Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa sababu ya ufinyu wa muda, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuzungumzia moja kwa moja mambo yanayohusu jimbo langu. Nimeshazungumza mara kwa mara na Mheshimiwa Waziri kuhusu tatizo kwenye Visiwa vya Zilagula pamoja na Maisome ambako wananchi wale wanategemea umeme kutoka kwa watu binafsi. Hivi ninavyozungumza wananunua unit moja kwa Sh.2,400. Huyu ni mwananchi wa kawaida, maskini, nimeshazungumza na Mheshimiwa Waziri naomba atakapokuwa anafunga hotuba yake hapa awaeleze wale wanaitwa Jumeme na PowerGen, alishatoa maelekezo wauze umeme kwa Sh.100 lakini baada tu ya Hayati kupumzika wamepandisha bei. Kuna maneno wanayasema kwamba aliyekuwa anatusumbua ameondoka, hawajui kama mama Samia ni moto wa kuotea mbali. Kwa hiyo, mimi nina nia ya kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri kama hatakuwa na maelezo ya kutosheleza kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nizungumzie maeneo ambayo bado kuna matatizo makubwa sana ya umeme kwenye jimbo langu katika Kijiji cha Itabagumba, Makafunzo, Bupandwa, Nyehunge, Kanyala, bado kuna shida kubwa sana ya umeme. Umeme uko kwenye center tu, ukizama huko ndani kuna nguzo na maeneo mengine hakuna nyaya. REA Mkurugenzi yuko hapa, Mheshimiwa Waziri na Naibu mko hapa mhakikishe sasa umeme unakwenda moja kwa moja mpaka kwenye maeneo ya ndani kabisa ili lawama hizi ziweze kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda niongelee kuhusu suala la nishati, kuna uhusiano mkubwa sana kati ya nishati na maendeleo ya watu. Taasisi moja inaitwa MDI ilifanya utafiti wakasema unapoongeza matumizi ya umeme kwa asilimia moja, unaongeza pato la Taifa kwa asilimia 1.72. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yangu hapa ni nini? Naomba kwanza nipongeze sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kwamba umeme unapatikana kwa asilimia kubwa. Hii imewezesha pato la nchi yetu kukua. Naomba kabisa tuendelee kutafuta nishati kwa gharama yoyote ili nchi yetu iweze kuwa Africa Power House. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili likifanyika, hata kama tunapingwa, mimi nakumbuka wakati tunaanza ujenzi wa Bwawa la Nyerere tulipingwa, walisema kwamba kuna masuala ya mazingira. Namshukuru sana Hayati, namshukuru mama Samia, walisema hata kama kuna issue ya mazingira bwawa litajengwa na bwawa limejengwa. Jana nimesikia wameanza tena Wazungu kusema bomba la mafuta lina issue ya mazingira kwa hiyo hatutapewa mkopo; tusiwasikilize Wazungu, wanajua kwamba tukishakuwa na nishati tutakuwa na nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Baba wa Taifa, Mwalimu J. K. Nyerere alijua kwamba ili tukue kiuchumi tunahitaji nishati. Rais wetu, Hayati, alikuja hapa ametekeleza ndoto ya Baba yetu wa Taifa. Kweli tutakuwa na umeme wa kutosha katika Taifa letu na umeme utakuwa ni wa bei rahisi kuliko wakati mwingine wowote, wawekezaji watakuja na biashara zitaongezeka. Unapoongeza umeme, unaongeza production na GDP ya Taifa lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge tulioko hapa leo, tuna bahati ya kuwa ndani ya Bunge hili, wazee wetu waliotangulia wamefanya maamuzi mazuri sana sisi leo ni Taifa bora na sisi tuliopo hapa ndani tufanye maamuzi bora kwa ajili ya watoto wetu watakaokuja baada ya sisi. Nataka Bunge la Kumi na Mbili likumbukwe kama Bunge lililohakikisha Tanzania inakuwa Africa Power House kwa kuwa na energy ya kutosha ili tuweze kukua na uwezo huo tunao. I don’t care where the source is, as long as ni power, leta power, hata kama ni nuclear power leta nuclear power ili tuweze kuwa na nguvu kama Taifa. Tukiwa na nishati hakuna atakayetutisha, uchumi wetu utakuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu wake na moyo wa kujituma. Nampongeza sana Naibu wake, TANESCO na REA. Ninachowaomba sasa wakachape kazi zaidi ili Taifa letu liweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kama hakutakuwa na majibu ya suala la umeme unit moja Sh.2,400 nitashikilia shilingi. Naomba niishie hapo, Mungu ibariki Tanzania, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)