Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, naomba niipongeze sana Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Kwa kweli wamefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii inashughulikia masuala ya nishati ambayo ni muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu. Naamini kwa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo wameianzisha, miradi kama ya SGR, Nyerere, Bomba na kadhalika, kwa kweli wakiisimamia vizuri itatoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nizipongeze taasisi ambazo ziko kwenye Wizara hii zinafanya kazi nzuri sana. Ni kwa mara ya kwanza nimesikia TANESCO wamepata faida kubwa, kwa kweli nawapongeza sana, nina imani kazi hii itaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji nishati na Serikali ya Awamu ya Sita imetenga fedha zaidi ya shilingi trilioni 2.3 ili mambo kadhaa yajitokeze katika nchi hii. Sasa kwa sababu ya muda nitasema mambo makubwa matatu.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, nishati itasaidia kuhakikisha kwamba kunakuwa na maisha bora kwa Watanzania wote. Watanzania wanaoishi mijini na vijijini, wanahitaji umeme wa uhakika, wanahitaji gesi, mafuta na kadhalika. Kwa hiyo, nina imani fedha hizi ambazo Serikali imewekeza zitachochea sana kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaimarika na umaskini unapungua kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, fedha hizi zilizotengwa tunategemea zitatengeneza ajira nyingi kwa Watanzania ambalo limekuwa ni tatizo la muda mrefu. Ajira zitakazotengenezwa katika bomba la mafuta, gesi, mafuta na vituo vya mafuta, zitawasaidia Watanzania. Nina uhakika kwamba iwapo vitasimamiwa vizuri, vitasaidia sana Watanzania kule vijijini kuanzisha biashara, kufanya kila aina ya kazi kwa sababu hivi vitu ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, nishati ya uhakika itasaidia na kuhakikisha tunajenga viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali za Tanzania. Hatuwezi kujenga viwanda imara kama nishati itakuwa siyo ya uhakika au kama tutakuwa na umeme unaokatikakatika. Kwa mfano, kama sasa hivi katika Mkoa wa Songwe, kuna tatizo kubwa sana la kukatika kwa umeme kila mahali. Unaweza ukakatika zaidi ya mara kumi kwa siku na kuna maeneo mengi hayana umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo wameifanya REA na ambayo Mheshimiwa Waziri ameifanya lakini vipo vijiji karibu 31 kwenye Jimbo la Vwawa havina umeme hadi sasa hivi. Bado kuna mitaa kadhaa haina umeme, Mitaa kwa mfano Isangu, ni kijiji lakini hakina umeme; Mitaa ya Rondoni na Shanko, kote hawana umeme. Vijiji kama Idunda, Ipyana, Iromba, Namwangwa, Nyimbili, Hantesya, Izumbi, Sakamwera, Mponera, Ipunga, Ipapa, Mpanda, Masangura, Ihoa, Welu II, Idibira, Rusungo, Namlonga, Maroro, Isararo, Sakamwera, Mantengu, Chizumbi, Rudewa, Msambavwanu, Kilimampimbi na Kata nzima ya Nyimbili; vyote havina umeme hadi sasa. Pamoja na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Waziri, naomba vijiji hivi vyote vipatiwe umeme kama alivyosema na naamini tutakuwa tumefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amesema nguzo hazilipiwi na wananchi watalipa Sh.27,000 wale ambao mitaa yao inafanana na vijiji. Mimi katika Jimbo la Vwawa bado ni vijiji na ndiyo maana tumeshindwa kupata sifa ya kuwa Manispaa kwa sababu maeneo mengi bado ni vijiji lakini mpaka leo hii ukienda TANESCO wanakwambia lazima ulipie nyaya na nguzo na wanakwambia kwamba sisi hatuhusiani na REA labda ukitaka hivyo nenda REA, REA wanakwambia huko TANESCO.

Naomba masuala haya yaangalie vizuri toeni waraka wa kuwaelekeza watendaji wa TANESCO ili wazingatie maagizo ya Wizara. Ikitokea Wizara mnatoa maagizo na TANESCO wanasema sisi hatutekelezi, hatuna waraka, kwa kweli mnaleta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)