoja na watendaji wao wote kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya. Pia napenda kuunga mkono hoja kutokana na hizo dakika tano kuwa ni chache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba umeme ni maendeleo lakini pia ni huduma. Lengo la Serikali ni kusambaza umeme vijijini zikiwemo na taasisi za umma kama vile zahanati, vituo vya afya pamoja na shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu la Nyang’hwale nina vijiji 62, vijiji ambavyo tayari vimeshapitiwa na umeme mpaka sasa hivi ni vijiji 44 bado vijiji 18. Katika vijiji 44, nakuomba Mheshimiwa Waziri ongea na Waziri wa TAMISEMI ili sasa Wakurugenzi waweze kupewa maelekezo wa nchi nzima wakiwemo wa Nyang’hwale ili waweze kulipia zile gharama za Sh.27,000 ili taasisi zetu; zahanati, shule za msingi na sekondari ziweze kulipiwa na kupewa huduma ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la pili kwamba Wilaya ya Nyang’hwale ina wachimbaji lakini pia umeme tunauhitaji sana kwenye maeneo ya wachimbaji. Maeneo hayo ni kama vile Igalula, Isekeli, Ifugale na maeneo mengine, waweze kuvutiwa umeme kule ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, shida kubwa iliyoko jimboni na maeneo mengine wamezungumza Waheshimiwa Wabunge, jambo la kukatikakatika kwa umeme linawatia hasara sana wananchi. Umeme kwa Jimbo la Nyang’hwale unakatika zaidi ya mara tatu au nne kutwa nzima. Vifaa vya umeme vinaharibika lakini pia bidhaa zilizomo ndani ya freezer, vinaharibika. Tatizo ni nini? Kwa sababu umeme unakatika unatutia hasara sana wananchi hasa tunaotumia umeme kwenye majumba yetu na shughuli zetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimepewa jina la mkandarasi wangu atakayeenda kusambaza umeme katika vile vijiji 18. Cha kushangaza na kusikitisha ni kwamba nimeongea naye jana akasema mpaka sasa hivi hajapata fedha kutoka CRDB, tatizo ni nini? Mheshimiwa Waziri lichukue jambo hili ongea naye kujua kwa nini hajapewa fedha mpaka sasa hivi ili aweze kwenda site. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, gharama ya kuunganishiwa umeme ni Sh.27,000, lakini wananchi wetu wapo maeneo mbalimbali, unakuta kutoka eneo moja kwenda eneo lingine ni zaidi ya mita 500 mpaka mita 1000, je, huyu aliyeko kwenye mita 500 mpaka mita 1000 gharama ni hiyohiyo Sh.27,000, nguzo na nyaya hazimhusu? Kwa hiyo, pamekuwa na changamoto nyingi, kuna wananchi wetu wengine wamelipia muda sana zaidi ya miezi mitano mpaka mwaka mmoja hajavutiwa umeme anaambiwa tatizo ni nguzo, hasa tuambieni Sh.27,000 ukiwa ndani ya mita ngapi unafungiwa umeme kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli mimi sina mchango mkubwa zaidi yangu ni hayo, lakini nampongeza sana Mheshimwia Waziri kwa kazi nzuri na Naibu Waziri na Katibu kazi zao ni nzuri na wanachapa kazi. Mheshimiwa Waziri yachukue haya ambayo nimeyachangia kwenye upande wa Jimbo langu la Nyang’wale.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)