Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kupongeza kazi nzuri ambayo inafanyika hasa ya usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Katika jimbo langu ni kweli kumekuwa na utekelezaji mzuri sana kwenye awamu hizo zilizopita hadi maeneo ambayo kwa kweli ni ya mbali sana na kwa sababu eneo langu ni la milima, Kata kama zile za Kimala, Idete na Masisiwe, nyaya na mita zimefungwa lakini umeme bado haujawashwa. Nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri baada tu ya kumaliza bajeti hii twende naye kwa sababu wakimuona najua kabisa umeme utawaka kwenye kata zile. Kwa hiyo, naamini kwamba yuko tayari na tutaongozana na kwa sababu nimeona dalili kwamba baada tu ya kuwa nimeongeaongea watakuwa wanaendelea kuhakikisha kwamba wanakamilisha wakijua ziara yako inakaribia. Kwa hiyo, Kata hizi za Kimala, Idete na Masisiwe tunamsubiri kwa hamu ili umeme uweze kuwaka.

Mheshimiwa Spika, lakini bado kuna kata tatu nzima ambazo hazijafikiwa na umeme. Kuna Kata nzima za Nyanzwa, Ukwega na Udekwa. Kwa mfano, Kata ya Ukwega kwenye Kijiji kile cha Ipalamwa kuna kituo cha afya kimejengwa kwa hisani lakini hakiwezi kufanya upasuaji hata kama wana vifaa kwa sababu hakuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi niliyoyataja haya tayari kuna kilimo kikubwa sana cha parachichi na watu wameshaanza kujenga majengo kwa ajili ya kuhifadhia mazao yale ambayo yanahitaji umeme. Kwa hiyo, naamini kwamba atakapokuwa ameshafikisha umeme kule basi shughuli za kiuchumi zitaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, napenda nimkumbushe Mheshimiwa Waziri nimeshaongea naye pamoja na Naibu Waziri; pale kwenye Kijiji cha Kipaduka, Kata ya Wambingeto ambapo kulikuwa na mradi ulipeleka pale transfoma, nguzo zipo, transfoma ile iko kwenye ofisi za kijiji kwa muda mrefu na tatizo ni kwamba kuna afisa mmoja huko hajatoa kibali ili REA iweze kufanya kazi ile. Wale watu wa Kipaduka wamekaa na zile transfoma kwenye ofisi ya kijiji muda mrefu mno, hawawezi hata kujua wafanye nini basi naomba yule anayetoa kibali kama yuko hapa kwa sababu najua maafisa wenu wanahudhuria akumbuke kutoa hicho kibali ili pale Kipaduka hilo tatizo liweze kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kutaja pia Kata ya Ilole, kwenye Kijiji hichohicho cha Ilole kuna tatizo kwamba umeme haujafika na hakimo kwenye orodha ya vijiji ambavyo havijapatiwa umeme. Kwa hiyo, naomba nacho kiongezwe ili vijiji vile ambavyo havijapata umeme viweze kufika 22 vikiwa ni pamoja na Vijiji vingine kama Muhanga, Idunda na Ibofwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kuzungumzia suala la hifadhi ya mazingira, hasa kwa sababu Jimbo la Kilolo ni jimbo ambalo ndilo linalotoa maji mengi yanayotiririka kwa ajili ya Bwawa la Mtera.

Naomba kutoa angalizo hili kwa sababu tunajua kwamba umeme wa maji bila kuhifadhi haya mazingira inawezekana ikafika wakati tukakosa maji. Kwa sababu najua Waziri anayehusika na mambo ya mazingira yuko hapa pia, napenda kuhimiza kwamba ni suala la kuliangalia kwa sababu katika maeneo haya kuna kilimo kinaendelea kama tusipopanga vizuri na tukaweka hifadhi ya mazingira vizuri, basi upo uwezekano baadaye kuja kukosa maji. Hii inategemea na ufadhili wa miradi iliyomo pembezoni mwa mito na hasa vile vijiji ambavyo maji yanatiririka kuelekea kwenye hilo eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)