Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, tunasema kwamba tunapaswa kutambua na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano nyuma katika suala la nishati na umeme.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi na kwa kweli katika hili mimi nitajikita zaidi katika kutoa complement na kuongelea maeneo mawili, matatu ya kitaifa, lakini pale ambapo tunaona Wizara zinafanya vizuri na kuleta mapinduzi chanya yanayobadilisha uchumi wa Taifa sisi kama Wabunge tuna nafasi ya kutoa complement ili Taifa lijue nini kimefanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwa dhati ya moyo wangu uzalendo ulionyeshwa na Waziri Kalemani, mimi kwa hili naomba niwe wazi. Nasema kwa dhati kabisa unyenyekevu wa Waziri Kalemani kwa kiasi kikubwa sana umefanikisha mapinduzi makubwa katika sekta ya kusambamba umeme nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hili kuweka rekodi katika Bunge lako Tukufu. Waziri huyu ukimpigia simu saa sita ya usiku lazima akupokelee na Waziri huyu ukimtumia ujumbe lazima akujibu. Kwetu sisi Wabunge kama kuna jambo linatupa faraja ni kuona namna tunahitaji kufanya mawasiliano na Mawaziri na wanakuwa wepesi katika kuitika. Kwa dhati ya moyo wangu, naomba nitumie Bunge lako kumpongeza sana Waziri Mheshimiwa Kalemani hili ameweza kulishinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nampongeza tena Waziri huyu Mheshimiwa Kalemani, juzi tuliona sintofahamu ikitokea katika Shirika letu la Umeme la TANESCO, LUKU zikaleta matatizo. Mimi kwa upande wangu nilihisi ni some sort ya sabotage kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi lakini nampongeza sana Waziri alichukua hatua za haraka za kuwasimamisha kazi watumishi wa TANESCO na Waziri Mkuu akaliunga hilo mkono kwa kuruhusu uchunguzi zaidi ufanyike, hilo tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, Rais wa Awamu ya Sita kwa muda mfupi na kwa haraka ameshasaini mkataba wa zaidi ya shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kuzalisha umeme mwingine kule Kigoma. Naipongeza sana Wizara na Serikali ya Awamu ya Sita kwa sababu changamoto zinazozungumzwa kwa watu wa Katavi ni wazi umeme utakaozalishwa sasa katika Mkoa wa Kigoma utaingizwa kwenye Gridi ya Taifa na utahudumia mikoa ambayo ilikuwa haipati umeme wa Gridi ya Taifa, kwa hilo pia tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa natoa pongezi kwa sababu wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi wamepata faraja. Waziri alipotoa namba za wakandarasi waliowapa kazi mimi nimepigiwa simu na mkandarasi anaitwa Central, nimepewa uhakika tutaanza kusambaziwa umeme katika vijiji vyote 34 kuanzia mwezi huu. Mheshimiwa Waziri tunakushukuru na tunakupongeza sana wewe na Serikali na tufikishie salamu hizi kwa Mheshimiwa Rais maana huenda tulidhani kwamba vijiji 2,000 vilivyoahidiwa na Serikali ya Serikali ya CCM kwenye uchaguzi uliopita vinaweza vikasuasua. Peleka pongezi kwa mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu ametutendea haki Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na wapiga kura wote kwa kuyaenzi na kuyashikilia yale mapambano yaliyoanzishwa na Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli katika suala zima la kusambaza umeme kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina taarifa Vijiji vyangu vya Mwaru, Mduguyu, Mlandala, Kaugeri, Mpungizi, Irisya, Munyu, Mwasutianga, Mtunduru, Kintandaa, Maswea, Jerumani na vingine vingi siwezi kuvitaja vinakwenda kuanza kuunganishiwa na umeme. Hapa mimi nasema, Mungu akinipa uzima mwaka 2025 nachukua, ninaweka waaa, kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kuiomba Wizara, Singida tuna mradi mkubwa wa kutengeneza umeme kwa kutumia upepo. Mradi huu umezungumzwa kwa muda mrefu, kaka yangu Mheshimiwa Kalemani unajua watu wa Singida tunakupenda pamoja na Naibu wako mdogo wangu Mheshimiwa Byabato, mdogo katika umri lakini kiongozi wangu kwa maana ni Naibu Waziri, nawaomba kabisa kwa niaba ya watu wa Singida…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Elibariki Kingu.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, oooh, naunga mkono hoja. (Makofi)